Ndoa ya Kikristo ina vigezo gani?

Ndoa ya Kikristo ina vigezo gani?

John Magongwe

Member
Joined
Jan 4, 2024
Posts
71
Reaction score
119
Ndoa ya Kikristo ina Vigezo Gani
Hii ni ndoa inayofungwa katika kanuni timilifu za Mungu alizozikusudia tangu mwanzo
.

Vigezo vinavyohusika vimeainishwa katika sehemu zinazofuata hapo chini.

Wote wawe waumini
(2Wakorintho 6:14-18)
Kuamini si lazima muwe katika viwango sawa kiroho, lakini wote muwe upande mmoja wa Kristo, Lakini mmoja ni mganga wa kienyeji mwingine Mkristo, au mmoja ni Muislamu mwingine mkristo. Hiyo si sawa, ni sharti wote wawe wakristo. Kwa sababu hakuna ushirika wowote kati ya nuru na giza. Vile vile, ni kwa sababu ndoa ya kikristo ni lazima iwe katika jina la Bwana, vinginevyo, itaangukia katika kundi la wasioamini Kristo.

Mume mmoja, mke mmoja
Tofauti na ndoa zisizokuwa za Kikristo, ambazo kwao unaweza kuwa na mke zaidi ya mmoja, lakini mtu anayetaka ndoa yake itimilike mbele za Kristo, basi mume/mke atambue kuwa hana ruhusa ya kuongeza mwenza mwingine.

Mathayo 19:4-5
4 Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, 5 akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?

Malazi yawe safi
Waebrania 13:4
4 Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.
Malazi kuwa safi maana yake ni nidhamu ya kiasi, katika kukutana kimwili. Mkristo hapaswi kuwa mtu wa hulka ambaye wakati wote anawaza zinaa, mpaka anakosa muda wa kujishughulisha na mambo ya rohoni.
1Wakorintho 7:5
5 Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.
Vilevile vitendo kama kuingiliana kinyume na maumbile haviruhusiwi ndani ya ndoa (1Wakorintho 6:9).

Hakuna talaka
Tofauti na ndoa ambazo si za kikristo, ambapo mtu anaweza kuacha/kuachwa kwa sababu yo yote, labda mfano wamechokana, au wameudhiana, lakini katika ukristo hilo jambo halipo. Mtaendelea kuishi pamoja mpaka kifo kitakapowatenganisha.
Bwana alitoa ruhusa hiyo ya kuachana katika eneo la uzinzi tu, lakini ukumbuke, Yesu alisema pia ‘samehe saba mara sabini’. Hivyo kwa kauli hiyo hakuna popote tunaona wigo wa wanandoa kuachana kwa sababu yo yote ile (1Wakorintho 7:39-40)
Mathayo 18:21-22
21 Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? 22 Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini..
Kwa muktadha wa maelekezo ya Yesu, ni wazi kuwa kusameheana saba mara sabini, maana yake ni kuendelea kusameheana, hivyo, hakuna kuachana.

Mume ni sharti ampende mkewe
Mume kumpenda mkewe ni amri ya kindoa
, anawajibu wa kumtunza na kumuhudumia na kujitoa kwa ajili yake, kama Kristo alivyolipenda kanisa (Waefeso 5:25-31).

Mume anapaswa kuchukua uongozi nyumbani
Uongozi huu (Waefeso 5: 23-24) haupaswi kuwa wa kulazimisha, kunyanyasa, au kumkandamiza mke, lakini lazima uwe kwa mujibu wa mfano wa Kristo kuongoza kanisa. Kristo aliipenda kanisa (watu wake) kwa mguso, huruma, msamaha, heshima, na bila ubinafsi. Kwa njia hiyo hiyo, waume wanapaswa kuongoza ndoa zao.

Mke ni sharti amtii mumewe
Ni amri mke amtii mumewe kwa agizo atakaloambiwa au kuelekezwa
. Tofauti na ndoa zingine ambazo hili linaweza lisiwe la muhimu. Kwenye ukristo, ni lazima utii wa mwanamke uonekane kwa mumewe. Waefeso 5:22: Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu.

Wake wanapaswa kujinyenyekeza kwa waume zao
Hii ni "kama kwa Bwana" (Waefeso 5:22), si kwa sababu yeye analazimishwa kuwa mtiifu kwake, lakini kwa sababu mume na mke wanapaswa "kunyenyekea kwa kuheshimu Kristo" (Waefeso 5:21), na kwa sababu kutakuwa na muundo wa mamlaka ndani ya nyumba, pamoja na Kristo kama kichwa (Waefeso 5: 23-24). Heshima ni kipengele muhimu katika haja ya kunyenyekea; Wake lazima waheshimu waume zao kama waume na vile vile wanaume kuwapenda wake zao (Waefeso 5:33).
Upendo wa pamoja, heshima, na unyenyekevu ndizo nguzo za ndoa ya Kikristo. Kujengwa juu ya kanuni hizi tatu, wote wawili mume na mke watakuwa katika ukristo, wakikua pamoja, siyo kando, kama kila mmoja anavyokuwa katika utawa.
Vigezo hivi wakivikidhi hawa wakristo ambao wanatarajia kuishi kama mke na mume, basi hiyo huitwa ndoa ya Kikristo iliyokidhi vigezo vitimilifu vya Mungu, haijalishi imefungwa kanisani au kwenye familia.

Je, ndoa ni lazima ifungiwe kanisani ? Je ni sharti?
Mkristo ambaye anathamini ukamilifu wote wa ki-Mungu, katika maeneo yake yote ya kiroho na kimwili, kufungia ndoa yake kanisani itakuwa ndilo chaguo lake bora. Kwa nini iwe hivyo?

Faida za ndoa kufungiwa kanisani

1. Kanisa ni mahakama ya Wakristo

Biblia inatueleza mashtaka yetu, hayapaswi kutatuliwa na watu wa ulimwengu, bali ndani ya kanisa. Kwa sababu kanisa ni zaidi ya mahakama yo yote, ambayo Mungu ameiheshimu mpaka akaamua malaika zake wahukumiwe katika hiyo.
Hivyo endapo kuna migogoro, au kutoelewana, au kupatiwa misaada, au mashauri, au maonyo, au maongozi, basi kanisa, limewekwa na Mungu kwa ajili yako kukusaidia katika hayo yote.
Lakini ikiwa hukuifungia ndoa yako kanisani, fahamu kuwa kuna mambo kama hayo yatakupita, au huenda yatakuwa magumu kutatulika.
1Wakorintho 6:1-3
1 Je! Mtu wa kwenu akiwa ana daawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki mbele ya wasio haki, wala si mbele ya watakatifu?
2 Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo?
3 Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika, basi si zaidi sana mambo ya maisha haya?

2. Ushuhuda mwema
Mungu anapenda mambo mema atufanyiayo tumtukuze mbele ya kusanyiko la watakatifu. Tunajua ndoa ni kitu chema, hivyo tunapoweka wazi mbele za Bwana, na mbele ya kanisa lake, yeye hutukuzwa, lakini pia tunapokea baraka za kanisa, Ikiwa tunapoumwa na kuponywa hatuoni sawa kukaa na shuhuda zetu ndani, tunakwenda kushuhudia mbele ya kanisa, si zaidi ndoa zetu?, ni ushuhuda mkubwa, ambao utawafariji wengine, lakini pia utaihubiri injili ya Kristo.
Zaburi 35: 18 Nitakushukuru katika kusanyiko kubwa; Nitakusifu kati ya watu wengi.
Kwa Mkristo, kuna utajiri unaohusishwa na ndoa ambao unaweza tu kueleweka kikamilifu, kuthaminiwa, na kufurahia ndani ya muktadha wa Mwili wa Kristo. Kwa kujua Yesu kuwa Bwana-arusi ajaye, tuna jambo la kusherehekea katika ndoa ambayo wasioamini bado hawawezi kuelewa.

Katika hali za kawaida, tungefikiri kwamba wenzi wa ndoa Wakristo wangetaka kuadhimisha ndoa yao mbele za Mungu na watu wake. Ni fursa nzuri kwa mwanamume na mwanamke kukiri imani yao katika Kristo na kutia muhuri kujitolea kwao wenyewe kwa wenyewe mbele ya macho ya ulimwengu unaotazama. Ulimwengu huo ni mbele ya waumini, KANISANI.

Hivyo, tunaweza kusema hakuna sababu ya Mkristo yoyote kufungia ndoa yake, mbali na kanisa.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, haimaanishi kuwa usipofungia kanisani, ndoa yako haitambuliwi na Mungu. Muhimu ni kukidhi vigezo “mama” vilivyoorodheshwa hapo juu, hiyo ni ndoa.
 
Back
Top Bottom