Sanda nimekusikia, yote uliyo usia
Sawa nitakusudia, la kwangu kujipatia
Niache ya kudandia, safarini sitafika
Wapi naweza pata, la injini siyoguswa
Sitaki eti lolote, moyoni sitaridhia
Au la kwenye matope, mjini yana kadhia
Kuna yale kiokote, kinunua tajutia
Wapi naweza pata, la injini siyoguswa
Nataka liwe jipya, mashine kichungulia
Hapa nina uhakika, dunia tazungukia
Nitaondokwa mashaka, sababu nalijulia
wapi naweza pata, la injini siyoguswa
Siwezi nunua gari, iliyokwisha tumika
Na kila siku si shwari, sipana ninajitwika
Nyingi kikiri kikiri, wabaki wataabika
wapi naweza pata, la injini isoguswa
sindano mwana wa ganzi
Sindano mwana ganzi,sije leta msiba.
Ukayaleta majonzi,chozi silo tiba.
Kwa kuleta weredi,injini kuzi chunguza.
Waweza leta ufundi,wenzio kwisha chakachua.
Walikuwapo wakwezi,mabingwa wa kupalamia.
Miembe na minazi,wako juu kudandia.
Matawi yakawa telezi,ahera kwenda mapema.
Magari sio nazi,ikivunjwa unaona.
Japo kwenye yadi,utacheza patapotea.
Yapo ya toka enzi,rami yana chubua.
Jaifongo na Bedifodi,yang'aa kama Korola.
Upwa injini si kazi,dukani wenda nunua.
Waweza pata uchizi,ukweli kuja fahamu.
Kuna yale Mashangingi,bei milioni mia.
Injini ni za Bajaji,zile kutoka India.
Bora kuacha chunguzi,safari unapo ridhia.