Naibu waziri Denis Londo ahimiza matumizi ya BOS kuimarisha huduma za BRELA

Naibu waziri Denis Londo ahimiza matumizi ya BOS kuimarisha huduma za BRELA

BRELA

Govt Institution
Joined
Dec 14, 2023
Posts
119
Reaction score
89
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Denis Londo (Mb), ameipongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa hatua ilizochukua kuboresha Mfumo wa Huduma kwa Njia ya Mtandao (BRELA Online Services – BOS), huku akisisitiza kukamilisha maboresho kwa wakati ili kuongeza ufanisi na kuboresha huduma kwa wadau wake.

Mhe. Londo ameyasema hayo leo Oktoba 11, 2026, wakati akifunga kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa BRELA kilichofanyika mkoani Morogoro, kilicholenga kuimarisha ushirikiano kati ya Menejimenti na watumishi, kujadili utendaji wa taasisi na kuweka mikakati ya kuboresha mazingira ya kazi.

Amesema Serikali inaendelea kusisitiza matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za umma ili kurahisisha upatikanaji wa huduma, kupunguza muda wa utoaji huduma na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

“Nimefurahishwa na hatua za BRELA katika kuboresha Mfumo wa BRELA Online Services (BOS), ambapo moduli tano kati ya saba zimeanza kutumika. Nawapongeza kwa hatua hii na kuwasisitiza kuendelea kuongeza ufanisi, kupunguza muda wa utoaji huduma na kuboresha huduma kwa wananchi na wafanyabiashara,” amesema Mhe. Londo.

Aidha, ameitaka BRELA kuendelea kufanya mapitio na maboresho ya sheria na kanuni mbalimbali kwa kushirikiana na wadau, kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na kurahisisha utoaji wa huduma nchini. Amesisitiza kuwa mchakato huo unapaswa kuwashirikisha wadau kikamilifu ili kupunguza urasimu, kuondoa masharti yanayokwamisha shughuli za biashara na kuimarisha uzingatiaji wa sheria.

Kwa upande wake Bw. Elias Kalist, akimwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara BRELA, amesema Bodi inatambua na kuthamini jitihada zinazofanywa na taasisi katika kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuboresha utoaji wa huduma.

“Bodi ya Ushauri inaendelea kusisitiza umuhimu wa BRELA kutumia mifumo ya kidijitali, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha Wakala inachangia kikamilifu katika utekelezaji wa mipango ya Serikali ya kukuza sekta binafsi na uwekezaji,” amesema Bw. Kalist.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, akiwasilisha hotuba yake, amesema katika Mwaka wa Fedha 2026/2027, Wakala utaendelea kuelekeza nguvu katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa BRELA wa mwaka 2026/2027–2030/2031, kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema maeneo yatakayopewa kipaumbele ni pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma kupitia mifumo ya kielektroniki, kukamilisha maboresho ya BOS, kuwezesha utoaji wa leseni za biashara za Kundi B kwa kushirikiana na mamlaka husika, pamoja na kuendelea kupitia sheria na kanuni mbalimbali kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa BRELA kimefanyika kwa siku tatu, kuanzia Oktoba 10 hadi 12, 2026, mkoani Morogoro. Kikao hicho kimehusisha mafunzo kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, msongo wa mawazo na afya ya akili, pamoja na mafao, haki na wajibu wa wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), kwa lengo la kuongeza uelewa wa watumishi kuhusu afya, ustawi na maandalizi ya maisha ya baadaye.
WhatsApp Image 2026-10-11 at 14.04.40 (1).jpeg


WhatsApp Image 2026-10-11 at 14.04.41.jpeg
 
Back
Top Bottom