SoC02 Nafasi ya Kiswahili

SoC02 Nafasi ya Kiswahili

Stories of Change - 2022 Competition

Shida Masuba

Member
Joined
May 30, 2016
Posts
6
Reaction score
4
Kiswahili ni nini?

Kiswahili ni lugha ya Kibantu yenye asili ya ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi katika bara la Afrika.

Kiswahili ni lugha yenye mawanda mapana kimatumizi na katika mwendo wake. Lugha hii ina nafasi nyingi kitaifa, kikanda na kiulimwengu.

Katika makala haya tutaangazia nafasi ya lugha ya Kiswahili, umuhimu wake, changamoto na na nini kifanyike ili kupanua wigo zaidi kuhusu matumizi na mweneo wa Kiswahili.

1. 0 Nafasi ya Kiswahili

1.1 Nafasi ya Kiswahili Kitaifa nchini Tanzania

Kiswahili nchini Tanzania ni lugha yenye hadhi kuu Tatu:

I. Lugha ya Taifa: hii ni lugha ambayo hutumiwa na raia, viongozi hata wageni wawapo ndani ya taifa la Tanzania katika mawasiliano ya kila siku. Lugha hii hutumiwa katika shughuli za kisiasa, kiutawala, kibiashara, kidini, za uandishi wa habari na utangazaji, na shughuli nyingine za kijamii kama sherehe za harusi, matangazo misibani nk. Hii imechochea lugha ya Kiswahili kuzidi kuenea zaidi na zaidi nchini, kutoka vizazi hadi vizazi.

II. Lugha rasmi: nchini Tanzania Kiswahili ni lugha rasmi ambayo hutumika katika kuandaa nyaraka mbali mbali katika taasisi na jumuiya za kiserikali na zisizo za kiserikali. Kwa mfano katiba ya nchi ipo katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza, Sera ya lugha ipo katika Kiswahili na Kiingereza. Sanjari na hilo nyaraka za benki (fomu) ziko katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza. Utajiuliza ni kwa nini lugha ya Kiswahili itumike? Ukweli ni kwamba lugha ya Kiswahili ni lugha rasmi katika uandaji wa nyaraka zinazohusu taifa la Tanzania.

III. Lugha ya Kufundishia: lugha ya Kiswahili nchini Tanzania ni lugha ya kufundishia elimu ya awali mpaka shule za msingi, astashahada ya ualimu, na kuwa somo katika ngazi ya sekondari na vyuoni.

1.2 Nafasi ya Kiswahili Kikanda

Lugha ya Kiswahili inazungumzwa katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo nchi za Tanzania, Kenya, Uganda ndiyo vinara wa kutumia Kiswahili wakifuatiwa na DRC, Rwanda na Burundi, nchi nyingine zinazozidi kupiga hatua katika kuhakikisha wanaifaidi lugha hii ni Botswana, Ghana, Namibia, Afrika Kusini, Sudan, Somalia, Sudan Kusini nk. Wengine walianza muda mrefu kufundisha katika vyuo vikuu vya nchi zao, na wengine wameruhusu Kiswahili kifundishwe ngazi ya msingi mfano Afrika Kusini. Uganda ikianza kuitambulisha lugha ya Kiswahili kama lugha ya mawasiliano na kufundishia katika elimu ya msingi, huku Kenya ikiitumia kama lugha ya taifa lao. Rwanda hawajabaki nyuma bali wameiongeza lugha ya Kiswahili kama lugha ya mawasiliano nchini mwao na kuifundisha pia katika chuo kikuu cha Kigali. Haya ni mafanikio makubwa sana kwa ukuaji na ueneaji wa Kiswahili katika ukanda za Afrika. Tunathubutu kusema Kiswahili kinapasua anga za Kikanda kwa kasi kubwa mno. Julius Malema ni balozi mzuri wa kuhubiri ufundishaji wa Kiswahili katika nchi za Afrika ili tuwe na lugha yenye asili ya Afrika itakayounganisha Waafrika wote.

Aidha tunaona jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika unahamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mawasiliano wakutanapo, iwe kipaumbele cha kuhakikisha Kiswahili kinakuwa lugha ya mawasiliano. Kwa upande wa jumuiya ya Afrika Mashariki ni lugha inayotumika hadi kwenye nyaraka zao za kiofisi na kiutawala.

1.3 Nafasi ya Kiswahili Kimataifa/Kiulimwengu

Kiswahili ni lugha yenye msambao mkubwa ulimwenguni baina ya lugha zenye asili ya Afrika. Nchi mbali mbali hufundisha Kiswahili na watumiaji wenye asili ya nchi hizo huzungumza Kiswahili, mataifa ni mengi yanayojibidisha kutafuta maarifa ya Kiswahili. Miongoni mwa mataifa hayo ni pamoja na Marekani, Japan, China, Uingereza, Ujerumani, Ufini nk.

Kubwa kuliko ni kwamba umoja wa Mataifa umeitambua lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya Taifa la Tanzania na kufanya lugha ya 7 katika lugha zinazotambuliwa na umoja wa mataifa. Hivyo Lugha ya Kiswahili inaungana na lugha za Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kirusi, Kihispaniola, na Kiarabu. Ni furaha ilioje kwetu wanaisimu wapangalugha kongoo, kwani wapangalugha kihadhi wametukonga nyoyo zetu.

Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO),halijaishia kuutambua tu bali na kuiwekea siku maalumu ya kuiadhimisha lugha ya Kiswahili duniani ambayo ni tarehe 7/7 kila mwaka. Haya ni mambo matamu kwa lugha ya Kiswahili katika USO wa ulimwengu.

2.0 Umuhimu wa Lugha ya Kiswahili

1. Lugha ya Kiswahili ni kiunganishi baina ya watanzania, waafrika na watu mbali mbali ulimwenguni. Huchagiza amani na upendo baina ya wanajamii. Kwa sababu ya kutumika kama lugha ya mawasiliano katika mataifa mbali mbali mfano Tanzania, Kenya nk. Sanjari na hilo lugha hii huwaweka pamoja wakubwa na wadogo, vijana na wazee, matajiri na masikini kwa sababu haina ubaguzi kwa kutofautisha matabaka katika utumiaji wake.

2. Kiswahili ni lugha ya kibiashara au kiuchumi, katika Masoko na katika mitandao ya kijamii. Zaidi imekuwa lugha ya kibiashara katika ngamizi, mifumo ya simu, na mawasiliano ya kiteknolojia.

3. Kiswahili ni lugha ya kupashana habari baina ya jamii na jamii, taifa na Taifa ulimwengu. Vyombo vya habari Kama BBC Swahili, DW, CRI Sauti ya Amerika, vyombo vya habari vya Tanzania, Kenya nk vinarusha matangazo yao na habari zao kwa lugha ya Kiswahili ili kutuhabarisha matukio mbali mbali yaliyojiri kwenye kona za ulimwengu.

5. Kiswahili ni lugha ya kutolea elimu na kuhawilisha maarifa kutoka kwa walimu kwenda kwa wanafunzi hasa katika mataifa ya Afrika Mashariki. Kwa mfano elimu ya awali na msingi nchini Tanzania, Kiswahili hufundishwa na kuzalisha wataalamu wake kuanzia ngazi ya astashahada mpaka shahada ya Uzamivu.

6. Lugha ya Kiswahili imefumbata maarifa, utamaduni, mila na desturi za Watanzania na Wa Afrika kwa ujumla. Utaniuliza kivipi? Nami nakujibu, majina ya vitu, falsafa ya Kiswahili, muundo wa lugha ya Kiswahili ni kiwakilishi cha miundo ya lugha za Afrika za Kibantu. Utamaduni wa Kiswahili ndiyo unajitokeza katika jamii nyingine za Kiafrika. Mfumo wa familia, makuzi, misemo, nahau, methali na mengine mengi husadifu maisha ya waafrika kwa ujumla.

3.0 Changamoto katika ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili

Jambo lolote jema halikosi ukinzani katika kulitekeleza. Kiswahili kinakumbana na misukosuko katika ukuaji wake na kuenea kwake kadiri lugha hii inavyopanua mawanda yake kimatumizi na kiueneaji. Changamoto hizo ni kama ifuatavyo:

1. Wazawa: wazawa wengi wa Kiafrika hususani wa Tanzania wana mtazamo hasi au potofu juu ya lugha ya Kiswahili, wakifikiri ukizungumza Kiswahili ni ushamba, jambo ambalo si kweli. Wanapenda kutukuza na kukuza Kiingereza wakidhani ndiyo kuwa bora zaidi.

Wazawa wa kwanza ni wale ambao hata shule hawakwenda lakini hulazimisha kutumia Kiingereza na matokeo yake huzungumza sarufi isiyo sahihi. Lakini wangelitumia Kiswahili wangezungumza vyema zaidi na kueleweka vyema. Kwa mfano utamsikia mtu anasema

"My wangu"

wakati neno "my" lina maana ya "wangu" wanasababisha uziada bileshi usio wa msingi katika matumizi ya lugha.

Wazawa wa pili ni wasomi ambao imani yao ni kwamba ukizungumza Kiswahili utaonekana haujasoma, hivyo ili uonekane msomi lazima uzungumze Kiingereza jambo ambalo si kweli. Tunajiuliza mbona Wachina hawazungumzi Kiingereza lakini wahandisi na wanasayansi wazuri na tunawapa tenda za kutujengea miundombinu kwa Kichina chao. Kumbe usomi ni maarifa na si lugha uitumiayo.

Hivyo wasomi tubadilike na kuheshimu vyetu, hatujiulizi kwa nini waingereza wakazane Kujifunza na kufundishana Kiswahili ikiwa ni lugha dhaifu? Ukweli ni kwamba lugha kama utambulisho wa mtu na jamii, hubeba siri za jamii inayohusika na lugha hiyo.

2. Uelewa mdogo kuhusu lugha na Msamiati

Watu wengi waliosoma huamini kuwa lugha ya Kiswahili ina uchechefu wa msamiati Wa sayansi na hivyo haiwezi kukidhi viwango vya kufundishia elimu kutoka ngazi ya swali hadi vyuo vikuu. Hapa kuna mambo kadhaa ambayo wasomi hawajayaelewa. Nayo nitayasema hapa:

(a) wasomi wenyewe wana ukata wa msamiati katika lugha ya Kiswahili. Lugha inapokuwa na kupewa majukumu makubwa lazima kuwepo na upangajilugha kongoo. Hawa ndiyo watoa dira wa matumizi ya lugha katika mawanda mapana na finyu. Katika majukumu yao ni kuunda msamiati kutokana na mahitaji ya jamii kiuchumi, kisiasa, kijamii, kiteknolojia na masuala mengine. Istilahi hizi huundwa kwa kutumia njia mbali mbali za uundaji wa maneno ikiwemo ya kutohoa maneno kutoka lugha chanzi.

(b) Tunapaswa tujiulize maswali, kwa nini lugha ya Kiingereza ina msamiati mwingi kutoka lugha za Kigiriki na Kilatini pamoja na Kifaransa. Maneno ya Kigiriki na Kilatini kuwa mengi katika lugha ya Kiingereza ambayo sisi tunaiona ndiyo lugha faafu ni kutokana na maarifa kuanzia Ugiriki na Italia. Waingereza walihawilisha maarifa hayo kuyaingiza katika Kiingereza huku wakitohoa baadhi ya maneno ambayo hayakuwa na visawe katika lugha ya Kiingereza. Kifaransa kimechangia msamiati mwingi katika Kiingereza kwa sababu ya nchi hiyo ya Uingereza kuwa kwenye utawala wa mfaransa kwa karne kadhaa. Unaweza kurejea kitabu cha Mastering the advanced English Language kilichoandikwa na Sara Thorne 1997.

Lugha yoyote inayokua lazima itohoe ili aendelee kuwa hai.

3. Utekelezaji wa Serikali katika Ufasiri wa Nyaraka

Serikali ina nafasi kubwa ya kuhakikisha Kiswahili kinakua kwa kasi na kutekeleza mipango kazi ya nyaraka zilizo kwenye lugha ya Kiingereza kwenda kwenye Kiswahili. Serikali na Bunge kama wapangajilugha Hadhi kwa maana ya matumizi ya lugha kitaifa. Iwapo serikali itawezesheza vyombo vya lugha yaani wapangajilugha kongoo (wanaisimu) kuwezesha kifedha, matini na vifaa vya kielektroniki vyenye mifumo hawilishi, na zoezi la ufasiri kuanza Mara moja, ndani ya mpango kazi wa miaka 5-10 lugha ya Kiswahili itakuwa imedhibiti katika nyanja zote na istilahi sahihi zitakuwa zimefikiwa kwa asilimia 99.

Iwapo tutashirikiana kikamilifu katika kukitangaza Kiswahili basi kitaendelea kupasua anga katika nchi mbali mbali ulimwenguni na kukua zaidi.

Kwa kusema haya sasa tunaweza kuona wapi tunapungukiwa na tufanye nini. Kila mmoja wetu awe balozi wa kuilinda tunu hii tuliyopewa na Mungu
 
Upvote 2
Back
Top Bottom