Kupanda kwa nauli: SUMATRA yawapa kibarua TABOA Friday, 07 January 2011 09:32 *Wataka nauli zipande mara dufu
Na Waandishi Wetu,jijini
WAKATI Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo Mikoani (TABOA), wakijipanga kushinikiza kuwe na ongezeko la asilimia 100 la nauli kwa abiria waendao mikoani, Chama cha Kutetea Abiria (CHAKUA), kimewajia juu na
kudai kuwa hawakubaliani na ongezeko hilo.
Akizungumza leo asubuhi, mshauri wa CHAKUA, Wilson Mashaka, amesema ongezeko hilo ni kubwa na wananchi hawataweza kulimudu kutokana na hali ya uchumi ilivyo hivi sasa.
Amesema ni kwa muda mrefu baadhi ya wa wananchi wamekuwa wakishindwa kusafiri kwenda mikoani kutokana na ukosefu wa nauli hali ambayo inatokana na ugumu wa maisha unaozikabili familia nyingi.
Tumekuwa tukitaniana sana mitaani huko kwamba watu hawaendi makwao hadi wapate misiba, je nauli ikiongezeko si ndiyo kutakuwa kuna hatari ya wengi kushindwa kwenda vijijini kwao kuwasalimia ndugu na jamaa, amesema Mashaka.
Ameongeza kuwa kutokana na hali halisi ya maisha ya Watanzania wengi, CHAKUA haikubaliani na ombi la kuongeza nauli na badala yake watafute mbinu mbadala ambayo itawasaidia wamiliki hao kuendesha biashara yao.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini ( SUMATRA), Gilliard Ngewe, amesema bei za mabasi zibakie kama zilivyo na amewashauri wamemiliki wa mabasi wanunue mabasi ya bei nafuu ili kuendesha biashara yao bila matatizo.
Amesema kinachochangia kupanda kwa nauli siyo bei kubwa ya mafuta kama inavyodai TABOA bali kuna sababu nyingi zikiwamo za kuzagaa kwa wapiga debe vituoni na ushuru wa aina mbalimbali.
Endapo SUMATRA itakubali ombi la wadau wa usafiri nchini itazidi kuwapa ugumu wa maisha wananchi wenye kipato cha chini ambao ndiyo walengwa wa usafiri huo.
Kutokana na bei hizo mpya zilizopendekezwa na TABOA, abiria wanaotoka Dar es Salaam kwenda Arusha watatakiwa kulipa sh. 43,000 kutoka 16,000 ya sasa na Dar es Salaam kwenda Mbeya itakuwa sh. 58,000 badala ya sh. 22,000.
Bei hiyo elekezi ya TABOA, kwa mujibu wa Katibu wa chama hicho, Wilbroad Mtenga, aliomba kila abiria alipe sh. 69.80 kwa kilometa moja badala ya sh. 26.6 ya sasa, sawa na ongezeko la asilimia 163.
Hata hivyo, msimamo wa SUMATRA uliotolewa jana ulipinga maombi ya TABOA ya kutaka nauli ipandishwe kwa kiasi hicho wakiungana na wanasiasa wa vyama mbalimbali na wananchi.
wanaJF kazi kwetu maisha yanazidi kuw magumu kila kona. je tutafika au nchi imeshauzwa kwa wenye nazo?