Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
MZEE PIUS MSEKWA HAIFAHAMU HISTORIA YA TANU
Katika gazeti la Tazama la leo tarehe 14 Oktoba 2019 kuna makala iliyoandikwa na Pius Msekwa yenye kichwa cha habari, ‘’Mwalimu Nyerere kama nilivyomfahamu (2),’’ ambamo ameandika maneno haya yafuatayo kuhusu Mwalimu Nyerere kuwa:
‘’...alifanikiwa kuwaridhisha kwa nguvu za hoja zake, wanachama wa iliyokuwa asasi ya kupigania maslahi ya wafanyakazi wa Kiafrika katika Serikali ya Kikoloni, iliyokuwa inaitwa ‘’Tanganyika African Association’’ (TAA).
Alifanikiwa kuwashawishi wanachama wa asasi hiyo kukubali wenyewe kuvunja chama chao hicho, na badala yake kuunda chama kipya cha siasa cha, ‘’Tanganyika African National Union (TANU), mnamo mwezi Julai, 1954, ili kiwe chombo cha kisiasa cha kupigania uhuru wa Tanganyika.’’
Mzee Pius Msekwa amekosea hii si historia ya kweli ya TANU na kwa bahati mbaya Mzee Msekwa hakutaja majina ya hao walioshawishiwa na Nyerere, ‘’ kuvunja chama chao.’’
TAA hakikuwa chama cha kupigania maslahi ya wafanyakazi wa Kiafrika katika serikali ya kikoloni.
TAA kilikuwa chama cha Waafrika kikipigania maslahi zaidi ya hayo ya wafanyakazi na kilifika wakati kikawa kinakidhi mahitaji ya Waafrika wa Tanganyika kama chama cha siasa kisichokuwa na katiba ya siasa na kwa ajili hii kikawa kinagongana na serikali ya kikoloni TAA ikishutumiwa kuwa ilikuwa inajihusisha na siasa dhahiri.
Gavana Twining alipata kutoa Government Circular kadhaa kuionya TAA kati ya mwaka wa 1951 hadi 1953 kuhusu kujihusisha na siasa.
Mzee Msekwa anaweza kuanza kuisoma historia ya African Association kutoka kwa kalamu ya mmoja wa waasisi wa chama hicho Kleist Sykes aliyoiandika kabla ya kufariki mwaka wa 1949 na mswada huu ukawa mikononi kwa mwanae Abdulwahid Sykes hadi mwaka wa 1968 pale bint yake, Daisy alipoutoa hadharani akiwa mwanafunzi Chuo Kikuu Cha Afrika ya Mashariki, Dar es Salaam kama mada katika semina ya Idara ya Historia ya chuo hicho.
Wakati huo Daisy alikuwa mwanafunzi chini ya mwalimu bingwa wa historia ya Tanganyika, John Iliffe.
Matokeo ya mada hii ni sura katika kitabu alichohariri John Iliffe, (Daisy Sykes Buruku, ‘’The Townsman: Kleist Sykes’’ Moderm Tanzanians, Nairobi 1973, pp 95 – 114).
Laiti angesoma kitabu hiki Mzee Msekwa angeijua historia ya si tu TAA na TANU pia.
Hakuna popote katika sura hii ambamo imeelezwa kuwa TAA kilikuwa chama kinachopigania maslahi ya wafanyakazi wa serikali ya kikoloni.
Katika kitabu hiki anaweza pia kusoma maisha ya Hassan Suleiman na Ali Juma Ponda.
Hawa walikuwa viongozi wa TAA (''The Politicians Ali Ponda and Hassan Suleiman,'' pp. 227 – 253) na hakuna popote viongozi hawa walishughulika na maslahi ya wafanyakazi wa serikali wakiwa viongozi wa TAA.
Ningependa kuhitimisha nukta hii kwa kumfahamisha Mzee Msekwa kuwa huyu Abdul Sykes niliyemtaja hapa ni mtoto wa Kleist Sykes na ndiye baba yake Daisy alikuwa kiongozi wa TAA 1950 na ni mmoja wa wale wazalendo 17 walioasisi TANU mwaka wa 1954 na imesadifu kuwa nimeandika kitabu cha maisha yake, ‘’The Life and Times of Abdulwahid Sykes (1924 – 1954) The Untold Story of the Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika,’’ Minerva Press, London 1998.
Mzee Msekwa akipenda anaweza kuisoma historia ya TANU kutoka kwa wenyewe waliounda African Association 1929 na wakaja kuunda TANU 1954 kutoka TAA Abdul akiwa na mdogo wake Ally, Julius Nyerere, Dossa Aziz, John Rupia na wazalendo wengine kutoka katika majimbo ya Tanganyika kama Japhet Kirilo, Joseph Kimalando, Saadan Abdu Kandoro kwa kuwataja wachache.
Kuwa Nyerere ndiye aliyewashawishi wazalendo hawa kuunda TANU hii si kweli.
Ikiwa utasoma kitabu cha maisha ya Abdul Sykes utaona mle mabadiliko yaliyotokea ndani ya TAA kuanzia mwaka wa 1950 baada ya Mwalimu Thomas Plantan kama Rais wa TAA na Katibu wake Clement Mtamila kuondolewa madarakani kwa mapinduzi na uongozi wa TAA ukachukuliwa na Dr. Vedasto Kyaruzi kama Rais na Abdul Sykes Katibu.
Abdul Sykes alikuwa na fikra ya kuunda chama cha siasa toka yuko Burma wakati wa Vita Vya Pili Vya Dunia (1939 – 1945) na alipoingia katika uongozi wa TAA na kuwa mjumbe katika TAA Political Subcommitee ambao wajumbe wengine walikuwa: Dr. Vedasto Kyaruzi, Hamza Mwapachu, Mufti wa Tanganyika Sheikh Hassan bin Ameir, Sheikh Said Churembo, Steven Mhando na John Rupia na nia ya kuunda hii kamati ikiwa kuunda chama cha siasa.
Itamshangaza mtu yoyote kusikia kuwa Nyerere aliyepokelewa ndani ya TAA na Abdul Sykes 1952 tena wakati huo Abdul akiwa Kaimu Rais na Katibu TAA, iwe Nyerere ndiye aliyemshawishi Abdul na wenzake katika uongozi wa TAA ati wavunje TAA waunde TANU.
Mzee Msekwa anazungumza historia ambayo yeye haijui.
Ukweli ni kuwa kulikuwa na mazungumzo kabla na nyuma sana kati ya Abdul Sykes na Hamza Mwapachu kuhusu kuunda TANU na kudai uhuru wa Tanganyika.
Abdul alishaanza mazungumzo na Chief Kidaha Makwaia achaguliwe Rais wa TAA na mwaka unaofuatia TANU iundwe na Chief Kidaha aongoze harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.
Kuna mengi hapa hadi Nyerere akaja kuchaguliwa kuwa Rais wa TAA mwaka wa 1953 na Abdul Sykes akawa makamu wake katika uchaguzi uliofanyika Ukumbi wa Arnautoglo.
Kikao cha kumpa Nyerere uongozi wa TAA kilifanyika nyumbani kwa Hamza Mwapachu, Nansio Ukerewe katika miezi ya mwanzoni 1953 kati ya mwenyeji Hamza Mwapachu, Abdul Sykes na Ally Mwinyi Tambwe aliyekuwa Katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika) chama ambacho aliasisi baba yake Abdul mwaka wa 1933 na chama hiki ndicho kilichotoa wanachama na viongozi wa mwanzo wa TANU mwaka wa 1954.
Kwa kumalizia ningependa kumweleza Mzee Msekwa ni chama gani kilikuwa kinashughulika na maslahi ya wafanyakazi Waafrika katika serikali ya kikoloni.
Chama hiki hakikuwa TAA.
Chama kilichoshughulika na maslahi ya wafanyakazi Waafrika kilikuwa kinaitwa, ''Tanganyika African Government Servant Association (TAGSA).''
Chama hicho kiliasisiwa mwaka wa 1927 kwa lengo la kuendeleza maelewano mazuri baina ya serikali ya Malkia na watumishi wake Waafrika ili kuboresha huduma na kuendeleza maslahi na ustawi wa waajiriwa Waafrika.
Katika kipindi hiki cha mwanzoni mwa mwaka wa 1950 viongozi wa TAGSA walikuwa Thomas Marealle kama Rais na Ally Sykes Katibu.
Rashid Kawawa, Dr. Wibard Mwanjisi, Steven Mhando, Dr. Michael Lugazi walikuwa wanakamati na hawa wote walihusika sana katika kuunda TANU na wakiishi na fikra ya kuunda chama cha siasa kudai uhuru wa Tanganyika wala hawajasikia jina la Julius Nyerere.
Huu ndiyo ukweli wa historia ya TANU.