MFUMO wa ulipaji nauli kwa mabasi ya abiria jijini Dar es Salaam na miji mingine nchini maarufu kama daladala, express na vifodi, uko mbioni kubadilika kwa abiria kulazimika kulipa nauli kwa kilometa watakazosafiri.
Hayo yamo katika mapendekezo ya Chama cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (DARCOBOA), kinachopendekeza ongezeko la nauli, lakini katika mfumo wa kulipa kwa kilometa.
Imependekezwa, mtumiaji wa daladala alazimike kulipia Sh 51 kwa kilometa, ili wamiliki wa vyombo hivyo vya usafiri wamudu gharama za uendeshaji ambazo zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku.
Hii ina maana kwamba, endapo pendekezo hilo litapita, kwa abiria anayetoka kwa mfano Bunju kwenda katikati ya Jiji, atalazimika kulipa Sh 1,530 kwa safari moja, na kama atarudi, basi kwa siku atalipa Sh 3,060.
Darcoboa walitoa mapendekezo hayo jana katika kikao cha wadau cha kukusanya maoni na kufanya mapitio ya ongezeko la viwango vya nauli za daladala Dar es Salaam yatakayoisaidia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), kupanga nauli.
Akitoa maoni yake, Mwenyekiti wa Darcoboa, Sabri Mabruk, alisema matumizi ya mafuta kwa kilometa moja ni lita tatu, huku bei ya mafuta kwa sasa ikiwa ni Sh 1,800 kwa lita, hali ambayo imekuwa ikiumiza wamiliki na kushindwa kuyafanyia matengenezo magari yao.
Alisema mwaka 1995 umbali usiozidi kilometa 10, nauli ilikuwa ni Sh 150 huku mafuta yakiuzwa Sh 385 kwa lita, lakini bidhaa nyingine zimekuwa zikipanda kwa kasi zikiiacha nauli chini huku vipuri na mafuta vikiendelea kupanda.
Kwa kipindi cha miaka 10 nauli ya daladala peke yake imebaki chini, yaani nauli imezidi kukandamizwa wakati tunasafirisha askari bure na watu wenye vitambulisho wakiwamo wanafunzi
jamani tuitendee haki sekta ya usafirishaji, alisema.
Alisema pamoja na kiasi hicho kidogo cha nauli wanachotoza, lakini gharama za uendeshaji ni kubwa, miundombinu mibovu hali inayofanya safari kutoka Ubungo hadi Buguruni, kutumia saa moja hadi nne kutokana na foleni, ambapo pia uchakachuaji wa mafuta unawaathiri zaidi katika kutoa huduma hiyo.
Kutokana na hali hii tunapendekeza nauli iwe Sh 51 kwa kila kilometa, kwa maana kwamba anayetoka kilometa 30 azidishe mara 51
kila mtu alipe nauli kulingana na umbali ili kila mtu abebe mzigo wake, alisema.
Aidha, utaratibu huo ukikubalika, wanapendekeza kupimwa na kuwekwa alama zitakazoonesha umbali, kwa maana ya kilometa kwa lengo la kupunguza malalamiko ya abiria.
Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), kilipinga mapendekezo hayo na kuwataka wamiliki kuboresha magari yao ambayo mengi ni kero hasa wakati wa mvua na kusema zipo njia nyingi za kuwaongezea mapato, ikiwamo kuondoa wapiga debe ambao wamekuwa wakilipwa kila siku.
Akijibu hoja hiyo, Katibu Mkuu wa Darcoboa, Mujengi Gwao, alisema ni kweli wana magari
mabovu, lakini hawatayarekebisha kwa nauli ya Sh 250 na kwamba wapiga debe hawawahitaji na walishazindua mpango wa kuwaondoa, lakini Serikali imeshindwa kuusimamia.
Aidha, waliiomba Sumatra kuelekeza makosa ya mtendaji na kumhukumu badala ya kila kosa la dereva kuelekezwa kwa mmiliki na wakati mwingine kudaiwa faini kubwa kwa kosa la kwanza tena bila onyo.
Madereva nao walisema hata nauli ikipandishwa na kuwa Sh 500, yasipoondolewa magari mabovu barabarani, bado itakuwa ni hasara kutokana na wenye magari hayo kushusha nauli ili kuvutia abiria.
Kwa upande wao Baraza la Watumiaji wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra CCC),
walipinga ongezeko hilo na kutaka kila kilometa itozwe Sh 29 na kutaka tatizo la msongamano wa magari liondolewe na kuboreshwa miundombinu ili kupunguza gharama za uendeshaji.
Akihitimisha mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Israel Sekirasa, alisema wanaendelea kupokea maoni hadi Januari 15 na kuwataka wasafirishaji hao kutowaona askari Polisi, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Magereza kuwa ni mzigo, kwa sababu kila wanapokuwa katika vyombo hivyo, wako kazini na kuongeza kuwa, baadhi ya majeshi yameendelea kununua magari kwa ajili ya watumishi wao.