SoC03 Natamani usiku ungelikuwa mchana

SoC03 Natamani usiku ungelikuwa mchana

Stories of Change - 2023 Competition

LEZIMA

New Member
Joined
Jun 1, 2023
Posts
3
Reaction score
4
Ulikuwa ni usiku wa Jumamosi, uso wa dunia ikiwa umekumbatiwa vilivyo na giza nene. Laiti kama mtu angelitoka kutembea nje kwa usiku ule, pengine asingeweza kuona hata kile kilichokuwa hatua moja mbele yake.

Ni usiku huo ambao ulileta mabadiliko katika maisha ya Jabali aliyekuwa akiishi katika Kijiji cha Makondeni. Ilikuwa imepita miezi miwili tu tangu Jabali achaguliwe kuwa mwenyekiti wa Kijiji kile.

Usiku huo Jabali akiwa amelala, alisikia sauti za watu wakiwa wanaongea nje ya nyumba yake, licha ya kuwa watu wale walikuwa wakinong'ona, lakini bado sauti zao zilipenya mpaka kwenye ngoma za masikio ya Jabali.

Alifanikiwa kuyasikia maneno machache waliyokuwa wakiyaongea watu wale bila hata haya huku wakibishana.

Pamoja na kuwa Jabali hakuwa na mpango wa kuamka, lakini maneno aliyokuwa ameyasikia kutoka nje yalikuwa yamekwishamchafua nyongo. Hivyo, akaamua kutoka nje, kutokana na giza nene lililokuwa limetawala nje, aliamua kuchukua tochi ili imsaidie kutembea katika lile giza.

"Kwanini mnapenda kuwa mabundi? Wakati Kama huu mlitakiwa kuwa mmelala vitandani mwenu mkiwaza namna ya kuvisaidia vijiji vyenu ambavyo vinanuka karaha kila siku. Mnashindwa hata kufikiria namna nzuri ya kuwafundisha watoto wenu wapendane au kuwafundisha amani ni nini, mnakalia kuwaza kuja kunipotosha kila siku mnafikiri mtafanikisha mpango wenu?" Aliongea Jabali kwa jaziba baada ya kuwamulika kwa tochi watu wale na kugundua kuwa ni walewale walikokuwa wamekuja usiku uliopita.

"Hapana Jabali, sisi tuna lengo la kukusaidia wewe na wanakijiji wako, tazama mpaka leo nyumba yako na Kijiji kizima hakuna nyumba yenye umeme. Tunakuahidi Kama utatutimizia hiki tunachokitaka, kesho tutakuwekea umeme kwenye nyumba yako nawe utafurahi." Aliongea mtu mmoja miongoni mwa wale watu waliyokuwa mbele ya Jabali.

"Ahahah! Na hilo ndilo tatizo lenu. Naona hamjanijua bado, hebu fahamuni hivi leo kuwa mimi sikuomba kuwa mwenyekiti ili nipate umeme au ili niishi Kama nyie mnavyoishi, na wala msidhani kuwa ule unafiki wenu mlionioneshea ili niwe kiongozi kwamba utanilewesha Leo hii mpaka nikawasikiliza hizo pumba mnazoziongea.

Mimi ndiye Jabali, nafahamu kilichoniweka hapa, nipo hapa kwa sababu niliwaona wanakijiji wakiteseka na kulia kila siku pasi na kupata msaada walipokuwa chini ya mwenyekiti ambaye ninyi mabundi mliichota akili yake halafu mkaiweka kwenye viganja vyenu, mkafanikiwa kumwendesha kama mlivyotaka wenyewe.

Bongo zenu leo na zikaririshwe kuwa mimi siwezi kutembelea nyayo za wale mliowaweza ninyi. Mnajua ni kwa nini? Ni kwa sababu hamjaniweza. Ahahah!" Aliongea Jabali kwa dharau sana halafu akafunga mlango na kuingia ndani.

Wale watu walibaki kimya kwa muda pale nje, maneno ya Jabali yakawa yamewavunja maini na kuwayeyushia matumaini yaliyokuwa yameota mizizi mioyoni mwao. Mmoja wao akauvunja ukimya kwa kusema kwamba, "mbona mnakuwa wepesi wa kukata tamaa kiasi hicho? Mmesahau kuwa hata mwenyekiti wa awamu iliyopita alikuwa anajifanya mbishi Kama huyu lakini tulipomletea pesa akasahau kuwa aliapa nini.

Mimi naona bado hatujachelewa, turudi tukajipange tena halafu kesho usiku tuje na pesa zitakazompumbaza akili, ninaamini tukishampumbaza hatakuwa na jeuri ya kuyasema hayo aliyoyasema leo. Pengine atasahau hata hicho kilichonifanya awe mwenyekiti."

Siku iliyofuata, Jabali aliamka asubuhi na mapema ili kwenda ofisini kwake, alikuwa akipitia mafaili mbalimbali kama aliyekuwa akitafuta taarifa fulani halafu baada ya kuipata ile taarifa, alilichukua faili lililokuwa na taarifa ile na kurudi nalo nyumbani.

Jabali alipofika nyumbani kwake, alimkuta mkewe akiwa amekwishamuandalia chai na maji ya kuoga, aliingia ndani akaweka lile faili kisha akaingia bafuni kuoga.

Ikumbukwe kuwa siku hiyo ilikuwa Ni jumapili, hivyo baada ya kunywa chai, Jabali alienda kanisani. Siku zote alikuwa anaamini kuwa Mungu ndiye atakayemsaidia katika uongozi wake. Alikuwa alitamani sana kuwatumikia vema wanakijiji na kuyafanya yale aliyoahidi kuwafanyia ili kuleta maendeleo.

Na maendeleo aliyokuwa akiyataka sio yale ambavyo wale wageni kutoka vijiji vingine walikuwa wakidai watamtimizia kama akiwaruhusu wafanye walichokuwa wakikitaka, bali alitaka yeye pamoja na Wanakijiji wawajibike kwa nguvu zao wenyewe ili wapate maendeleo na mafanikio yasiyo na jasho la mtu mwingine. Aliwaaminisha Wanakijiji kuwa wakifanikiwa kwa jasho lao wenyewe, hawatskuwa watumwa wa mtu yeyote yule.

Siku iliyofuata wale wageni walikuja tena kumshawishi Jabali wakidhani huenda siku hiyo watafanikiwa kuulainisha moyo wa Jabali na kumfanya afanye lile walichokuwa wakikitaka.

Kama ilivyokuwa kawaida yao, wageni wale hawakuwahi kuja nyakati za mchana bali usiku. Siku hiyo idadi yao ilikuwa imeongezeka. Walimgongea mlango Jabali kisha akatoka. Walianza kumuonyesha fedha wakisema, "Kama utakubali kufanya kile tunachokitaka, hizi zitakuwa zako." Lakini hilo halikupenya hata kidogo katika masikio ya Jabali, ni kama sauti ile iliingilia sikio la kulia na kutokea katika sikio la kushoto.

Mwingine akasema, "mbona Hawa wenzako wanafanya kile tunachowaamuru tena wana mafanikio makubwa kuliko wewe na Wanakijiji bado wanawapenda, Ni kwa nini wewe unajifanya nunda?" Jabali alijibu "hao si mimi na mimi siwezi kuwa wao."

Jabali akawageukia wale ambao mchana waliofanya kuwa ni viongozi bora halafu kumbe usiku wanashirikiana na wale matapeli wanafanya mambo kwa manufaa yao wenyewe. Baada ya kuwatazama kwa muda akawaambia, "je, so ninyi ambao Wanakijiji wamewaamini na kuwaona mnafaa kuwakomboa?

Sasa mbona mnawaza kujinufaisha wenyewe? Mbele za watu wenu mnajifanya kuwa kondoo kumbe ndani Ni mbwa mwitu! Daah! Natamani huu usiku ungelikuwa mchana ili maovu yenu yawekwe wazi na kila mtu ajue uhalisia wenu.

Watu wale walipoona kuwa Jabali hadanganyiki, waliamua kuondoka zao na wala hawakurudi tena. Jabali aliendelea kuwatumikia Wanakijiji huku akiwahimiza wafanye kazi kwa bidii ili waweze kufanikiwa.
 
Upvote 3
Back
Top Bottom