Mbali na hilo, ushindi wa Pascal umekosolewa ‘kiduchu' na wadau kwamba licha ya kuwa msanii huyo ana sauti nzuri, yenye nguvu na pumzi lakini alifanya makosa wakati wa fainali ambayo hayakukosolewa na majaji.
Ilielezwa na wadau kuwa, mshindi huyo wa mwaka huu, alikuwa na tatizo la kukatika pumzi mara kwa mara wakati anaimba lakini majaji hawakumkosoa, badala yake walimpongeza, hivyo kuondoa uhalisia wa uwepo wa majaji siku hiyo.
Katika hilo, Samson Kashlata wa Mbezi Beach, Dar alisema kuwa, inawezekana majaji walishindwa kukosoa baada ya kuona sehemu kubwa ya wahudhuriaji wa fainali walikuwa wanampongeza.
"Suala hapa ni kusema ukweli, nakubali kuwa, Pascal ni mzuri lakini siku hiyo alifanya makosa mengi ya kitaalamu jukwaani, pumzi ilikatika halafu majaji hawakukosoa, hii si sawa. Ushindi angepewa lakini angekosolewa kwanza kwa sababu leo (usiku wa kuamkia Jumatano) amefanya shoo mbaya.
"Ingependeza majaji wetu wamuige Jaji Ian wa Project Fame, yule jamaa ilikuwa hata mashabiki washangilie wote lakini ukikosea kitaalamu atakukosoa tu, tunataka na hapa iwe hivyo," alisema Samson.
Wadau pia, walimshauri mtaalamu wa ‘voko' za Kiingereza, Kelvin kujiandaa na mashindano ya Project Fame Season Four kwa maelezo kuwa uwezo wake unatosha kumfanya mshindi katika mashindano hayo.
"Kelvin ana uwezo mkubwa, hapa wapigakura wa Tanzania ni wale wenye mitazamo ya ki-Bongo Flava zaidi, naamini Kelvin ni bonge la mwanamuziki, kwahiyo naamini kule atafanya vizuri kwa sababu sauti yake inakubalika kimataifa," alisema Sadala K wa Sinza, Dar.
Kukamata nafasi ya nne kwa mshiriki kutoka Tanga, Jackson kumechukuliwa kama maajabu kwa kuwa historia inaonesha kwamba, tangu mashindano hayo yafikie hatua ya 20 Bora, alikuwa ni mmoja kati ya waliopokea misukosuko mingi ya kutoka.
Hata wakati 10 Bora inatangazwa, Jackson alionekana kuingia hatua hiyo kwa staili ya kupenya katika tundu la sindano kwa sababu mara kwa mara alitajwa kuwemo kwenye orodha ya waliokuwamo katika mstari wa kutoka.
Mshiriki huyo wa Tanga, pia alilamba msoto 10 Bora, baada ya kuingia na kujikuta akiwekwa kwenye mstari wa hatari, ingawa alipona na kubaki Saba Bora kabla ya kufanya ‘wandaz' na kutinga Tano Bora a.k.a fainali.
Katika kuingia Tano Bora, Jackson alifanyakazi ya ziada, akisaidiwa na wapigakura ili kumuondoa aliyekuwa mshiriki mwenye kipaji kikubwa, Catherine Ntepa.
Maajabu ya Jackson, pia yalijionesha siku ya fainali ambapo aliweza kukusanya kura nyingi kumzidi Kelvin ambaye aliokolewa na majumuisho ya kura za nyuma ambazo zilimuwezesha kubaki nafasi ya tatu.
Aidha, kwa ushindi wa nne mbele ya Beatrice, Jackson pia anatafsiriwa kuwa alifanya ‘wandaz' kwa kumtoa ‘knock out' dada huyo, aliyelitawala shindano hilo kwa muda mrefu wakati linaanza.
Ushindi wa Pascal, pia nao unatafsiriwa kama maajabu yaliyotokea, kwani wakati anaanza, baadhi ya majaji, hasa Joachim Kimaryo ‘Master Jay' walimuelezea kuwa habebeki katika soko la muziki kutokana na sauti yake ‘kubezi' katika nyimbo za kanisani.
Hata hivyo, ubishi wa Chifu Jaji wa BSS, Rita Paulsen ‘Madam' kuwa Pascal a.k.a Baba Rita ni mwanamuziki mzuri na anaweza kubadilika, ulizaa matunda kwani baada ya staa huyo wa Bongo kwa sasa, kuanza kuimba staili nyingine, alijichotea mashabiki wengi waliomfikisha alipo.
Kutokana na uwezo wake wa kubadilika na kuimba staili mbalimbali, Pascal alipewa a.k.a ya Mzee wa Mavoko, ikiwa ni zawadi ya majaji na mashabiki kukubali sauti yake nzuri na yenye nguvu anapoimba.
Mbali na hilo, Rita ambaye pia ni Mkurugenzi wa Benchmark Production inayoratibu BSS, amepongezwa kwa kubuni shindano hilo kwa kuwa sasa linatoa mwanga mpana wa mafanikio kwa vijana wenye vipaji.
Hata hivyo, Rita ameshauriwa kuwasimamia wanamuziki wake ipasavyo yaweze kufika mbali ili yasije kutokea yale ya akina Jummne Idd (mshindi BSS 2007), Misoji Nkwabi (BSS 2008), Rogers Lucas (BSS namba mbili 2008) na wengineo.
Rita, ameshauriwa pia kuendeleza vipaji vya washiriki wa mwaka huu, kama Peter, Beatrice, Catherine na wengineo kwa kuwa wao wakifanikiwa, ni kielelezo tosha cha mafanikio ya BSS na harakati zake.
Aidha, kubwa lililozungumzwa na wadau ni majaji kwamba wakati mwingine walikuwa wanaelemewa na mapenzi binafsi kwa baadhi ya washiriki na kushindwa kufanya uamuzi sahihi pale ilipohitajika.
Janet Byemerwa wa Makongo, Dar alisema: "Hatukatai mtu kumpenda yule anayekuvutia, lakini kama jaji hutakiwi kuonesha mapenzi wazi wazi. Kubwa ambalo nililiona tangu shindano hilo likiwa kwenye mchujo ni kauli za majaji, kuna watu ambao walipondwa na wanaweza lakini wapo waliosifiwa ingawa hawakuwa na uwezo.
"Tulipofika 10 Bora ndiyo ikawa tatizo kabisa, mshiriki mwenye uwezo mkubwa anapondwa kwa sauti kali tena ya juu, wakati yule ambaye wanampenda wao hata akiboronga wanamsifia tu, kwahiyo tunaomba mwakani mambo haya yasijirudie."
Gazeti hili linampongeza Madam Rita na timu yake nzima kwa kuwezesha BSS kufikia hatua iliyopo. Sisi Ijumaa tunaamini kuwa BSS ni mkombozi wa vijana, pia tunampongeza Pascal kwa ushindi wake. MHARIRI.
http://www.globalpublisherstz.com/2009/10/16/az_bss_2009.html