Kutoka Mwananchi ya Leo. FMES you are on top of the news, man!
Date::2/19/2009 Umoja wa Vijana CCM waanza kutimuana Na Leon Bahati
MGOGORO upya unafukuta ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapiduzi (UVCCM) baada ya Kaimu Katibu wake Mkuu, Isaack Francis, kuenguliwa kwenye madaraka kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali na matumizi mabya ya madaraka.
Baada ya kumtuimua Isaack, nafasi ya Kaimu Katibu wa UVCCM, inashikiliwa na Ally Issa, ili kupisha uchunguzi huru dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana, zimesema kuwa uamuzi wa kumwengua Katibu Mkuu huyo, umefikiwa na kikao cha Kamati ya Utekelezaji kilichofanyika siku mbili kuanzia Jumanne chini ya Mwenyekiti wa umoja huo Masauni Hamad Masauni katika ofisi ndogo za Makao Makuu ya CCM zilizoko Mtaa wa Lumumba, jijini Dar es Salaam.
Taarifa zinasema kuwa, baada ya kumwengua Isaack, kamati imeunda tume ya watu watano inayoongozwa na Ridhiwan Kikwete kuchunguza tuhuma hizo.
Kwa mujibu wa habari hizo, Isaak anatuhumiwa kuingia mkataba na wafanyabiashara wa jengo la Makao Makuu ya UVCCM bila kuijulisha Kamati ya Utekelezaji na Baraza Kuu la umoja huo jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.
Kwa mujibu wa kanuni za UVCCM, kabla ya mikataba kutiwa saini, inatakiwa kupitia kwenye Kamati ya Utekelezaji, Baraza Kuu na Baraza la Wadhamini.
Taarifa za ndani ya kikao cha kamati ya utekelezaji zilieleza kuwa, baadhi ya wajumbe walikuja juu na kutaka Isaack afukuzwa kazi moja kwa moja kwa sababu maelezo juu ya tuhuma zake yako wazi.
Hata hivyo, Mwananchi lilipowasiliana na Issack, alikanusha taarifa hiyo akisema, tuhuma hizo sio za kweli na kusisitiza kuwa yeye bado yupo kwenye madaraka hayo ya Kaimu katibu Mkuu wa UVCCM.
"Hiyo siyo kweli. Mimi bado naendelea na kazi. Kwa sasa nimetoka tu kidogo ofisini niko maeneo ya Kariakoo," alisema Issack wakati akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu.
Hata hivyo alikiri juu ya kuandamwa na tuhuma hizo na kusema kuwa, waliozianzisha walikuwa na tafsiri tofauti.
Isaack alieleza kuwa katika shughuli za ukarabati wa jengo la UVCCM makao makuu, baadhi ya mafundi waliweka vifaa katika chumba kimoja cha jengo hilo na baadhi ya wanachama wakatafsiri kuwa wamepangishwa.
"Hii ni sehemu tu ya shughuli za ukarabati wa jengo na wala sikumpangisha mtu," alisema Isaack nakubainisha kuwa katika shughuli za ujenzi zinazofanyika katika eneo hilo, kuna wanaokarabati jengo na wanaojenga eneo la wazi nyuma yake.
Akizungumzia suala hilo, Ali Issa ambaye aliteuliwa kukaimu nafasi ya Isaack, alikiri kuwa tayari ameshaanza kazi hiyo.
Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Masauni Hamad Masauni hakupatikana ili kufafanua suala hilo jana baada ya simu yake ya mkononi kuita muda wote bila kupokelewa.
Mgogoro huo umekuja miezi michache tangu Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), Nape Nnauye, kulituhumu Baraza la Wadhamini la UVCCM kuwa limesaini mkataba wa wawekezaji wa jengo hilo kinyume na taratibu.
Nape alidai kuwa baraza hilo na kumtaka mwenyekiti wake, Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa kujiuzulu, kwa madai kuwa mchakato wa ukarabati wa jengo hilo una harufu ya rushwa.
Tuhuma hizo zilikanushwa vikali na UVCCM na hata mkutano wa Baraza Kuu uliofanyika Dodoma Oktoba,mwaka jana kiliamua kumvua uanachama kwa madai ya kusema uongo.