Josh Michael
JF-Expert Member
- Jun 12, 2009
- 2,523
- 87
- ASEMA WALIOJIPENYEZA MADARAKANI, SASA WANAUMBUKA
RAIS mstaafu, Ali Hassan Mwinyi amelipua kombora jingine kwa viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi, akisema kuwa walijipenyeza kwa bahati mbaya kushika uongozi, lakini sasa wanahaha.
Mwinyi anaongoza kamati ya watu watatu iliyoundwa na Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kuchunguza chanzo cha wanachama na viongozi wa chama hicho tawala kuchukiana kiasi cha kurushiana maneno makali wakati wa kikao hicho na kupendekeza hatua za kuchukuliwa.
Maneno hayo makali yalitokana na baadhi ya wanachama kutaka kulinyamazisha kundi ambalo limekuwa likijinadi kuwa linaongoza vita dhidi ya ufisadi ambayo watuhumiwa wa ufisadi waliitafsiri kuwa inakichafua chama na serikali yake.
Lakini jana Mwinyi alirusha maneno makali dhidi ya watuhumiwa hao wa ufisadi, akisema wameshikwa pabaya.
Mwinyi, ambaye aliongoza serikali ya awamu ya pili iliyoruhusu mabadiliko makubwa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi kiasi cha kupewa jina la Mzee Ruksa, alisema viongozi hao sasa wanafedheheka kutokana na kushikwa pabaya.
Ingawa hakutaka kufafanua alikuwa na maana gani, Mzee Mwinyi, ambaye alikuwa akizungumza kwenye kijiji cha Ndungu wilayani Same ambako alialikwa kuzindua wodi ya wazazi, alisema watu hao sasa wako kwenye wakati mgumu.
Mwinyi hakutaja majina ya viongozi ambao wameshikwa pabaya lakini katika siku za karibuni baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara na maofisa waandamizi wa Benki Kuu (BoT) wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali ya ufisadi, ikiwa ni pamoja na kutumia madaraka vibaya na kuisababishia hasara serikali, wizi na njama za wizi wa fedha za umma.
Kundi la watu hao limekuwa likisakamwa na wapiganaji hao wa vita ya ufisadi ambao wanataka viongozi wengi zaidi wafikishwe mbele ya sheria kujibu tuhuma zinazowakabili.
Mwinyi alilazimika kutoa kauli hiyo baada ya mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, ambaye ni mmoja wa vinara wa vita ya ufisadi, kububujikwa na machozi kuonyesha jinsi anavyokerwa na tatizo la ufisadi nchini huku akiapa kuendeleza vita hiyo.
Mwinyi alisema Kilango amekuwa akikerwa na tatizo hilo kwa kuwa anaguswa sana na maendeleo ya wananchi.
"Hakuna mwenye shaka na uzuri na usafi wa uongozi wa Kilango... kiongozi mzuri lazima awe na sifa 10 ikiwamo huruma na hiyo ndiyo iliyomfanya Mama Kilango alie leo kuelezea machungu aliyonayo," alisema.
"Ndio maana unamuona Mama Kilango anabwata kule Bungeni kwa nguvu zake zote akiona kuna dalili za uhaini ambao utawapokonya watu wake maendeleo... anasema sikubali na nyote mnafahamu."
Akizungumza katika sherehe hizo Mzee Mwinyi alimwelezea Kilango kama kiongozi wa kweli mwenye kipawa adimu cha kuongoza Watanzania katika misingi ya uadilifu.
"Aliyekosa kipawa hicho hawi kiongozi mzuri... na kiongozi wa namna hiyo akijipenyeza kwa bahati mbaya ndio hao wanaofedheheka ni waliofanya ufisadi na sasa wameshikwa," alisema Mwinyi.
Alisema ufisadi si wa wana-CCM, lakini hutokea mmoja au wawili kama vile chuya isivyoweza kukosekana katika mchele mwingi na hiyo huwa ni hila ya chuya na si ya mchele wenyewe.
Kwa mujibu wa mzee Mwinyi, CCM na wanachama wake ni safi na kusisitiza kuwa uongozi ni fani na kipawa na kiongozi mwenye vitu hivyo viwili hajifichi kama ilivyo kwa Kilango.
Huku akitumia maneno ya "asante sana", "hongera sana" na "heko mama Kilango" kuonyesha anavyounga mkono msimamo wa mbunge huyo, Rais Mwinyi alimwelezea mbunge huyo wa Same Mashariki kuwa ni mtu anayeguswa na maendeleo ya Watanzania.
Kilango, ambaye alikuwa kimya kwa muda mrefu tangu Nec imalize kikao kilichoonekana kutaka kuwafumba midomo vinara wa vita ya ufisadi, alibubujikwa machozi alipokuwa akiwahutubia wananchi waliofurika katika sherehe za uzinduzi wa wodi hiyo.
Akizungumza kwa hisia kali, Kilango alisema hakuna jambo linalomuuma kama kuona kiongozi aliyechaguliwa na wananchi ili awatetee, anawageuka na kuwa mla rushwa na kuwaumiza wananchi waliomchagua.
Mbunge huyo aliapa kupambana na mafisadi na wala rushwa hadi kifo na akawataka wananchi wasidanganywe kuwa CCM inakumbatia rushwa.
"Msidanganywe na watu kuwa CCM inakumbatia wala rushwa, hiyo si kweli hata kidogo mimi ni mbunge wenu wa CCM na siku zote nitapambana na rushwa na siku zote sijawahi kwenda nje ya katiba ya CCM," alisema Kilango.
Kilango, ambaye ni mke wa waziri mkuu wa zamani na mbunge wa jimbo la Mtera John Samuel Malecela, alisema kiapo cha CCM inatambua kuwa rushwa ni adui wa haki na ndio maana mwanachama ni lazima aape kuwa hatatoa wala kupokea rushwa wala kutumia cheo chake au cha mtu mwingine kwa maslahi binafsi.
Mwinyi alitumia mkutano kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Same Mashariki kwa kupata kiongozi mwenye sifa kamili za uongozi kama Mama Kilango na akazitekeleza kwa ukamilifu bila ubaguzi wa rangi, dini, kujuana au jinsia.
Awali akitoa taarifa ya ukarabati wa wodi ya wazazi na watoto ambayo imekarabatiwa kwa kiwango cha juu, mganga mkuu wa wilaya ya Same, Dk Charles Kifunta alisema ukarabati huo umegharimu Sh75 milioni.
Katika mradi huo ambao wananchi wa Ndungu walishirikishwa kwa asilimia 100, nguvu za wananchi ni sawa na Sh5 Milioni na fedha nyingine zilitolewa na Mama Kilango kupitia akaunti ya maendeleo.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi wa serikali, akiwemo mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Monica Mbega, mkuu wa wilaya ya Mwanga na kaimu mkuu wa wilaya ya Same, Athman Mdoe.
Ingawa kauli za Mwinyi hazikuwa wazi, wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema ziliashiria kumuunga mkono Kilango na wabunge wenzake katika mapambano dhidi ya ufisadi.
Wabunge wengine ambao tayari wameapa kula sahani moja na mafisadi ni pamoja na mbunge wa Urambo Mashariki ambaye pia ni spika wa Bunge la Jamhuri, Samuel Sita na mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro.
Wengine wanaotajwa katika orodha ya wabunge hao ni pamoja na Lucas Selelii wa Nzega, Dk. Harrison Mwakyembe wa Kyela.