Ndoto ya Tanzania katika Michezo ya Olympic: Mpango wa Miaka mitano.

Damaso

JF-Expert Member
Joined
Jul 18, 2018
Posts
3,978
Reaction score
6,739
Mwaka 1964 ndio ulikuwa mwanzo wa Tanzania kuanza kupeleka wanamichezo kwenye michezo ya Olympic na tumekuwa tukifanya hivyo kila wakati isipokuwa michezo ya Olympic ya mwaka 1976 huku pia tukiwa hatujawahi kushiriki kwenye ile michezo ya Olympic ya Winter.



Katika michezo hii toka mwaka 1964 tumefanikiwa kupata medali mbili pekee medali ya shaba na medali zote zimetokana na wanariadha, Suleiman Nyambui ambaye alipata medali ya shaba kwenye mbio za mita 5000 za wanaume kwenye michezo ya Olympic ya Moscow ya mwaka 1980 pamoja na Filbert Bayi ambaye alipata medali pia ya shaba kwenye mbio za mita 3000.


Mwaka huu pia tulipata kupeleka wanamichezo katika michezo ya Olympic iliyoanza Julai 26 na kutamatika Agosti 11, kwa nafasi ya kipekee sana Tanzania tulikuwa na wanamichezo katika michezo mitatu, mbio (marathon), judo pamoja na kuogelea, jumla ya watanzania saba walikwenda kujaribu bahati yao ya kuongeza medali, wanawake walikuwa watatu huku wananume wakiwa ni wanne.



Upande wa wafukuza upepo tulikuwa na Gabriel Geay pamoja na Alphonce Simbu kwa wanaume huku tukiwa na Jackline Sakilu pamoja na Magdalena Shauri kwa upande wa wanawake.



Katika mchezo wa Judo, kwa mara ya kwanza tokea mwaka 2016 Tanzania tulifuzu kumpelekea judoka kwenye michezo ya Olympic, Andrew Thomas Mlugu katika uzani wa kilogramu 73. Pia ikawa ni mara ya kwanza tokea 2016 Tanzania tukapeleka waogeleaji wawili, Collins Saliboko kwa upande wa wanaume huku upande wa wanawake akiwa ni Sophia Latiff. Kiukweli hawa wanamichezo wamejitahidi sana kufika hapo ingawa hatukupata medali yoyote ila wameonesha uzalendo mkubwa sana.



Ili Tanzania ipate kuonesha jambo kubwa ndani ya michezo ya Olympic basi inahitaji maandalizi makubwa sana, maandalizi ambayo sio ya kuanza mwaka mmoja kabla ya kwenda kwenye michezo ya Olympic, Los Angeles ndo watakuwa wenyeji wa michezo ya Olympic ya mwaka 2028 kuanzia Julai 14 mpaka Julai 30, sasa haitokuwa kitu kizuri kama tukianza kujiandaa Oktoba mwaka 2027 ili kuandaa watu wa kwenda Los Angeles.



Haya ni baadhi ya maoni yangu kama mdau wa maendeleo na mpenda michezo ndani ya Tanzania. Kabla sijaendelea kabsa, ningependa kuweka wazi kuwa michezo ya Los Angeles sisi kama Tanzania tusiende tujiandae na michezo ya Olympic ya Brisbane ya mwaka 2032.

Maoni yangu yanaweza kuwa tofauti na wengi ila nimejaribu kuonesha mikakati baadhi ambayo tunaweza kuifanya kujenga wanamichezo bora watakaoenda kuonesha changamoto na sio kubeba tu bendera ya Tanzania. Katika andiko hili utakutana na mipango kama vile, tamthini ya kina kuhusu michezo ambayo Tanzania ina uwezekano mkubwa wa kupata medali, ukiachana na hilo kuna kuanzishwa kwa programu za maendeleo ya michezo mahususi kwa ajili wa Olympic pekee, pamoja na kuanzishwa kwa prograu za utambuzi wa vipaji ambayo vinaonesha uimara.



Kufanya tamthini ya Michezo ambayo tunaweza kuleta ushindani.

Hatua ya kwanza ambayo kamati ya Olympic Tanzania inapaswa kuwa makini ni utambuzi wa michezo ipi sisi kama Tanzania tunaweza kupambania medali, sio kila mchezo tunaweza, hio tukubali au tukatae ila ndo ukweli. Wizara ya Michezo kupitia wataalamu wawe na andiko maalumu linaloonesha kuwa Tanzania ina uwezo kwenye michezo fulani bin fulani.



Kumpeleka Collins Saliboko kushindana na Kina Pan Zhanle kutoka Uchina, au Kyle Chalmers kutoka Australia ni unafiki mkubwa sana, ingawa tumsaidia kuona jukwaa lilivyo ila ni sawa na kwenda kutalii tu pale Paris. Bwana Mkubwa Andrew Thomas Mlugu alimchapa vibaya sana William Tai Tin kutoka Samoa ila alipokutana na jitu Joan-Benjamin Gaba, mtoto wa 2001, Andrew alipigwa kwa alama 10 kwa sifuri.

Michezo ambayo kwa Tanzania tunaweza kwenda kuonesha umwamba ni hii:

Kubeba chuma! Nadhani umepata kukutana na utingo wenye kubeba magunia ya mahindi kilogramu 200 hawa wanaweza kutuletea medali kutoka mikononi mwa watu kama vile Meza Domingo Francisco, pamoja na watu kama Jordan Elkin. Nina imani tukipata utingo kama kumi tukawaweka kambi kisha tukawapeleka wakashtue majukwaa kama vile IWF Elite World Championships, Africa Championships, IWF Grand Prix na kadhalika. Tanzania tunaweza kupata medali kwenye kunyanyua vyuma.



Kupiga kasia na kuendesha mitumbwi, hivi kweli tumeshindwa kuchukua wavuvi kadhaa kutoka Ziwa Victoria pamoja na Bahari ya Hindi na kuwafua ili waende kutuwakilisha kimataifa. Kama Msukuma mmoja anaweza kupiga kasia akiwa ziwani kutoka Sengerema mpaka Igombe kwenda na kurudi, je tunashindwa kumuongezea nguvu kwenda kwenye mashindano ya kimataifa.



Kuna wakati kulikuwa na mashindano ya kupiga kasia yakidhaminiwa na kampuni inayotengeneza pombe aina ya Balimi na Safari Lager, ukiwatazama washiriki unaweza kuona kabsa hii ni almasi tuliyoilalia kwenye mto.

Kuendesha baiskeli, huu ni mchezo ambao kiukweli tungesema tuwape nguvu watanzania basi kuna medali kibao zitakuja. Chukua picha mashindano ya kuendesha baiskeli kutoka Shinyanga uwanja wa CCM Kambarage mpaka Mwanza kwenye uwanja wa CCM Kirumba, yaani watu wanaingia uwanjani kumaliza mbio hizo kuna wengine ndo kwanza wapo Buhongwa.



Baiskeli maarufu kama Mkulima, baiskeli ambayo mnyororo wake umekazwa kweli kweli, watu watatembeza padel kama wana ugomvi. Kuna watu tokea wana miaka 8 wanaendesha baiskeli mpaka sasa wana miaka 30 hawa ndo wanamichezo wa kupeleka Olympic pamoja na Tour de France, Giro d’Italia pamoja na Vuelta a Espana, tena waende na basikeli zao hizo hizo marufu kama Mkulima.



Kupima na kulenga shaba, maarufu kama Archery katika michezo ya Paris kulikuwa na kivutio kikubwa cha Mwamba mmoja kutoka Uturuki, Yusuf Dikec ambaye hakuwa na muda wa kuvaa vifaa vya kumsaidia kulenga shaba, alichohitaji ni miwani yake na alilenga shaba akiwa na mkono mmoja mfukoni bila taabu yoyote.

Nina imani kwa Tanzania kuna ndugu zetu wamaasai ambao hawa ni balaa kwenye kulenga shaba, Olaiboni anafahamu kupima shaba pasipo kuhitaji vifaa vyovyote, tunaweza kutafuta watu wenye kujua kulenga shaba, hata katika vikosi vyetu vya usalama tupate watu watakaoingia darasani kujifua kwa ajili ya Olympic ya Brisbane 2032.

View attachment 3105914

Mbali na hivyo pia sisi kama Tanzania tunaweza kuanzisha vituo maalumu vya kufanyia mazoezi, mfano, kwa wale wanamichezo wa ngumi, pamoja na mbio wapate kuwa na vituo kwenye maeneo ya baridi kama vile Mbeya, Njombe, Kilimanjaro huku wale wanamichezo wanaojifua kwa ajili ya kupiga mbizi wapate nafasi ya kuwa karibu na maziwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Sisi kama Tanzania tusiwe na haraka ya kupeleka timu ili mradi tuonane tupo kwenye michezo hiyo bali twende kuonesha ubora wetu tusiwe wasindikizaji bali tupeleke ushindani. Kamati ya Olympic isione kama jukumu ni la kwao pekee bali ni jukumu letu sote kama taifa. Tukifanyia kazi haya maoni pamoja na mengine basi tutaona matunda ya watanzania katika ramani ya dunia.
SIO KWA UBAYA!​
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…