Swahilian
JF-Expert Member
- Apr 28, 2009
- 591
- 69
NAPENDA KUANDIKA
Kalamu ya risasi tosha, naandika na kufuta.
Matendo yalonikosha,pia yalonikokota.
Yote nayaoanisha, wazo kamili napata.
Kwa njia ya ushairi, mie hupenda andika.
Lugha yangu ni rahisi, yeyote ataisoma.
Natoa yalo halisi, uwongo waja nichoma.
Hamasa ni ufanisi, najifunza toka zama.
Ushairi ulo wazi, hujikita kwa jamii.
Nawe naomba usome, kesho ushike kalamu.
Zili mbivu uzichume,walishe wapate hamu.
Nikosowe nijitume. Niithamini kalamu.
Ushairi kwazo beti, nafundisha maadili.
Nyimbo za chekecheani, na hadithi za nyakati.
Pia zao tafrani, za masai na mangati.
Sekeseke za mitaani,na mbu funua neti.
Shairi lajazwa ladha, kwa lugha ilo mkato.
Naandika lugha ya watu, Kiswahili ndo yetu.
Nawazima roho kwatu,wanoabudu ya watu.
Haishiki kutu katu, haipambi ukurutu.
Shairi lilo hisia, hakika talirudia.
Wanoumwa subiria, zipo dawa nawagea.
Tamathali ndo tumia, siku zote kwa kwongea.
Hisia sije achia, mafumbo sije tegea.
Shairi liwe makini, lipambwe vina mizani.
Iwe dhiki au nema, sintopotosha asili.
Lilo baya liwe jema, mi si pungufu akili.
Sintochelea kusema, japo meshika makali.
Shairi ni kama tumbo, njaa yake iwe wimbo.
Tamati nina kiburi, lughaye ni Kiswahili.
Yatamba zote bandari,yauza bila dalali.
Wateja haisubiri, wafata wale asali.
Napenda tena andika, shairi la kusomeka.