MAHENDEKA
JF-Expert Member
- Jul 9, 2010
- 337
- 179
mpendwa789 naona tumeelewana haswa kuhusu humanism/ utu.
Kwa sababu unajifunza Kiswahili, itakuwa vyema nikiandika kiswahili. Nilikuwa na mfanya kazi mwenzangu wa kutoka Uskochi (Scotland), alikuwa anafanya kazi za mazingira Tanzania. Basi alilalamika sana kwamba Watanzania walikuwa hawampi nafasi ya kujifunza kiswahili kwa maana kila mara walipokutana naye waliongea kiingereza, labda na wao ndiyo ilikuwa nafasi yao ya kujinoa kiingereza.
Miaka kama kumi iliyopita nilitaka kufanya kazi na kikundi fulani kutafsiri kitabu cha Brian Greene "The Elegant Universe". Nikagundua, hususan kwa nyanja za sayansi zenye mambo mengi mapya kama katika unajimu, kiswahili si tu hakina maneno, bali hata dhana zenyewe ni ngeni. Kwa mfano, tuna sayari na nyota lakini sifahamu kama kuna neno la kiswahili asilia la kumaanisha "galaxy". Katika hili, sioni ubaya wa kutohoa kutoka kiingereza na kusema "galaksi". Hata kiingereza chenyewe kimenufaika sana na kutohoa kutoka kilatini, kigiriki na lugha nyingine. Hii ni tabia ya lugha, na kama wanazuoni wataona kuna maneno yanahitajika, ni wajibu kuongeza, kwani lugha hukua.
Pia, watu wa kawaida hawafahamu maneno mengi sana ya kiswahili ambayo hayatumiwi kila siku, hivyo mara nyingine tunaweza kufikiri kiswahili hakina maneno, kumbe yapo mengi sana na mengine hata katika kamusi hayapo, wanaongea watu wanaojua lahaja ya Pemba tu huko waliojikita katika uvuvi, au watu wa Barawa, na kadhalika. Nikisoma vitabu vya Shaaban Robert, muandishi mashuhuri wa kiswahili aliyeandika sana kabla ya uhuru wa Tanganyika, na malenga walioandika miaka ile - na hata washairi mashuhuri wa sasa- naona maneno mengi yametumika ambayo watu wa kawaida hawatayajua katika mazungumzo ya kila siku, au hata katika mhadhara wa chuo kikuu. Lakini hili ni suala lililo sehemu nyingi, wengi hawawezi kuwasiliana kwa kiingereza cha Michael Erick Dyson au Noam Chomsky katika mazungumzo ya kila siku. Hili si kwa kiswahili na kiingereza tu, mfalme Hirohito wa Japana alipomaliza kutoa hotuba yake ya kujisalimisha baada ya Japan kushindwa vita vikuu vya pili, Wajapan walianza kujiuliza "huyu mfalme hapa kasema nini?", kwa sababu alitumia kijapani cha hadhi ya juu sana. Inabidi tuepuke umwinyi katika mawasiliano kwa kutumia lugha sahihi lakini isiyowafungia wengine kuelewa. Kwa wapenda lugha hili linaweza kuwa gumu kwa sababu kutafuta urembo wa lugha kunaweza kumaanisha kuwafungia wengine wasielewe. Mimi pia nina tatizo hilo.
Kuhusu " I am glad to have the opportunity to practice Kiswahili. unaweza kusema " Nafurahia kupata nafasi ya kujizoeza kutumia Kiswahili.. "To practice" = " ku jizoeza".
Asante kwa kukisifu kiingereza changu, bado nina mengi ya kujifunza.Naishi Marekani, ila tangu mdogo nilipenda sana kusoma vitabu vya kiingereza ikiwa pamoja na kamusi za kiingereza kwa kiingereza na kiswahili kwa kiingereza ili kujenga msamiati. Nina mapenzi sana na lugha, sayansi na falsafa na mambo mengi niliyotaka kufahamu hayakuwa yameandikwa kiswahili, hivyo nilikuwa natumia muda mwingi sana kwenye maktaba za British Council, United States Information Services na Maktaba Kuu ya Taifa pamoja na za shule nilizosoma. Kama methali ya kiswahili inavyosema "mgaagaa na upwa hali wali mkavu" na mimi ingawa siwezi kujisema kama ni gwiji wa kiingereza, ila kupenda kusoma kumejenga msamiati na ujuzi wa kiingereza.
Karibu kutumia nafasi hii kujifunza lugha na mambo mengine ya utamaduni wa kiswahili na Afrika Mashariki.
Hongera sana Kiranga,kwa uandishi mzuri,wewe unafaa sana