SoC03 Nchi isogiza

SoC03 Nchi isogiza

Stories of Change - 2023 Competition

Enigmatic_

Member
Joined
May 12, 2023
Posts
16
Reaction score
13
Sauti ya nyenje na wadudu wengine iliendelea kunisindikiza taratibu kuelekea nisipopajua. Safari yangu niliyoifanya wiki moja ilinichosha na kunipotezea matumaini. Jua lisilokoma liliendelea kujenga uzio mkubwa kichwani mwangu. Adha zote hizi zilizalishwa na upepo wa “ijue dunia” Uliovuma kutoka pande mbalimbali za kichwa changu.

Baada ya kutembea sana, hatimaye nilifika kwenye nchi iliyojipatia umaarufu duniani kote. Nchi hiyo, iliyotawaliwa na mchanga wa pwani, ilipata umaarufu kutokana na kuwa na vivutio vingi vya utalii. upepo uliostaarabika ulivuma kila kona ya nchi na kuleta harufu nzuri ya ardhi iliyotunzwa. Hakika kuangusha mguu wangu katika nchi ile kulinijazia vifurushi vya matumaini.

“Mageshi!” ilisikika sauti nzito iliyojaa mikoromo. Nilishtuka kisha nikajigeuza taratibu tamthili ya chatu aliyemeza ng’ombe. Kuitwa jina langu lilikuwa jambo geni. “Aahe!” nilijiongelesha kwa hamaki baada ya kuona kiumbe mkubwa mwenye umbo kama sokwe na shingo ndefu kama korongo akinifuata chini ya mnazi niliojiketisha. Kila mguu wake ulipotua, ardhi ililalama, na kutoa vumbi kama machozi yake. Suruali yangu nzito ilinitolea aibu baada ya kuzuia chemichemi kufikisha maji juu. “ogopa kisichooneka kuliko kinachoonekana!” aliongea kiumbe Yule huku akinisogelea. Tetemeko kubwa la mwili liliendelea kupita kadri kiumbe Yule alivyonisogelea. Unyonge wangu na hali ya kutoongea chochote, kutokana na
njaa na woga, kulimfanya kiumbe Yule kunishika mkono, na kunipeleka kwenye pango moja kubwa.

Ndani ya pango lile niliwakuta viumbe wale wakipata chakula. Nilipelekwa katikati ya ukumbi wa pango, na kisha kiumbe Yule akapiga makofi matatu kwa nguvu, na hatimaye macho ya ukumbi mzima, yaliyokuwa kama kurunzi, yakahamia kwetu. “Kiswahili! Kiswahili!” aliongea huku akinishika bega langu. Ukumbi mzima ulisimama na kisha sauti za “karibu! Karibu!” zikasikika. Majibu yao na hata sura zao vilionyesha kujua lugha na vitu vingi duniani. “Asante!” nilijibu. Baada ya hapo nilipelekwa kwenye chumba maalum, nikaletewa chakula nisichokijua⸺ ambacho sikuwahi kukiona katika maisha yangu. Lakini, Kama debe tupu halikatai mkaa, mimi ni nani hata ningekataa chakula? Tangu lini mwenye njaa akachagua chakula? Nilikula!

Ulipita mwezi mmoja huku nikiona vitu vya tofauti sana. Jua katika nchi ile halikuzama. Usiku wala kiza havikuwepo. Ubukuzi wa jamii ya viumbe wale ulinishangaza. Si viumbe wadogo wala wakubwa; wote walikuwa wabukuzi haswa! Ngamizi na simujanja zao ziligeuka nyavu nzuri za uvuvi wa maarifa. Nilitamani kuuliza, lakini pepo msafi wa utulivu alinipitia.

Hakika mwenye hamu ya kujua hutaabika kuliko kinyume chake. Siku moja niliamua kukitoa kinywa changu kwenye kifungo cha muda mrefu. “je!” niliongea huku nikimsogelea kiumbe mmoja aliyekuwa na tumbo mithili ya kichuguu. “kipi hasa kimefanya hata usiku na kiza visiwepo katika nchi hii?” “kwa hakika,” alisema huku akijishika kidevu chake kilichokirimiwa na ndevu chache mithili ya kambale. “kiza na mwanga havichangamani lakini havitengani. Huachiana nafasi.

Kwa hiyo, palipo kiza mwanga hujiweka kando akisubiri kuitwa. Imekuwa jadi kwa viumbe wageni kwenye ardhi hii kusema hawaoni kiza bali mwanga. Kuna ukweli ulionakishiwa kwenye hilo.” Alitulia kidogo, kisha akaendelea, “kuona kiza na mwanga ni kazi. Yahitaji muda. Yahitaji matumizi ya maarifa uliyonayo. Yahitaji maarifa yaliyochotwa kwa nguvu zako mwenyewe, si za kuhamishiwa. Maarifa hayo, wengine husema hutokana na kujifunza kwa kuhoji. Bila shaka umebumbuwazika kuona kila kiumbe⸺ si mkubwa wala mdogo akihangaika kuyatafuta bila mwalimu. Imani yetu huku ni kwamba ukizaliwa, tayari wewe ni mwanafunzi, kwa hiyo kujifunza ni lazima. Mapana ya ulimwengu hayawezi fundishwa kwa muda mfupi upatikanao shuleni. Haiwezekani.”

Baada ya kuongea hivyo alinyanyuka taratibu na kuingia pangoni. Muda mfupi baadaye alirudi akiwa na kitu chenye kufanana na kioo kidogo. Alikaa gogoni kisha akaniashiria nimsogelee. Alichukua kifaa kile na kukisugua kwenye tumbo lake lililoishiwa manyoya mithili ya jangwa lisilo na miti. Bila shaka ilikuwa ni ishara ya idadi ya viroba vingi vya chumvi alivyobwia. “Angalia” alisema huku akinisogezea kifaa kile machoni mwangu. masalale! nilishtuka baada ya kuona kitu kikubwa kama mpira wenye rangi aina aina kikizunguka kwa kasi ya kimbunga.

Kiumbe Yule alicheka huku meno yake yaliyoachiana nafasi yakipata fursa ya kuonekana. “Dunia inazunguka kwa kasi. Kwa kasi mno. Elimu inayonyata haiwezi kwenda na dunia hii. Elimu ipatikanayo na kuishia darasani si elimu bali ni utumwa uliohalalishwa. Hakika ni utumwa. Na, kama ujuavyo, elimu ni moyo wa nchi. Nani asiyejua matatizo ya moyo yahatarishavyo maisha? Uhai wa nchi unategemea afya ya elimu yake.

Sasa dunia inataka wanariadha mashuhuri haswa. Wanariadha wanaoweza kufukuzana nayo. Dunia inataka viumbe wenye ashki na maarifa. Inataka nchi zilizowekeza katika maarifa; katika matumizi na uvumbuzi wa kiteknolojia, tupo pamoja?” “ndiyo”

Baada ya jibu langu, kiumbe Yule aliupitisha ulimi wake kuzunguka mdomo wake, kisha akaendelea: “lengo la elimu si kuwafanya viumbe wajue kusoma na kuandika, bali ni kuwafanya waijue na kuitumia vyema asili, na kuwafanya waijue jamii yao na jamii zinazowazunguka. Si rahisi sana kwa walimu kufundisha mambo yote haya katika muda upatikanao shuleni. Hakika haiwezekani.

Jambo kubwa na la muhimu ni kutengeneza jamii ya wawinda maarifa. Ni kutengeneza jamii ambayo mwalimu sio mwanzo na mwisho wa maarifa! Katika jamii hiyo, mwalimu si safari, bali ni sehemu ya safari. Kufanya kazi kama hii yahitaji mtaji wa muda. Kufanya mabadiliko kama haya yahitaji kuvunja miiko na myenendo ya zamani! Lakini nani asiyejua ya kuwa penye nia pana njia? Nani?! Nani?! Tazama sasa, sisi twaona giza na mwanga!” Aliongea kwa msisitizo, na baada ya kumaliza, alinyanyuka na kuelekea pangoni…

***
Sauti ya jimbi iliangusha rungu zito sikioni, na kunifanya nishtuke. Baridi kali ya juni iliniparamia, na kunikumbusha kuvuta blanketi. Hakika sikuamini kwamba nilikuwa ndotoni. Niliamka alfajiri ile, nikiwa na furushi kubwa la mawazo. Sauti nzito ya kiumbe Yule iliendelea kurindima kwenye ngoma za masikio yangu. Maneno “giza na mwanga” yaliusurubu mtima wangu. Mvua ya hekima iliyonyesha kutoka kinywani mwake ilinishajiisha. Nilitamani kurudi ndotoni walau nikaweke makazi huko, lakini hakukuwa na uwezekano. Nilitamani kuchukua kipaza sauti na kutangaza ndoto ile, Lakini niliwaza: ningewezaje hasa kusema kuhusu ndoto, kitu cha kufikirika, na nikaeleweka? Nilikaa kimya, na nitaendelea kukaa kimya: tangu lini ndoto ikaaminika?
 
Upvote 1
Back
Top Bottom