Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Ndugu zangu nilikuwa napita Maktaba Idara ya Picha.
Nia yangu ni kuandika kitu kidogo kuhusu mji wa Alexandria.
Katika pekua pekua nikakuta picha hiyo hapo juu niliyopiga Port Said Holiday Hotel.
Ilikuwa Jumatano Juni 15, 1988.
Hii picha yangu ikanishtua kidogo na kilichonishtusha ni mkao wangu. Nakuombeni muweke "caption," ya picha hii.
Alexandria ni katika miji mizuri duniani na sishi kuukumbuka lakini kwa sasa nitaukumbuka zaidi pamoja na magoli 5 waliyofungwa Simba na Al Ahly.
Ijumaa moja niliswali sala ya Ijumaa Montaza Palace, Alexandria. Hii ilikuwa kasri la Kiangazi la King Farouk na baada ya mapinduzi ya Gamal Abdel Nasser 1952 Montaza Palace ikawa moja ya majumba ya fahari ya serikali.
Ndani ya Montaza Palace kuna msikiti mzuri sana ambao niliswali Ijumaa nikifuatana na mwalimu wanvu mmoja kutoka Arab Maritime Transport Academy (AMTA) chuo kikubwa Arabuni yote katika mambo ya bahari.
Baada ya sala mwalimu wangu huyu akaniuliza kama nimeweza kuelewa khutba ambayo ilikuwa ya Kiarabu. Alishangaa nilipomwambia kuwa khutba ilikuwa kuhusu hijja. Nikamwambia nimeelewa khutba ile kutokana na aya za Qur'an kuhusu Hijja. Mwalimu wangu yule akaniuluza iweje nielewa Qur'an lakini sijui lugha ya Kiarabu?
Hii Montaza Palace ina sehemu muhimu moyoni kwangu kutokana kitabu cha Mohamed Hasnain Heykal, "The Road to Ramadan," alichoandika kuhusu Vita Vya Yom Kippur baina ya Misri, Syria na Israel mwaka wa 1973.
Baada ya mafanikio makubwa katika uwanja wa mapambano Anwar Sadat alikwenda Montaza Palace huku vita vikiendelea.
Heykal mwandishi mkubwa sana aliyekuwa mhariri wa gazeti la Alhram la Misri alikwenda Montaza Palace kufanya mahojiano na Sadat. Heykal katika staili yake ya uandishi wa "satire," kwa jambo asilopenda kwenye kitabu hicho anasema kamkuta Sadat ana glasi ya kinywaji.
Akampa swali.
Sadat hakujibu akaongeza kinywaji kwanza.
Taratibu akawa anakunywa hadi akamaliza ndipo akafungua kinywa chake akasema, "Mohamed mimi ni Amiri Jeshi Mkuu hayo maswali yako wapelekee wanasiasa Cairo watakujibu."
Katika sura hii Heykal anamnanga sana Sadat anasema uniform yake ya Commander in Chief aliagizisha kwa ‘’designer,’’ mabingwa wa mitindo ya nguo kampuni maarufu ya Paris - Yve Saint Laurent.
Kuna mengi ya kejeli Heykal kaandika...kila ninapoikumbuka Alexandria nakumbuka Montaza Palace, Sadat, Heykal...na goli 5.