Sorry sijaelewa ni wapi? Au unamanaisha hii hapa kwenye makutano ya Mkunguni na Lumumba ave? Mbele yake kidogo penye Shopping Mall kubwa ambayo nasikia majengo ni ya Bakwata?
Kinyungu,
Jengo lipo kona ya Mtaa wa Makisi Mbwana na Lumumba Avenue.
Katika miaka ya 1930s Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika walikuwa wanajenga shule ambayo sote tunaijua lakini hela zilikuwa tatizo jengo likawa linachukua muda mrefu kukamilika.
Sababu ya kujenga shule hii ni kuwa wazee wetu na wao walitaka wawe na mahali pa kuwasomesha watoto wao kuepuka vijana wao kubatizwa katika shule ambazo serikali ya kikoloni iliziweka mikononi kwa Kanisa.
Kleist akiwa kiongozi wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika alitambua mapema sana kuwa tatizo kubwa lililokuwa likiwakabili Waislam ilikuwa ni kukosa elimu ambayo serikali ya kikoloni iliwaachia wamishionari waisimamie.
Si kama Waislam hawakuwa wanatambua faida ya elimu kwa watoto wao.
Wazazi wengi walichelea kuwapeleka watoto wao shule kwa sababu wamishionari walichukua fursa hiyo kuwabatiza.
Kuliko kwa watoto wao kutolewa katika Uislam na kuwa murtad, wazazi wengi waliamua kuisamehe elimu yenyewe kabisa.
Kleist aliona kuwa ufunguo wa tatizo hilo kwa Waislam ilikuwa ni kuanzisha shule zao wenyewe ambazo zitasomesha Qur’an pamoja na masomo mengine.
Wakati ule, na hata hivi sasa, Qur’an ilikuwa ikisomeshwa kwa mtindo wa asili ambapo mwanafunzi anakaa chini sakafuni mbele ya maalim akiwa na ubao wake na juzuu.
Kleist hakuona sababu kwa nini Qur’an nayo isisomeshwe kama elimu nyingine, wanafunzi wakiwa madarasani wakikaa katika madawati.
Alilitoa wazo hili kwa rafiki zake akashauri madrasa ipanuliwe ili masomo mengine yasomeshwe pamoja na Uislam.
Ushauri huu ulijadiliwa kati ya Kleist, Ali Kiro, Maalim Popa Saleh na Shariff Salim.
Wakitambua kazi kubwa iliyokuwa ikiwakabili, waliamua waanze hiyo shule kwa kidogo kidogo kwa awamu.
Nyumba itakayokuwa shule ya muda ilitafutwa na wanafunzi wakaanza kusoma.
Kati ya walimu wa mwanzo wa shule hiyo walikuwa Mzee Ali Comorian na Sheikh Abdallah Iddi Chaurembo ambao walikuwa kati ya wasomi wa Kiislam waliokuwa wakiheshimika.
Wazazi wa Kiislam waliombwa wachange fedha ili jengo la kudumu lijengwe.
Al Jamiatul Islamiyya ikawa inapita nyumba hadi nyumba ikikusanya michango kutoka kwa Waislam.
Bahati nzuri mwaka wa 1936 Aga Khan alitembelea Tanganyika na akafahamishwa kuhusu ujenzi wa shule ile.
Katika hafla ile mtoto aliyesoma risala kwa Aga Khan alikuwa Abdul Sykes akiwa na umri wa miaka 12.
Marehemu Kanyama Chiume amenihadithia kuwa wakati huu alipofika Aga Khan Tanganyika yeye alikuwa anasoma Shule ya Kitchwele na alikuwa katika bendi ya shule iliyompokea yeye akipiga, ‘’triangle,’’ na alinieleza kuwa picha yake yeye akipiga, ‘’triangle,’’ ilitokea katika gazeti.
Aga Khan alitoa fedha na shule ikajengwa New Street si mbali sana na ilipokuwa ofisi ya African Association.
Kleist akawa katika kamati ya ujenzi akikagua kazi hadi ujenzi ulipokamilika.
Hii ni moja kati ya shule za mwanzo kujengwa na Waislam wa Tanganyika.
Jengo la Al Jamiatul Islamiyya lipo limesimama hadi leo kama ushahidi na kumbukumbu za juhudi za Waislam katika kujiletea maendeleo yao.
Serikali katika kuthamini mchango wa Kleist katika kupeleka mbele elimu kwa ajili ya watoto wa Kiislam ikamchagua kuwa katika Provincial Education Committee of Tanganyika Education.
Mwanae Abdulwahid na yeye vilevile akaja kuwa katika Aga Khan Education Committee.