JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 685
- 1,124
Namna ya Kumueleza mtoto:
Ni muhimu mzazi au mlezi kwa kushirikiana na mtoa huduma kuandaa mpango wa namna ya kumueleza mtoto hali yake ya maambukizi ya VVU, kabla ya mtoto huyo kupata habari hiyo kutoka vyanzo vingine.
Kusikia habari kuhusu hali yake ya maambukizi toka kwa mtu mwingine, kunaweza kumfanya mtoto ajisikie vibaya na atingwe na msongo wa mawazo na hata kupelekea kuchukua maamuzi yasiyofaa kama vile kujiua, kuacha shule, kuacha dawa hata kutokuwa na imani na wazazi wake.
Ni vizuri kuongea na kumwambia mwanao mambo yanayomuhusu na kumfariji.
Mtoto aelezwe ukweli kuhusu afya yake huku akifundishwa namna ya kujikinga na kuwakinga wenzake. Mtie moyo kukubaliana na hali halisi ya mabadiliko ya kiafya yanayoweza kujitokeza mara kwa mara na namna ya kujihudumia.
Tujenge tabia ya kuamini watoto wetu kuwa wana uwezo mkubwa wakipatiwa muongozo mzuri wanaweza kufanya makubwa kujilinda na kuwalinda watoto wenzao.
Wazazi/walezi wanapaswa kuzungumza na watoto juu ya ugonjwa huu kwa njia inayolingana na umri wao ili isiwatishe. Watoto wanahitaji kujua kwamba sio kosa lao, wao ni wagonjwa na wanapaswa kumeza dawa kila siku.
Mzazi amtie moyo mwanae kuwa hayuko mwenyewe katika kukabiliana na ugonjwa huu. Msaada wa kijamii, kifedha, na kimhemko/kisaikolojia kwa familia nzima ni muhimu pia.
Watoto wenye VVU na UKIMWI wanaweza kwenda shule salama. Ila wanaweza kukabiliwa na unyanyasaji na ubaguzi ikiwa wanafunzi wengine na waalimu hawana uelewa mzuri wa jinsi VVU vinavyosambazwa.
Uhamasishaji na mipango ya elimu husaidia kuvunja unyanyapaa wa VVU ili watoto wawe na marafiki na kuhisi wanapendwa na wako sawa na watoto wengine.
Upvote
0