Ndani ya CCM watu wanaogopana nahawataki kuambiana ukweli. Lazima tutafute tiba ya rushwa na tuache unafiki

Ndani ya CCM watu wanaogopana nahawataki kuambiana ukweli. Lazima tutafute tiba ya rushwa na tuache unafiki

Kiwalani finest

Senior Member
Joined
Jul 6, 2024
Posts
116
Reaction score
85
Siku tutakapopeana makavu live bila chenga, machawa watakaibika. Siku hiyo itakuwa mwanzo sahihi wa kuitokomeza rushwa na kuunyonga unafiki.

Nakumbuka tarehe 13/03/2023, Profesa Anna Kajumulo Tibaijuka — aliyewahi kuwa mtumishi wa mashirika ya kimataifa, Waziri wa Ardhi, Mbunge wa Muleba — alisema: “Mzee kama mimi hapa, kama kuna jambo la kulisema, nalisema. Lakini nalisema constructively nichangie lifanyiwe kazi.” Mwisho wa kunukuu.

Ndani ya chama watu tunaogopana kuchanana hadharani. Ili kuepuka kuchukiwa au kutengwa, tunalazimika kuishi maisha ya kinafiki ya kuushangilia uongo huku ukweli ukiwa wazi. Tumekosa hofu ya Mungu na kumkaribisha Shetani ili atende kazi ya kuudumisha unafiki.

Tarehe 13/03/2025, Sheikh Othman Khamis Juma wa Masjid Mwinyiamani alisema: “Mtu yeyote akimuogopa Mwenyezi Mungu inavyotakiwa hapa duniani, ajue kila kinachomtisha kitakuwa ni amani kwake. Wanaomuogopa Mungu hawaogopi kitu kingine.” Mwisho wa kunukuu.

Tuna Ilani, Katiba, Kanuni, Miongozo na Taratibu. Zinataka wenye nacho na wasio nacho watendewe haki. Lakini nguvu ya rushwa huchezewa na njaa za watu. Wengi wasioelewa siasa hujikuta wakijipendekeza kwa watoa rushwa wakitaka hata nafasi ya kuwa machawa, mradi mkono uende kinywani.

Nakumbuka tarehe 24/03/2025, Profesa Anna Kajumulo Tibaijuka alisema: “Karl Marx alisema: Power makes law — yaani mwenye mamlaka ndiye anaweka sheria.” Mwisho wa kunukuu.

Tunayaona haya: mtu ananunua cheo kwa rushwa bila kujua ilani ya chama, Katiba wala miongozo. Kisha anaanza kupanga safu za viongozi wengine wasiostahili. Hatimaye, anajenga mazingira ya kutokuwajibishwa. Anabaki madarakani akiongozwa na hisia zake binafsi. Wenye njaa kali — wanaojua haki na wasioijua — wote wanamiminika kwa mtoa rushwa, wakifanya vitendo vya hovyo kwa hofu ya kuukosa ubwabwa wa dezo.

Wakati wa uchaguzi, watu wenye njaa kali huanza kumtafuta mtu mwenye fedha ili wamshawishi agombee, hata kama hajui lolote kuhusu ilani au taratibu za chama. Hii ni sawa na kumuokota mchinjaji wa nguruwe ukamfanya aswalishe msituni.

Je, uzalendo wetu uko wapi? Je, tuna hofu ya Mungu? Tumeacha hata kuona aibu?

Nakumbuka tarehe 28/03/2025, Mufti Abubakar bin Zuber bin Ally Bin Mbwana alisema: “Kufikiri saa moja ni bora kuliko ibada ya mwaka mzima.” Mwisho wa kunukuu.

Tarehe 12/03/2025, Sheikh Othman Khamis Juma alisema: “Mtume Muhammad (SAW) alikuwa mwalimu wa viumbe.” Mwisho wa kunukuu. Kama hatumfuati mwalimu wetu katika kufikiri, je, tunastahili kuwa wafuasi wa nani? Tunapoitwa makafiri tunaonewa?


Sheikh huyo huyo aliongeza: “Watu waliokufuru, Amaal zao ni kama mazigazi ya jangwani. Mwenye kiu anayadhani kuwa ni maji — hadi ayafikie, anakuta si kitu.” Mwisho wa kunukuu.

Nyakati za uchaguzi, wenye njaa huwaona watoa rushwa kama “maji ya jangwani.” Baada ya uchaguzi hukipata cha mtema kuni. Tunapaswa kuwakata watu wa aina hiyo — wasiojua ilani, kanuni wala miongozo.

Tujue: mwenye fedha si kiongozi. Tuache ujinga wa kurithi, tukumbatie ukweli.

Nakumbuka tarehe 06/04/2025, Sheikh Muharram Rashid Mziwanda alisema: “Dini yetu imeagiza tupatanishe na kuwaunganisha watu, lakini tumekuwa tukifanya kinyume chake.” Mwisho wa kunukuu.

Haki za watu zimo ndani ya ilani, Katiba na taratibu halali zisizo na ubatili. Sisi tunawawekea zengwe wenye kustahili na kuwapa wasiofaa. Kisha tunajifanya kuwa karibu na watumishi wa Mungu ili kuficha fitna zetu.

Tarehe 24/03/2025, Profesa Anna Tibaijuka alisema: “Huwa nasema kila saa, tujisahihishe. Lakini mtu mwenye hasira atawezaje kujisahihisha?” Mwisho wa kunukuu.

Watu wababaifu wenye njaa hutanguliza maslahi binafsi kuliko uzalendo. Mgombea aliyechaguliwa kwa fedha huongoza kwa hisia binafsi na nguvu ya unafiki. Akishindwa kuongoza, machawa humgeuka na kuanzisha zengwe ili kutengeneza bifu na kutafuta ATM mpya ya ubwabwa na posho.

Chama ndicho huomba ridhaa kwa wananchi. Kikichaguliwa, huunda serikali yenye wasomi na wataalamu. Wasomi hawa hulazimika kuishi maisha ya kunyanyaswa kwa sababu ya viongozi waliopatikana kwa rushwa.

Tunahitaji mabadiliko. Elimu ya vitabu vya kimfumo isambazwe. Watu wajengewe kujielewa na waelezwe madhara ya kuwa machawa wa “ndiyoooo.”

Askofu Almachius Rweyongeza, tarehe 20/03/2025 alisema: “Baba wa Taifa alipambana na maadui watatu: Ujinga, Umaskini, na Maradhi. Je, tumefanikiwa kwa kiwango gani?” Mwisho wa kunukuu.

Kuhusu adui Ujinga, tujiulize kama tumemfahamu. Adui usiyemjua, anakumaliza.

Wakili Boniface Anyisile Kajunjumele Mwabukusi, tarehe 08/04/2025 alisema: “Kila hoja inayopigiwa kelele ina mantiki, ni lazima ipate ufumbuzi wa kitaalamu.” Mwisho wa kunukuu.

Wakili Othman Masoud alisema: “Jamani mambo mengine hebu tukae tuyafikiri.” Mwisho wa kunukuu.

Lazima kuwepo na uwajibikaji usioangalia nani ana nini. Sasa hivi mtu anaadhibiwa kwa mitazamo yake badala ya matendo yake. Viongozi walikula viapo vya kutokuwa wabaguzi wala wapendeleo, lakini leo tunashangilia adhabu za maskini huku tukilinda watoa rushwa.

Tarehe 21/03/2025, Balozi Dkt Emmanuel John Nchimbi alisema akiwa msibani: “Kitu tulichojifunza kwa Padre Shirima ni nidhamu na uwajibikaji.” Mwisho wa kunukuu.

Nikashtuka ndotoni. Nikasema: Tuchezee vyote, lakini tisie kiapo kwa mdomo huku matendo yetu yakitugeuza watumishi wa Shetani.

Kidumu Chama Cha Mapinduzi.
 
Alieelewa anieleweshe nahitaji sana kuelewa!
 
Back
Top Bottom