Jackson94
JF-Expert Member
- Sep 14, 2016
- 492
- 560
Chanzo cha picha,EPA
Maelezo ya picha,Viongozi wa Hamas watakutana tena kumchagua mrithi wa Yahya Sinwar
Maafisa wawili wa Hamas wameambia BBC kwamba majadiliano ya kumchagua mrithi wa kiongozi wa kundi hilo Yahya Sinwar, ambaye mauaji yake yalithibitishwa siku ya Alhamisi wiki jana, yataanza hivi karibuni.
Maafisa hao walisema Khalil al-Hayya, naibu wa Sinwar na afisa mkuu wa kundi hilo nje ya Gaza, anazingatiwa kuwa mgombea aliye mstari wa mbele kuichukua nafasi hiyo.
Al-Hayya mwenye makazi yake nchini Qatar kwa sasa anaongoza ujumbe wa Hamas katika mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya kundi hilo na Israel, na ana ujuzi wa kina, uhusiano na uelewa wa hali ya Gaza.
Viongozi wa Hamas watakutana kwa mara nyingine tena kumchagua mrithi wa Sinwar, ambaye alikuwa mtu anayesakwa sana na Israel, miezi miwili tu baada ya kuuawa kwa kiongozi wa zamani Ismail Haniyeh mjini Tehran.
Unaweza Pia Kusoma
- Yahya Sinwar: Kiongozi wa Hamas ni nani?17 Oktoba 2024
- Jinsi Israel ilivyompata na kumuua kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar18 Oktoba 2024
- Kifo cha Sinwar ni pigo kubwa kwa Hamas, lakini sio mwisho wa vita18 Oktoba 2024
Tangu Julai, mazungumzo ya kusitisha mapigano yamekwama, na wengi wanaamini kuwa uongozi wa Sinwar ulikuwa kikwazo kikubwa kwa mpango wowote wa kusitisha mapigano.
Licha ya kuuawa kwa Sinwar, afisa mkuu wa Hamas alikariri BBC kwamba masharti ya vuguvugu hilo ya kukubali kusitishwa kwa mapigano na kuachiliwa kwa mateka wa Israel hayajabadilika.
Hamas inaendelea kuitaka Israel iondoke kabisa Gaza, kukomeshwa kwa uhasama, uhamishaji wa misaada ya kibinadamu, na ujenzi wa eneo hilo - masharti ambayo Israel imeyakataa kabisa, ikisisitiza kuwa Hamas lazima ijisalimishe.
Walipoulizwa kuhusu wito wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa Hamas kuweka chini silaha zake na kujisalimisha, maafisa wa vuguvugu hilo walijibu: “Haiwezekani sisi kujisalimisha.
"Tunapigania uhuru wa watu wetu, na hatutakubali kujisalimisha. Tutapigana hadi risasi ya mwisho na askari wa mwisho, kama vile Sinwar alivyofanya."
Kuuawa kwa Sinwar ilikuwa moja ya pigo kubwa zaidi kwakundi hilo katika miongo kadhaa. Hata hivyo, licha ya changamoto za kuiziba nafasi yake, Hamas ina historia ya kuvumilia mapigo ya uongozi tangu miaka ya 1990.
Wakati Israel imefanikiwa kuwaua viongozi na waanzilishi wengi wa Hamas, vuguvugu hilo limethibitisha kuwa na uthabiti katika uwezo wake wa kutafuta wapya.
Katikati ya mgogoro huu, maswali yanasalia kuhusiana na hatma ya mateka wa Israel wanaoshikiliwa huko Gaza na nani atawajibikia usalama na ulinzi wao.
Katika muktadha huu, Mohammed Sinwar, kakake Yahya Sinwar, amejitokeza kama mtu muhimu. Anaaminika kuwa anaongoza makundi yaliyosalia yenye silaha ya Hamas na huenda akawa na jukumu muhimu katika kuunda mustakabali wa harakati hiyo huko Gaza.
Wakati Hamas inapitia wakati huu muhimu, vita huko Gaza vinaendelea.
Makumi ya watu waliuawa katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Gaza siku ya Jumamosi wakati wanajeshi wa Israel walipozidisha mashambulizi dhidi ya kile Israel inachosema ni majaribio ya Hamas kujipanga upya.