Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Kushoto: Mzee Bilal Rehani Waikela na Sheikh Ponda Issa Ponda nyumbani
kwa Mzee Waikela Tabora
Leo nilitembelewa na Mzee Bilal Rehani Waikela, mwasisi wa TANU Tabora 1955 na Katibu wa EAMWS Western Province kwa miaka mingi hadi ilipopigwa marufuku na serikali mwaka wa 1968 kupisha BAKWATA.
Mzee Waikela ndiye aliyenisaidia katika kuandika sehemu ya tatu ya kitabu cha Abdul Sykes kwa kunipa nyaraka halisi za barua, ''cutting,'' za magazeti na miniti za mikutano wakati wa kile kiichokuja kujulikana kama, ''Mgogoro wa EAMWS.''
Nyaraka hizi bila ya kuogopa vitisho alizificha kwa miaka 20 hadi alipozifikisha MSAUD katika miaka ya 1980 na kupitia MSAUD zikanifikia mimi.
Nyaraka hizi alimkabidhi Mohamed Lulengelule kijana kutoka Tabora aliyekuwa Mwenyekiti wa MSAUD.
Wenzake wengi waliokuwa katika uongozi wa EAMWS katika kipindi cha Mgogoro wa EAMWS kwa hofu ya kuwekwa kizuizini walizitia moto nyaraka zao.
Ukumbi wa H.H. Aga Khan, Girls School, 1963
Nyerere alitulia tuli pembeni mwa Rais wa Baraza la Tanganyika la EAMWS Tewa Said Tewa akimsikiliza Waikela.
Aliposimama kujibu hotuba ya Waikela Nyerere kwa upole alisisitiza msimamo wa serikali wa kutoa haki na usawa kwa raia wake wote.
Kwa kiasi fulani Nyerere alikuwa amefanikiwa kupunguza joto kati ya Waislam na serikali.
Hotuba ya Waikela na ya Nyerere zikapewa umuhimu mkubwa katika Tanganyika Radio Corporation (TBC).
Waislam wengi wakajitokeza stesheni ya gari moshi Tabora kuja kumpokea shujaa Waikela.
Alipewa heshima ile kwa kuwa na ujasiri wa kuweza kusimama kidete dhidi ya wale waliodhani kuwa wanaweza kuwakalia Waislam vichwani.
Mara ya kwanza nilipomsikia Mzee Waikela anahadithia haya yaliyotokea mwaka wa 1963 Ukumbi wa Aga Khan Girls School nilisisimkwa mwili mzima na malaika wakanisimama.
Ile hadhira ilikuwa kubwa na baadhi ya waalikwa siku zile katika mikutano ya EAMWS walikuwa mabalozi kutoka nchi za Kiislam...kisa kizima kipo katika kitabu cha Abdul Sykes.
(Nilifanya mahojiano haya mwaka wa 1987 nyumbani kwa Mzee Waikela, Gongoni, Tabora, nikiwa nimesindikizwa na marehemu Ilunga Hassan Kapungu na shemeji yake Salum Ali Mkangwa ambae alikuja baadae kufasiri kitabu hiki kwa Kiswahili mwaka wa 2002).
Hizi nyaraka zipo katika Maktaba ya MSAUD sasa inakimbilia miaka 40.
Huwezi kuchoka kumsikiiza Mzee Waikela kwa hakika ni hazina na ‘’Encyclopedia,’’ ya historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika.
Katika utafiti wangu ni Mzee Waikela na Hamza Aziz ndiyo watu wawili ambao Mufti Sheikh Hassan bin Ameir alipata kuwaombea dua maalum Allah awanusuru na shari zilizokuwa zimejikita katika siasa baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961.
Allah amzidishie umri mrefu na aimarishe afya yake.