Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba ameelekeza kuanzia tarehe 1 Julai, 2024, Wadau wote wa ndani, Taasisi za umma, Wafanyabiashara, Asasi za kiraia, Mashirika ya kimataifa na Watu wote waliopo Nchini Tanzania wenye tabia ya kuweka bei kwenye huduma au kuuza bidhaa kwa fedha za kigeni, kuacha mara moja na kuhakikisha bei za bidhaa na huduma hizo zinatangazwa na kulipwa kwa Shilingi ya Tanzania.
Akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 Bungeni Jijini Dodoma leo June 13,2024, Mwigulu amenukuliwa akisema “endapo una fedha za kigeni unatakiwa kuzibadilisha kupitia Benki au maduka halali ya kubadilishia fedha ndipo ufanye malipo kwa kutumia shilingi ya Tanzania, naielekeza Benki Kuu pamoja na vyombo vingine vinavyohusika kuendelea kudhibiti suala hili, kufuatilia kwa ukaribu ili kubaini wote wanaoendelea kufanya makosa hayo na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria, tunafanya kila malipo kwa fedha za kigeni, halafu shilingi ikishuka thamani tunajiuliza tumekosea wapi.
“Watanzania tunalikuza tatizo la upungufu wa dola kwa baadhi ya Watu kudai malipo au kufanya malipo ya bidhaa na huduma zinazotolewa ndani kwa kutumia fedha za kigeni yaani, dollarization, Taasisi ipo Tanzania na pengine hata Taasisi ya Serikali inamuuzia huduma Mtanzania inamwambia alipe kwa dola, Taasisi nyingine zinataka Mtu alipe ada kwa dola, alipe kodi ya nyumba kwa dola, vibali vya kazi, leseni na kadhalika kwa dola”
“Tunawafanya Watanzania wahangaike kuitafuta fedha ya kigeni kununua huduma zinazotolewa ndani ya Nchi yao badala ya kuwafanya Wageni wahangaike kuitafuta shilingi ya Tanzania wanapotaka huduma ndani ya Nchi, jambo hili linasababisha kuongezeka kwa mahitaji yasiyo ya lazima ya fedha za kigeni na kuwanyima fursa Watu wanaohitaji fedha za kigeni kwa ajili ya kulipia bidhaa na huduma muhimu kutoka nje ya Nchi, kitendo cha kuuza bidhaa au huduma za ndani kwa kutumia fedha za kigeni ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha sheria ya Benki kuu ya mwaka 2006 ambacho kinabainisha kwamba shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali pekee kwa malipo ya ndani ya Nchi"
“Aidha, nazielekeza taasisi zote za Serikali zinazotoza ushuru, ada na tozo mbalimbali kwa fedha za kigeni kurekebisha kanuni zao ili tozo hizo zilipwe kwa shilingi, hata Mgeni akija na fedha za kigeni ni vyema akaibadilisha kuwa fedha ya kitanzania ili aweze kupata huduma” ——— Dr. Mwigulu. #MillardAyoUPDATES