SoC02 Namna nilivyoweza kupunguza gharama za kilimo kwa kutengeneza mbolea yenye uwezo mkubwa wa ajabu

SoC02 Namna nilivyoweza kupunguza gharama za kilimo kwa kutengeneza mbolea yenye uwezo mkubwa wa ajabu

Stories of Change - 2022 Competition

Lpt

Member
Joined
Oct 9, 2020
Posts
13
Reaction score
13
Kilimo tangu nyakati za uhuru mpaka leo hii ndiyo sekta pekee inayoajiri asilimia kubwa ya watanzania. Inakadiriwa kuwa zaidi ya 60% ya watanzania wamejiajiri au kuajiriwa katika sekta ya kilimo. Na kilimo imekuwa mhimili mkubwa wa maisha ya kila siku ya watanzania wengi. Pamoja na kuwa kilimo ndiyo mhimili mkubwa katika maisha yetu lakini kumekuwa na changamoto kadha wa kadha zinazoikumba sekta hii ya kilimo. Changamoto hizi ni pamoja na gharama kubwa za uzalishaji zinatokana na kupanda kwa gharama za mbolea, mbegu bora, viuatilifu n.k.

Katika kukabiliana na changamoto hii ya kupanda kwa gharama za pembejeo za kilimo niliamua kujifunza zaidi namna ya kupunguza gharama hizi hasa kwa kutumia rasilimali zinazopatikana kwa urahisi na rafiki kwa mazingira yetu. Nilijifunza namna ya kuandaa mbolea ya asili ambayo ni rafiki kwa mazingira yetu na pia inayotunza na kuboresha afya ya udogo shambani. Nilitumia mbolea hii kwenye kilimo cha mahindi katika eneo lenye mita za mraba 1200 (robo eka) mwaka huu 2022 na kufanikiwa kupata gunia 9 za mahindi tofauti msimu wa mwaka 2021 ambapo nilipata gunia 1½ katika eneo hilo hilo bila kutumia mbolea.

NAMNA YA KUAANDAA MBOLEA HII.
Uandaji wa mbolea hii ni mrahisi sana na utaandaa kulingana na uhitaji wako. Hapa mimi nitaelezea uandaaji wake kwa ujazo wa lita 200.

Mahitaji.

Pipa lenye ujazo wa lita 200
Ndoo kadhaa
Mti mdogo wa kukorogea
Kinyesi cha ng'ombe/mbuzi/kondoo/kuku n.k. ndoo moja
Mkojo wa ng'ombe ndoo moja
Maziwa lita 10
Amira (yeast)
Majivu yanayotokana na mimea (miti au taka za shambani) kilo 5
Majani mabichi
Maji
Molasses (sukari, guru)
Mabaki ya chakula (unga kilo 2)

HATUA ZA KUFUATA
Kinyesi cha ng'ombe kiasi cha ndoo moja huwekwa kwenye pipa ikifuatiwa na mkojo wa ng'ombe ndoo moja, maziwa lita 10, amira vijiko viwili mpaka vitatu vya chakula, molasses lita 5 na majivu kilo mbili. Majani mabichi hasa yakipatikana ya mbaazi yanafaa zaidi kwa kuwa na wingi wa nitrogen. Majani haya huandaliwa kilo tano na kutwangwa twanga kisha huwekwa kwenye pipa. Mabaki ya chakula ni muhimu sana na kama hakuna mabaki hayo, huweza kutumika unga wa mahindi, muhogo, mtama au soya kiasi cha kilo mbili. Mchanganyo huo hukorogwa kwa kutumia kipande cha mti na kisha maji huongezwa kujaza pipa kiasi cha ujazo wa lita 200. Baada ya pipa kujazwa mchanganyo hukorogwa tena na kishwa kufunikwa. Na kila siku mchanganyo hukorogwa mpaka siku ya tano na baada ya hapo tunauacha kwa siku 10 kisha utakuwa tayari kwa matumizi.

MATUMIZI
Mbolea hii nimekuwa nikitumia kwa namna mbili. Namna ya kwanza nimeitumia kunyunyiza kwenye udongo (mizizi) ya mimea na hapa nimekuwa nikitumia lita moja kwa lita 14 za maji na kwa kutumia pampu ya mgongoni na nyunyiza mbolea kwenye udongo kuzunguka mmea.
Katika namna ya pili natumia mbolea kunyunyiza kwenye majani ya mimea shambani. Yaani natumia kama busta (foliar spray) mililita 50 (50cm³) hutumika kwa pampu ya lita 15 hadi 20. Kisha mbolea hii hunyunyizwa kwenye mimea kwa kuiloanisha.

FAIDA
Mbolea hii hufurahiwa sana na mimea shambani. Mimea muda wote hupendeza kabisa. Pia mia inakuwa haishambuliwi hovyo na magonjwa pamoja na wadudu. Mbolea hii huzuia magonjwa ya mimea inayotokana na bakteria. Mimea ya aina yote inaweza kukuzwa na kuwa na matokeo chanya kama utatumia mbolea hii.

Pia nimekuwa nimekuwa nikitumia majani ya mpera, mwembe, mwarobaini na mjohoro. Hapa naandaa kilo mbili za majani haya kisha ninayapondaponda mpaka yaanze kutoa juisi yake na baada ya hapo nachanganya na mbolea lita 18. Mchanganyo huu naukoroga kwa dakika mbili na kisha nauweka kwenye kivuli mbali na mwanga wa hua kwa siku 7 huku ukiwa umefunikwa. Baada ya hapo nautumia kudhibiti wadudu kwenye mboga mboga, viazi na nyanya ninazolima. Hapa natumia mililita 50 mpaka 100 kwa pampu ya mgongoni ya lita 15 hadi 20. Inasaidia sana kudhibiti wadudu waharibifu kwenye mimea jamii ya mboga mboga, nyanya na mahindi pia. Mbinu hii imenisaidia sana mwaka huu wa 2022 kwenye kilimo changu. Japo siyo kilimo cha eneo kubwa.

Rai yangu kwa wakulima wenzangu hasa wakulima wadogo tujifunze uandaaji wa mbolea hii na kuitumia ili kupunguza gharama za kilimo. Mimi ninaitumia sana kwenye kilimo changu tangu mwezi Julai 2021 na imekuwa na matokeo mazuri sana kuanzia kilimo cha nyanya, mboga mboga mpaka mahindi.

Pia nimekuwa nikitoa elimu kwa wanafunzi wangu pamoja na majirani zangu utengenezaji wa mbolea hii na wapo walioanza kufurahia matokea ya mbolea hii.

Hapa kuna picha baadhi ya wanafunzi wangu wakitengeneza mbolea hiyo baada ya kujifunza uandaaji wake.

IMG_20220819_131243_237.jpg
IMG_20220819_132318_613.jpg
 
Upvote 12
Mnhhh tusije kutengeneza bomu lol....

Mkuu nimekupa vote, labda topic yako inaweza kuwa utatuzi wa mbolea nchini, waziri Bashe akalitazame na hili.....
 
Mnhhh tusije kutengeneza bomu lol....

Mkuu nimekupa vote, labda topic yako inaweza kuwa utatuzi wa mbolea nchini, waziri Bashe akalitazame na hili.....
Mbolea hii inafanya vizuri sana. Tena kama watu wakiwa na umoja wanaweza tengeneza pamoja wakagawana.
Lengo ni kuhakikisha tusishindwe kuzalisha vyakula kutokana na gharama kubwa sana pembejeo za kilimo
 
Mbolea hii inafanya vizuri sana. Tena kama watu wakiwa na umoja wanaweza tengeneza pamoja wakagawana.
Lengo ni kuhakikisha tusishindwe kuzalisha vyakula kutokana na gharama kubwa sana pembejeo za kilimo
Sawa mkuu, na hivi vyakula ni gharama sana kwa sasa hivi...
 
Back
Top Bottom