Nguruvi3 isauti ya nguruvi. Nmekuelewa. Kama alisema anazungumzia HISTORIA YA WAZEE WAKE HAPO KWA KWELI TUTAKOSA LA KUSEMA. NI SAWA NAMI NIJE NISEME NAZUNGUMZIA HISTORIA YA FAMILIA AU JAMAA ZANGU
Akianza kuzungumzia HISTORIA YA TAIFA BASI tusimtupe mkono....angalau tuchangie changie kitu. Maana haileti picha nzuri nyuzi zake mnazipita tu utadhani ni za matangazo yà kuuza shombo ya samaki.
Chizi...
Hii ni moja ya historia nyingi za wazee wangu wakati wakipigania uhuru wa Tanganyika:
"Dunia ni ndogo sana.
Siku ya Jumanne nilikuwa kwenye foleni benki Mlimani City na jirani yangu alikuwa amekaa binti mdogo na katika vitu alivyokuwanavyo ni kitabu, ''Vuta, Nkuvute,'' cha Adam Shafi.
Kitabu hiki ni toleo jipya hivyo ikanivutua ''cover,'' yake nikamuomba huyu binti nikiangalie kile kitabu na hapo ndipo mazungumzo yalipoanza.
Kama nilivyotangulia kusema, dunia ni ndogo sana.
Yule binti akaniambia kuwa yeye ni mjukuu wa Mzee Omari Londo.
Kwa wasiomjua Omar Londo huyu ni mmoja wa wanachama wa mwanzo wa TANU aliyekuwa akiishi Mtaa wa Somali, Gerezani.
Hivi sasa mtaa huo umebadilishwa jina na unaitwa Mtaa wa Omari Londo kwa heshima ya mzalendo huyu.
Nikamwambia kuwa namfahamu vyema babu yake.
Akanifamisha pia kuwa yeye ni kitukuu cha Bi. Tatu binti Mzee.
Kwa wasiomfahamu Bi. Tatu binti Mzee ni kuwa Bi. Tatu binti Mzee ndiye chanzo cha Bi. Titi kuingia TANU na kuwa kiongozi mkubwa aliyeongoza wanawake katika kuijenga TANU na kupandisha haiba ya Mwalimu Nyerere wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.
Hiki kitukuu cha Bi. Tatu bint Mzee ni muhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na akanitajia jina lake kuwa ni Hawa binti Ali.
Hawa akanieleza kuwa ilikuwa wakati wa kupigania uhuru ndipo Bi. Tatu bint Mzee alipomtoa mwanae aolewe na Omari Londo na hivyo mama yake kuzaliwa lakini sasa ni marehemu.
Hawa alifahamisha kuwa amesikia mengi katika kupigania uhuru wa Tanganyika nyumbani kwao akitajwa babu yake na wazee wengine lakini kilichomstaajabisha ni kuwa historia hii hajaweza kuisoma popote.
Hapo ndipo nilipojitambulisha na nikamuahidi kumrushia picha ya bibi mkuu wake akimsindikiza Mwalimu Nyerere Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam safari ya kwanza anakwenda UNO, New York mwaka wa 1955 akiwa na Bi. Titi Mohamed, Bi. Chiku Kikusa na akina mama wengine.
Nikamweleza kuwa nimezaliwa Kipata na wazee wangu wameishi mitaa kadhaa ya Gerezani katika 1920s hadi kufikia 1960s pamoja na Mtaa wa Somali jirani na kwa babu yake.
Bahati mbaya sikuweza kumkumbuka marehemu mama yake.
Hii picha hapo chini nilipewa na Abdulrahman Ali Msham mtoto wa Ali Msham mmoja wa wazalendo walioingia TANU mapema sana kupigania uhuru.
Sikiweza kumtambua Bi. Tatu binti Mzee hadi jana Hawa baada ya kumpelekea picha hii aliponirudishia majibu na kunambia kuwa Bi. Tatu binti Mzee ni huyo wa pili kulia waliokaa na wa nne ni Bi. Titi Mohamed.
Ali Msham ni wa pili kushoto waliosimama.
Hili ni tawi la kwanza la TANU Magomeni."
2018