Ndugu Masoud Abdullah Salim

Ndugu Masoud Abdullah Salim

Abdull Kazi

JF-Expert Member
Joined
Dec 29, 2012
Posts
337
Reaction score
296
Huwezi kuzungumza siasa za Pemba bila kumtaja Masoud Abdulla Salim, mwamba katika uwanja huo kwa miaka kadhaa na mwanasiasa jabari na nguli.

Aliingia kwenye siasa mara baada ya mfumo wa vyama vingi kuanzishwa akitokea Jeshi la Polisi, alikokuwa akifanya kazi kwa miaka kadhaa jambo lililofanya upinzani ufaidike sana na ujuzi na uelewa wake kuhusu vyombo vya dola.

Masoud alitumikia jimbo la Mtambile kwa miaka 20 mfululizo akiwa Mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuanzia jijini Dar es Salaam hadi Dodoma.

Wengi tukimwita Masoud wa Mtambile jinsi alivyowawakilisha na kuwa alama yao na muda wote alikuwa mwanachama mtiifu wa Civic United Front.

Masoud alikuwa na ushawishi mkubwa kwa hivyo mbali ya Ubunge alikuwa Mjumbe wa ngazi za juu kwa kipindi chote cha uongozi, na kutakiwa mara kadhaa kutoa ushauri.

Bungeni Masoud sio tu alikuwa mzoefu lakini alikuwa ni mwenye uelewa mkubwa wa taratibu zote za Bunge na hasa Kanuni.

Alikuwa akivijua vifungu vyote vya matumizi vya Serikali nzima na kuvitaja kwa uelewa na weledi mkubwa sana.

Bungeni alikuwa ni KAMUSI kama sio 'Encyclopedia' kwa kichwa kilicho jaa taarifa za miaka kadhaa ambazo ikiwashwa switch tu zinamwagika kama maji ya Mto Nile.

Bungeni Masoud alijulikana kwa uzoefu wake kushika vifungu na kukamata shillingi si kwa sekta ya ulinzi aliyoitumikia miaka yote bali pia sekta na Wizara nyengine.

Ikumbukwe pia ni mmoja wa Wabunge wachache ambao pika pakua kwa umri wake wote ndani ya Bunge alikuwa katika Kamati ya Mambo ya Nje na Ulinzi.

Kwenye Kamati hiyo alipigana vikumbo na wakuu wote wa vyombo vya usalama na tuliokuwa au Ilipotokea ishu eneo hilo, kama watu wetu kukamatwa Zanzibar, simu yake moja au uso kwa uso kwa wakuu wa vyombo ilisaidia.

Nilimkuta Bungeni 2015-2020 na nikafanya nae kazi kwa karibu sana nikivuna faida za uzoefu wake.

Wabunge wenzangu walinichagua kwa kura kuwa mnadhimu wa Kambi ya CUF bungeni Ila moyoni nilijua Masoud ndie aliestahiki.

Uzoefu wake iliokuwa wa kunifunika kwa sana haukufanywa awe na chuki kwangu Ila alisaidia kuniongoza na kunipa uzoefu.

Masoud alikuwa mtu wa utani ule wa kuchomekea na saa zote ni mtu wa kucheka. Lakini pia alikuwa mkimya na rafiki kwa wote.

Tulikuwa nae Masoud Bega kwa Bega katika harakati za kubaki Bungeni baada ya CUF kuparaganyika na ni kapewa zigo la kufungua kesi Mahkama Kuu kupinga CUF wakati pia tukiendelea kuwa Wabunge wa Chama hicho.

Bila ya shaka kilikuwa ni kipindi kigumu mno ambapo kwa zaidi ya miaka mitatu tulikuwa tumekalia kutu kavu. Hio ilikuwa ni sababu kuu Wabunge sisi wengi wetu wasiweze kufanya vyema majimboni.

Vikao vyetu vingi tukifanya nyumbani kwa Mhe Yussuf Salim na Marehemu Khatib Said na pia kwa Marehemu Masoud.

Hata kikao na Zitto Kabwe hata kabla ya kuhamia ACT WAZALENDO sisi tukiwa bado ni CUF tulifanyia nyumbani kwa Marehemu Masoud.

Pamoja na Marehemu Masoud tukiichangia ACT WAZALENDO tukiwa hata si wanachama na tukahajiri nae mara baada ya kumalizika kwa Bunge 2020.

Kiongozi wa Chama Zitto Kabwe amekutana na Masoud huko Bungeni sio tu 2020 bali hata kabla ya hapo, aliamua kuteua kuwa Msemaji wa Kisekta wa Ulinzi, alisaidiwa na Nd. Said Bakame, lakini Masoud hakuwahi kuitumikia nafasi hiyo kwa sababu ya ugonjwa.

Kifo ni fardhi tusoweza kuiepuka, na tumepokea fardhi hio, Ila tumepoteza mwanasiasa wa kiwango cha juu, mweledi wa siasa za Zanzibar, kinara wa siasa za Tanzania na kamusi hai.

Jengine Masoud alikuwa mpenzi mkubwa wa mpira na hakukosa kila siku ya Mungu... Na wajue watakao jua kuwa timu yake ilikuwa ni Simba Sports Club.

Nasita hapo kuandika hii taazia si kwa kuwa nimechoka au wino umekwisha bali kuna mengi ya wema, ihsani na msaada kama binaadamu ikiwa ndio sifa yake kubwa

Ally Saleh Alberto
IMG-20220725-WA0195.jpg
IMG-20220725-WA0174.jpg
 
Back
Top Bottom