Nataka nianze Elimu ya Ngumbalu nisomee Uandishi wa Habari na mimi niwe Mwanahabari

Nataka nianze Elimu ya Ngumbalu nisomee Uandishi wa Habari na mimi niwe Mwanahabari

Kijana wa Ifoza

JF-Expert Member
Joined
Oct 31, 2025
Posts
1,180
Reaction score
2,302
Wakuu wa JamiiForums, habari za wakati huu.

Leo nimeamua kuja mbele yenu kufungua moyo wangu kuhusu ndoto ambayo imelala ndani yangu kwa miongo kadhaa. Hii ni tasnia niliyoipenda sana tangu nilipomaliza elimu ya Sekondari. Mapenzi yangu kwenye uandishi na utangazaji wa habari hayakuanza leo; yale yalikuwa ni mazingira ya kuvutiwa na kazi zilizotukuka za magwiji walioishi kabla yetu.

Katika ukuaji wangu, nilikuwa na watu walionivutia sana na kuwa masanamu wangu (idols) wa mfano kwenye tasnia hii. Sauti na weledi wa watu kama Mzee Jacob Tesha, Uncle J (Julius Nyaisanga), Mzee Charles Hilary Nkwanga, Salum Seif Nkamba (S.S. Nkamba, Mzee wa Mikingamo), Mshindo Mkeyenge, na Khalid Ponera zilikuwa zikiteka masikio yangu na kunijenga kila siku. Nilitamani sana kuwa kama wao.

Shauku hii ilikuwa kubwa kiasi kwamba nakumbuka mnamo mwaka 1988, nilifunga safari kwenda pale Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania (TSJ) kuangalia tu yale majengo na kuvuta picha ya siku nitakayokuja kukaa kwenye madarasa yale. Hamu haikuishia hapo; nilizunguka mpaka makao makuu ya RTD kule Pugu Road kuona pale inapopeperushwa Idhaa ya Taifa, na baada ya hapo nikasogea mpaka Mabibo ambako kulikuwa na mitambo na studio za ile Idhaa ya Kiingereza (External Service). Moyo wangu ulikua unadunda kwa shauku kubwa ya siku moja nami kuja kushika maikrofoni au kalamu.

Kama isingekuwa uandishi wa habari, kazi nyingine pekee niliyotaka kuisomea ilikuwa ni usimamizi wa mahoteli (Hotel Management). Kuvutiwa kwangu na sekta hiyo kulinifanya wakati huo nitembelee hata kile Chuo cha Utalii cha Forodhani ili kujionea mazingira yake na kuona namna tasnia hiyo inavyoendeshwa.
Lakini kama wasemavyo, maisha yana njia zake na mipango ya binadamu sio kila wakati inanyooka. Mambo hayakuwa kama nilivyotaka. Kwa ushawishi wa bosi wangu mmoja nilipokuwa nafanya kazi kama kibarua (Temp), aliniambia, "Unaonaje kama utaingia kwenye mambo ya mahesabu?" Basi, mambo yote yakabadilika kuanzia pale. Nikajikuta nimeingia kwenye tasnia ya namba na kuwa karani wa mahesabu, kazi ambayo nimeifanya kwa muda mrefu lakini bila kuwa na ule upendo wa dhati wa kutoka moyoni.
Sasa nimeona inatosha. Huu ni wakati wangu na mimi kutimiza kile ninachokipenda kutoka moyoni mwangu—au kama wenzangu Wapogoro wanavyosema, "Niifira mpaka kumoyo". Nataka nianze Elimu ya Ngumbalu (Elimu ya Watu Wazima) ili hatimaye nisomee uandishi wa habari na kutimiza ndoto yangu ya kuwa mwanahabari kamili. Umri na majukumu yasinifanye nife na ndoto yangu mfukoni.


Mwisho kabisa, namuomba ushauri mzee wangu na nguli wa tasnia hii hapa jukwaani,Pascal Mayalla. Mzee wangu, kwa uzoefu wako mkubwa kwenye tasnia hii ya habari: Je, nimechelewa? Je, soko la sasa na mifumo ya sasa ya habari itanipokea mtu mzima niliyeamua kuanza upya kupitia Ngumbalu? Pia kwa mtazamo wako, weledi wa kizazi kile cha dhahabu cha akina Jacob Tesha, Julius Nyaisanga na S.S. Nkamba tunaweza kuuamsha tena kupitia safari yangu hii?

Nawasilisha kwenu wakuu kwa ushauri, maoni, na miongozo yenu.
Asanteni.
 
Back
Top Bottom