Kuomba radhi kwa Waziri wa wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye hakusaidii kuondoa wasiwasi wananchi na wadau wa siasa na demokrasia juu ya uhalali wa matokeo ya uchaguzi nchini Tanzania, wanasema wachambuzi wa masuala ya kisiasa.
Nnauye ameomba radhi baada ya mjadala kuibuka kufuatia kauli aliyoitoa katika kipande cha video kilichosambaa katika mitandao ya kijami kuhusu namna ushindi unaweza kupatikana katika uchaguzi.
”Matokeo ya kura si lazima yawe yale ya kwenye box. Inategemea nani anayehesabu na kutangaza. Na kuna mbinu nyingi, kuna halali, kuna nusu halali na kuna haramu. Na zote zinaweza kutumika, ilimaradi tu ukishamaliza, unamwambia Mwenyezi Mungu nisamehe pale nilipokosea” Nnauye aliwaambia wafanyabiashara katika soko la Kashai mjini Bukoba mkoani Kagera, kaskazini magharibi mwa Tanzania.
Nnauye alishangiliwa na wafanyabiashara hao, lakini katika mitandao ya kijamii wengi walimpinga na kumkosoa kwa kutoa kauli hiyo.
“Rais Samia anahangaika na Maridhiano, anahangaika na 4R’s, Waziri wake anakuja kusema hakuna kitu kama hicho kura tutaiba.. na hajali wala haogopi!” aliandika Salim Alkhasas.
Mchambuzi wa masuala ya siasa Thomas Kibwana anasema kwa nafasi aliyo nayo Nnauye ndani ya serikali na chama pia ni ngumu kwa wananchi kuchukulia kauli yake kama utani tu, kama ambavyo Nnauye alivyodai wakati akiomba radhi.
”Kwa kweli kuna kauli zikitoka huwezi kuzirudisha. Wazungu wanaita ‘pandora’s box’. Kwa cheo chake serikalini na ndani ya chama, kwa kauli aliyotoa, kurudisha imani ya watu inakuwa ngumu kwa sababu wengi watachukulia kwamba alichokisema mara ya kwanza ndiyo ukweli” anasema Kibwana.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Sanyansi ya Siasa na Utawala wa Umma Dkt.
Consolata Raphael Sulley alisema kauli ya Nnauye ichukuliwe kwa uzito kwa sababu uchaguzi ni mtiririko wa matukio na utaratibu, unaanza na kuelimisha watu umuhimu wa uchaguzi hadi kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi. Anasema ikiwa hata hatua moja tu ikakatika, huo uchaguzi, hauwezi kuwa wa demokrasia.
”Kauli kama hii haiji kwa bahati mbaya. Ni lazima tuangalie muktadha wa mfumo wa siasa zetu, mfumo wa uchaguzi, masuala mazima ya nani hasa anahesabu kura. Utani mtu haweza kukwambia bwana fulani uko hivi, halafu akasema bwana natania, halafu akarudia tena baada ya muda mrefu. Kwa hiyo nadhani kuna kitu. Unaona pia kwamba ameomnba msamaha. Ni kauli ambazo kwa kweli zinaleta sintofahamu hasa tunapoelekea kwenye uchaguzi” alisistiza Dkt. Consolata.
Hii si mara ya kwanza kwa Nnauye kutoa kauli yenye utata kuhusu uchaguzi. Mwezi June 2015, akiwa katika mkutano wa hadhara Nyehunge Sengerema, kaskazini magharibi mwa Tanzania Nnauye aliapa kwamba CCM ingerudi ikulu kwa namna yoyote ile.
“Tuna uhakika na ushindi wa Rais. Kwa namna yoyote ile CCM itarudi Ikulu hata kama ni kwa bao la mkono. Bao ni bao tu, ilimradi refa hajaona” alisema Nnauye wakati huo akiwa Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM.
Miaka sita iliyofuata ya Rais John Magufuli aliyeshinda uchaguzi huo, iligubikwa na kile kilichoelezwa kuwa ukandamizaji wa haki za msingi za siasa na demokrasia. Lakini baada ya kuchukua madaraka, mrithi wake Rais Samia Suluhu Hassan, aliahidi kufanya mageuzi ya kisiasa na kidemokrasia pia.
”Ninawaahidi mageuzi zaidi ya kisiasa ili kujenga taifa letu jipya kupitia siasa za ushindani” alisema Rais Samia alipokuwa akizungumza katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani yaliyoandaliwa na Baraza la Wanawake Chadema.
Mwaka mmoja kabla, Rais Samia alitambulisha falsafa aliyoiita 4Rs, yaani Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu), Reforms (Mabadiliko), na Rebuilding (Ujenzi Mpya), zifanyike kama dira ya alichosema kuwa ni dhamira yake ya kuleta mageuzi ya kisiasa nchini Tanzania.
Mapema Februari mwaka huu, Bunge lilibadilisha sheria tatu za uchaguzi – vyote vikiwa ishara ya mageuzi. Pamoja na kukiuka misingi ya kimedokrasia.
Hivyo kauli aliyoitoa Nnauye mwanzoni mwa wiki hii imeonekana kukiuka ahadi hiyo ya Rais Samia kufanya mageuzi ya kisiasa na demokrasia.
Kwa mujibu wa Kibwana, namna pekee ya kurejeshasha imani kwa wananchi kwamba hiyo kauli kweli ilikuwa utani, itategemeana na mchakato wa uchaguzi utakavyokwenda na jinsi vyombo husika vitakavyosimamia uchaguzi huo.
”Vitu vikienda kushoto, au pakiwa na hitilafu ya namna yoyote ile, wadau watarejerea na kusema ‘hili limeshasemwa’. Alichofanya ni jambo zuri, muungwana akikosea shurti aombe radhi. Lakini namna pekee ya kurudisha imani kwa wananchi itaonekana kwenye mchakato wa uchaguzi na si kwenye hii kauli ya kuomba radhi” alisema Kibwana. chanzo.BBC