Nadhiri isiyo takatifu

Nadhiri isiyo takatifu

Joined
Oct 5, 2015
Posts
90
Reaction score
482
NADHIRI ISIYO TAKATIFU

|Umuhimu wa kutunza kumbukumbu na umuhimu wa teknolojia katika uchunguzi wa matukio ya uhalifu.

Kitabu: Istilahi Za Uhalifu Na Usalama: Sura ya 4: uk. 77
images (24).jpeg
aviary-image-1576429510266.jpeg

Na. Dr. Chris Cyrilo

Somo simulizi
Miongo miwili baada ya Adolf Hitler kuiingiza Ulaya katika vita kuu ya pili ya dunia, kiongozi mkubwa wa dini huko nchini Marekani alijikuta kwenye hali ya sintofahamu, jina lake Askofu Valerian Trifa. Muhamiaji huyo kutoka Romania alikuwa mtu mwenye historia ya siri, alihusika katika mauaji ya mamia ya wayahudi wakati wa vita kuu ya pili ya dunia. Lakini Askofu Trifa alikana tuhuma hizo. Ili kupata uhakika wa taarifa hizo, serikali ya Marekani ilianza kufanya kazi ya kuutafuta na kuubaini ukweli kwa njia za kisayansi.

Ilikuwa wazi kwamba mwaka 1950, muhamiaji kutoka Romania aliyeitwa Viorel D. Trifa alisafiri kutoka Ulaya hadi nchini Marekani kutafuta maisha mapya. Viorel D. Trifa aliwaambia maofisa wa uhamiaji kwamba yeye alikuwa mwathirika wa vita ya pili ya dunia. Aliendelea kusema kuwa alipokuwa Romania alichukuliwa mateka na askari wa jeshi Ujerumani na kupelekwa kwenye makambi ya wakimbizi walipokuwa wakiuawa watu wengi, lakini yeye alibahatika kutoroka. Kisha baada ya vita, kama ilivyo kwa mamia elfu ya waathirika wengine, naye aliamua kuhamia marekani kwa mujibu wa sheria ya watu waliokosa mahali pa kuishi kutokana na uharibifu mkubwa uliotokea wakati wa vita.

Sheria hiyo iliitwa ‘Displaced Persons Acts’, ilitungwa na bunge la marekani na kutiwa sahihi na Rais Harry S. Truman mnamo mwaka 1948, kwa lengo la kuwasaidia waathirika wa vita waliokosa makazi, hasa wale waliokuwa kwenye makambi ya halaiki.
Katika Nyaraka alizojaza wakati wa kuomba kuingia nchini Marekani, Trifa alijitambulisha kama mtu aliyekuwa mfungwa wa kisiasa, aliyekamatwa na askari wa siri wa Ujerumani wa wakati huo, maarufu kama Gestapo. Mwaka 1957, Viorel Trifa alipatiwa uraia wa Marekani. Akiwa Romania, Trifa alikuwa muumini mzuri na mtu wa karibu wa kanisa la Orthodox la Romania, na alipoingia nchini Marekani aliendelea kuwa muumini na kujiongezea elimu ya dini, na muda mchache baadaye akapanda daraja na kuwa Padre. Kisha alipanda ngazi za uongozi wa kanisa haraka, na hatimaye akawa Askofu mkuu wa Dayosisi ya Detroit na kutwaa jina la kidini la Valerian.

Punde, wingu la wasiwasi lilianza kutanda. Baadhi ya waumini wa kanisa la Orthodox waliokuwa wahamiaji kutoka Romania walihisi wanamfahamu Askofu Trifa tangu ujana wake akiwa huko Romania. Waumini walisema Trifa alikuwa mfuasi mtiifu wa Adolf Hitler na zaidi alikuwa kiongozi wa kikosi kilichoitwa ‘Iron Guard’, kilichokuwa na ufuasi wa utawala wa Nazi. ‘Iron Guard’ lilikuwa kundi kubwa, lenye ukatili mkubwa na lenye chuki dhidi ya wayahudi ndani ya Romania. Mwanzoni mwa vita kuu ya pili, kundi la ‘Iron Guard’ lilitumia sare na salamu za chama cha Nazi cha Adolf Hitler wa Ujerumani. Mtu aliyeitwa Viorel D Trifa alikuwa kiongozi wa kundi hilo.

Askofu mkuu Valerian Trifa alikataa tuhuma hizo. Endapo tuhuma hizo zilikuwa za kweli ilimaanisha mambo mawili yasiopendeza. Moja ni kuwa Askofu Trifa alighushi taarifa za uhamiaji wakati akiingia nchini Marekani. Pili ni kuwa kiongozi mkubwa wa dini ndani ya Marekani alikuwa muhalifu wa kivita.

Waumini wenye asili ya Romania wa kanisa la Orthodox nchini Marekani waliendelea kuamini kuwa Valerian Trifa, Askofu mkuu wa Dayosisi ya Detroit ndiye Viorel D. Trifa aliyekuwa kiongozi wa ‘Iron Guard ‘huko nchini Romania.

Januari 20, 1941, Trifa alitoa hotuba ya kuhamasisha chuki na mauaji dhidi ya wayahudi kupitia redio moja mjini Bucharest, mji mkuu wa Romania. Siku iliyofuata baada ya hotuba hiyo, wafuasi wa kundi la ‘Iron Guard’ walifanya mauaji ya wayahudi kwa maelfu. Kwanza wayahudi walitafutwa na kukusanywa pamoja kwa nguvu ya kundi la ‘Iron Guard’, kisha walipakiwa kwenye magari na kusafirishwa hadi kwenye ‘mabucha’. Huko walilazimishwa kuvua nguo, kulala chini na kuchinjwa kwa kuanzia kooni, mfano wa wayahudi wanavyochinja mifugo wakati wa maadhimisho ya sikukuu zao.
Taarifa zaidi kutoka kwa waumini zilisema kuwa Vorel Trifa, pamoja na kuwa kiongozi wa ‘Iron Guard’ pia alikuwa mhariri wa gazeti la Libertate, ambalo lilitangaza propaganda za chuki dhidi ya wayahudi. Chuki na ukatili dhidi ya wayahudi yalikuwa mambo yalioruhusiwa, na zaidi ya hapo, yalihamasishwa.

Serikali ya Marekani ilijikuta njia panda kuhusu tuhuma hizo dhidi ya Askofu Trifa. Je! Kulikuwa na namna ya kupata uhakika kwamba Askofu Valerian Trifa ndiye Viorel D Trifa aliyekuwa kiongozi wa ‘Iron Guard’ huko nchini Romania? Ushahidi pekee ulikuwa kumbukumbu za wahamiaji wenzake kutoka Romania, lakini huo sio ushahidi wa kisayansi. Ilikuwa ni vigumu sana kutafuta ushahidi wa kisayansi wa matukio ya miaka karibu 20 iliyopita, hivyo jambo hilo likaanza kupoteza umaarufu.

Mtu mmoja, naye muhamiaji kutoka Romania, Daktari bingwa wa meno aliyeitwa Charles Kremar hakukubali jambo hilo lipotelee hewani. Dr. Kremar alikuwa muhanga wa vita kuu ya pili ambaye ndugu zake waliuawa na kikundi cha ‘Iron Guard’, hivyo alitamani kuona Askofu Trifa anahukumiwa kadiri inavyostahili. Kwa karibu miaka 20 mingine, Dr. Kremar alikuwa akiishawishi serikali ya marekani kufanya uchunguzi wa jambo hilo. Na mwaka 1973, mahakama nchini marekani ilianza rasmi kufanya uchunguzi ili kubaini endapo Askofu Trifa ndio mtu aliyekuwa kiongozi wa Iron Guard, aliyeua na kuhamasisha mauaji ya maelfu ya wayahudi wakati wa vita kuu ya pili. Maofisa wa idara ya mahakama wa Marekani waliomba msaada kwa serikali ya Ujerumani ambayo ilikuwa imetunza maelefu ya rekodi zinazohusu vita kuu ya pili ya dunia. Katika kupitia nyaraka moja baada ya nyingine, maofisa hao walikuta nyaraka zilizoandikwa na mtu anayeitwa Trifa, aliyekuwa mfuasi wa ‘Iron Guard’. Jambo la kushangaza ni kuwa nyaraka hizo zilikuwa miongoni mwa nyaraka chache ambazo hazikuwa zimehifadhiwa mahali maalumu, kwa sababu hazikueleweka ziwekwe kundi gani. Nyaraka nyingi zilihifadhiwa kwa mpangilio wa makundi maalumu kulingana na aina ya nyaraka husika.

Nyaraka hizo zilizoandikwa na mtu aitwaye Trifa zilikuwa zikieleza mambo ya kawaida tu. Zilieleza ratiba za kazi, kutazama filamu, hali ya hewa na mambo mengi ya kawaida. Maofisa walijiridhisha kuwa mtu aliyeandika nyaraka hizo alikuwa na maisha mazuri ya amani, asiye na wasiwasi na kesho yake ingawa ilikuwa wakati wa vita. Nyaraka hizo zilikuwa na sahihi ya mtu aliyeitwa Viorel Trifa. Swali lilibaki kuwa, Je! Viorel Trifa ndiye askofu mkuu Valerian Trifa? Wanasayansi wa sanaa ya uchunguzi wa uhalifu walitafuta namna ya kujua endapo mtu aliyeandika na kutia sahihi nyaraka hizo alikuwa Askofu Trifa.

Mwanasayansi Gideon Epstein, mtaalamu wa alama na miandiko ya mikono alikabidhiwa nyaraka 22 zilizoandikwa kwa mkono na Viorel Trifa, ili kufanya uchunguzi na kubaini endapo muandiko huo ndio muandiko wa Askofu Valerian Trifa.

Kila mtu ana muandiko wake tofauti, hata mapacha wanaofanana huandika tofauti. Muandiko ni zao la mifumo mingi ya mwili, ikiwemo mifumo ya fahamu, misuli na mifupa ya mikono na vidole inayoshirikiana kwa pamoja na kutoa kitu cha kipekee ambacho ni tofauti kati ya mtu mmoja na mwengine.

Gideon Epstein alitumia miezi kadhaa kufanya upembuzi wake. Alifanya kulinganisha sahihi zilizopo kwenye nyaraka zilizotoka ujerumani na sahihi za Askofu Valerian Trifa zilizoptikana kwenye kumbukumbu za kanisa. Katika sanaa ya uchungzui wa miandiko, mwanasayansi hutumia mbinu mbalimbali kulinganisha muandiko wa mtu anayejulikana na ule wa mtu asiyejulikana ili kubaini endapo anayejulikana ndiye huyo asiyejulikana au ni watu tofauti. Kasi ya kuandika, aina za maneno anayotumia mwandishi, nafasi kati ya neno na neno, herufi na herufi, mstari kwa mstari, uundwaji wa herufi na namna zinavyounganishwa, nguvu ya mgandamizo wa kalamu, na mambo mengine mengi huzingatiwa wakati wa kulinganisha miandiko. Baada ya miezi kadhaa ya upembuzi, mwanasayansi Gideon Epstein alitoa kauli;

‘Hakuna shaka kuwa mwandiko katika nyaraka zilizotoka ujerumani ni muandiko wa Askofu Valerian Trifa’

Askofu Trifa alipinga matokeo hayo. Hata hivyo bado maofisa wa idara ya mahakama nchini marekani walikuwa na kigugumizi. Ushahidi uliopo ni ule wa kulinganisha muandiko pamoja na kumbukumbu za watu za matukio ya miaka 30 iliyopita. Je! Ushahidi huo ulitosha kumtia Askofu Trifa hatiani? Hapana.

Katika kupekua zaidi, nyaraka moja ilionesha anuani ya mwandishi, na chini ya anuani hiyo kulikuwa na alama zingine zisizoonekana vema. Wachunguzi walihisi ni alama za vidole ambazo kwa sababu ya kupita muda mrefu zilianza kufutika. Maofisa wa marekani waliomba tena msaada kutoka Ujerumani, wakitaka kadi halisi za posta (stamps) zilizotumiwa wakati Viorel Trifa akituma nyaraka zile, lakini maofisa wa ujerumani walikataa kwa sababu hawakutaka kadi zile ziharibiwe. Poda maalumu zinazotumika kwa ajili ya kusafishia kadi ili kupata kwa urahisi alama za vidole, ingeharibu kadi mara tu baada ya kutumika. Wajerumani hawakutaka kuharibu kadi zile kwa sababu ni kumbukumbu muhimu. Jambo hilo lilisababisha kesi kusimama kwa miaka kadhaa.

Mwishoni mwa miaka ya 1970 watafiti wa sayansi ya uchunguzi waligundua kuwa miale ya mwanga mkali aina ya ‘Laser’, inaweza kung’arisha eneo fulani na kufanya alama zisizoonekana kwa macho zionekane vema. Kwahiyo, iliwezekana sasa kutumia miale ya ‘Laser’ kuweza kuona alama za vidole kwenye kadi za posta bila kuziharibu kadi hizo kwa kutumia poda. Mwaka 1982, maofisa wa Ujerumani wakisindikizwa na wanausalama wa Marekani walisafirisha kadi za posta hadi makao makuu ya shirika la FBI, mjini Washington DC kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi kwa teknolojia ya Laser. Wakati huo teknolojia hiyo ilikuwa ni siri ya nchi, au ‘Classified Technology’ na kwa hiyo maofisa wa Ujerumani hawakuruhusiwa kuingia na kuona mashine hiyo ya ‘Laser’.

Pamoja na teknolojia hiyo, bado kulikuwa na changamoto. Wachunguzi hawakuwa na uhakika endapo kadi zile za posta zina alama za siri, kwanza kwa sababu muda mrefu ulikuwa umepita, pili kwa sababu haikujilikana kama zina alama za vidole. Mwishoni mwa mwaka 1982, uchunguzi wa kesi ya Valerian Trifa, Askofu mkuu wa Dayosisi ya Detroit ulipamba moto. Waendesha mashitaka wa Marekani walimtuhumu Askofu Trifa kwa mauaji na kushawishi mauaji ya maelfu ya wayahudi yaliyofanywa na kikundi cha Iron Guard huko nchini Romania wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Askofu Trifa aliendelea kupinga madai hayo kwa kusema kuwa, wachunguzi hao walimlenga mtu ambaye siye. Askofu alidai kuwa Trifa wa Romania si Trifa wa Marekani. Lakini kadi moja ya posta iliyotumwa mwaka 1942 kutoka Romania kwenda Ujerumani ilipatikana na alama za vidole.

Wanasayansi katika maabara ya uchunguzi huko Marekani walitumia miwani maalum yenye uwezo mkubwa wa kutofautisha rangi na maumbo ya vitu. Kisha wakazima na kuziba vyanzo vyote vya mwanga ndani ya maabara na kubakiza mwanga wa ‘Laser’ pekee. Ndipo ilipopatikana picha halisi ya alama za vidole iliyokuwapo kwenye kadi ya posta kwa miaka 40 iliyopita, walipiga picha alama zile, kisha zikalinganishwa na alama za vidole za Askofu Valerian Trifa, zilizokuwapo katika nyaraka za uhamiaji. Alama zilifanana kwa silimia 100. Alama hizo za vidole za Askofu Trifa zilizodumu kwa miaka 40 ndiyo alama za kale zaidi kuwahi kugundulika na kulinganishwa duniani kote. Teknolojia ya ‘Laser’ ikawa yenye mafanikio makubwa. Wachunguzi waliamini kwamba, wakati Viorel Trifa akiandika kadi ile ya posta, kwa kutumia kalamu za wakati huo zenye wino wa mafuta, kidole chake gumba cha kushoto, chenye mafuta kiliacha kwa bahati mbaya alama kwenye upande mwingine wa kadi. Ingawa muda mrefu ulipita na mafuta yale kukauka na kufanya alama zisionekane kwa macho, lakini teknolojia ya mwanga aina ya ‘Laser light’ iliweza kuona alama zile.

Alipotaarifiwa kuhusu kufanana kwa alama zake za vidole, Askofu Trifa hakuwa na cha kusema, alijiuzulu na kuamua kujivua uraia wa Marekani. Haki iliyosubiriwa kwa miaka 40 miongoni mwa raia wa Romania pamoja na Dr. Kremar ilipatikana. Ndugu na jamaa wengi wa Romania walipoteza maisha mikononi mwa kikundi cha Iron Guard kilichoongozwa na Viorel D. Trifa, aambaye baadaye alijiita Valerian Trifa, akajificha nyuma ya madhabau hadi kuwa Askofu mkuu wa kanisa la Orthodox katika Dayosisi ya Detroit.

Ndani ya Marekani hakukuwa na adhabu ya kumpatia Askofu Trifa kwa makosa aliyofanya wakati wa vita isipouwa lengo hasa lilikuwa kutafuta kujua yaliyofichika. Baada ya kujivua uraia aliendelea kuishi Marekani kwa muda wa miaka miwili, kusiwe na Taifa duniani lilokubali kumpokea Askofu Trifa. Lakini mwaka 1984, Ureno waliamua kumpokea na kumpa uraia. Mtu aliyeishi ujana wake kwa ukatili mkubwa dhidi ya binadamu, kisha akaamua kujificha katika madhabahu ya kanisa, alimalizia muda wa maisha yake akitengwa na dunia. Januari 28, 1987, Viorel ‘Valerian’ Trifa alifariki dunia kwa shambulio la moyo huko mjini Cascais, Ureno.

‘Ni karatasi tu. Waathirika walikufa lakini karatasi hazikufa. Karatasi zenye alama na zisizo na alama zimefanya uchunguzi huu kuwa wa maana’. Alimalizia mwendesha mashitaka – Eli M. Rosxenbaum.

"Binadamu wote ni sawa, binadamu wote ni wahalifu"
 
Bavicha wameamua kuandika upuuzi usio na faida wapate hela ya kula. Mmbwa nyie na bado.
 
Bavicha wameamua kuandika upuuzi usio na faida wapate hela ya kula. Mmbwa nyie na bado.
sijui Kama wewe ni mzee au kijana kwa sababu unatumia 'avatar' , na sina shahuku wala hamu ya kukujua upo wapi. Lakini nikujulishe, Mimi ni Daktari niliyehitimu chuo kikuu cha afya na sayansi shirikishi Muhimbili.
 
Back
Top Bottom