NECTA: HIVI NDIVYO KUDUMISHA MUUNGANO?
Na: Malik Nabwa
Katika mambo ambayo yanauma sana na kuumiza matumbo ni pale mtu au kikundi cha watu chenye kufanya mabaya, kinapojitakasa kwa kutumia lugha nzuri kuhalalisha maovu wayafanyayo. Kwa mfano, kuna watu huweza jiita mujahidina ili kutoa picha nzuri kwa jamii kubwa ya Waislamu ili pia na vitendo vyao viungwe mkono kwa kuamini wao ni wana jihadi, lakini ukivipima hivyo vitendo vyenyewe havimo katika uislamu kabisa
Kuna watu hujiita watetezi wa haki za binaadamu lakini kiudhati wao huwa ndio wavunjaji wakubwa wa haki hizo. Na wako pia wanaojiita watetezi wa wanyonge lakini ikawa hiyo ni njia yao au kibali chao cha kupata kuwanyonyoa vizuri hao wanyonge inaojitia kuwatetea.
Natamaka haya kwamba hapa kwetu tumepata kijisababu kiitwacho Muungano. Imekuwa jambo kunuka kiambo. Kila Mzanzibari anavyojaribu kujitetea na kudai haki zake basi hubambikizwa neno la ‘mvunja muungano'. Wakati tukijuwa wazi kuwa muungano ni mashaka na zigo la mazagazaga ya taka iliyokolea vundo kwa Mzanzibari, Viongozi wetu wa bara na Wa hapa Zanzibar wakija kwetu, hutuimbia wimbo huu wa ''kudumisha Muungano''. Ninavyojua mimi muungano madhubuti hujengwa kwa misingi halali iliyosimamiwa kisheria ikiwa ni pamoja na kutendeana haki pande zote zilizoungana bila ya kuwepo hujuma au kinyume , mtima nyongo, au machapa kungu Fulani hivi.
Nijuavyo Muungano ni kupendana kwa dhati na kutakiana mema kila uchao. Muungano ni kudumisha amani na utulivu wa kweli na sio wa katika bomba tu. Muungano ni kuunga nguvu isiyo chembe ya unafiki, wala Uazandiki ndani yake. Muungano ni kujitakasa na unafiki, na unyonyaji au Ukandamizaji wa aina zote kati ya pande zinazoshirikiana. Muungano ni kuungana nguvu, na kushikana mikono pale mmoja anapokwama akakwamuliwa. Hivi tujiulize huu muungano wetu una maana hii? Una sifa hizi?
Mfano mdogo tuzungushie shingo Baraza la mitihani la taifa (NECTA).Tangu miaka ya 1970 na baada ya kuundwa kwa baraza la mitihani la Bara na sio la Tanzania, Wazanzibari tumekuwa wahanga wakubwa wa baraza hili hasa pale inapokuja mitihani ya masomo inayosimamiwa na wao wenyewe chini ya baraza kandamizi pendelezi liitwalo NECTA.
Kuna wakati kabla ya Marehemu Kigoma Malima baraza hili likuwa na njama dhidi ya wanafunzi wenye asili ya kiislamu. Ikawa ukiwa na uislamu tu hupiti kwa njia yoyote ile. Unaletewa ‘C' ya dini, na kiarabu, tena hapo uwe ni hodari wa kutafutiwa watu. Mungu akampa maarifa kabla hajahujumiwa Bwana Malima akabadilisha mfumo akaleta nambari za mitihani bila majina. Tukawa tunapata asilimia kumi kuendelea usoni. Ndio akina sisi wawili watatu.
Lakini kila uchao, muelekeo wa sasa ni wazi kuwa Baraza la mitihani linaendesha hujuma za chini kwa chini dhidi ya Waislamu na hasa sasa wazanzibari. Mimi siwezi amini hata siku moja kama watu wote katika darasa moja huwa na ufahamu wa aiana moja au unaolingana kwa karibu mno kwa wote darasa zima.
Hakuna utafiti uliowahi kuthibitisha hili kuwa watu 40 Darasani waliochaguliwa tu hivi (randomly) kisha wakawa na uwezo wa aina moja kwani watalamu husema Individual differences are Inevitable''. Lakini hili bara wanalikataa kabisa kupitia NECTA. Kuna shule huko darasa zima lina Div 1, na nyengine Division 1-2, hakuna 3 Darasa zima. Kila mwaka huwa hivi. Maajabu ya nani haya, maana si ya Musa wala Firauni.
Sasa kwa sisi ambao hatuujui ualimu hata kidogo hatuwezi fahamu kitaalamu lakini kwa akili hii ya kichwa mchungwa hili haiyumkiniki hata kidogo. Lakini kwa baraza la mitihani hii ni hali ya kawaida katika dunia yao. Ukweli ni kwamba bara kuna Skuli haizijawahipo kukosa hizo Div 1 na 2 kwa kila mwaka na kila mwanafunzi utamkuta kapata alama hizo.
Huku Zanzibar Division One huwa lulu au kipusa (Pearl in the Crown). NECTA kwa maana yao inajaribu kutushawishi kila hali tukubali kuwa Zanzibar hawana uwezo wa kusoma na kwa maana hiyo Muungano ni msaada mkubwa kwetu kutufikisha anaglau hapao padogo tulipo. Na ndio ukaona hata Viongozi wanatuchagulia wengi huwa ni wale waliowakataa wao NECTA kwani wakiwaeka wenye maarifa makubwa watahoji kama alivyofanya Bwana Kigoma Malima.
Ukiuliza sababu za kufeli sana huku siku hizi utatajiwa nyingi sana. Hakuna walimu wazuri, moja bara bila shaka walimu wao hutoka angani. Mbili, hakuna vifaa vya kutosha, mbili, bara hutengeneza vyao. Walimu hawalipwi vizuri, tatu, sawa lakini khaah! Hata hili?. Wazanzibari hawataki kusoma ni wanyeye (Bogus), nne, ni kiasi tuitwe hivi maana mtu kukubali changanya ng'ombe mmoja na mmasai alien a Ng'ombe milioni arubaini si ubwege mdogo huo, lakini sidhani kama unaathiri matokeo nchi nzima, pengine labda!. Na sababu nyengine mutajazia nyie wenyewe. Maneno haya ndio yanayosemwa na kufanywa kuwa hoja kuu huko NECTA na kwa wenzetu wa bara kuhusu kuanguka kwetu katika matokeo ya mitihani ya taifa..
Lakini mimi kwa maarifa yangu kumvikumvi, na mawazo manayaufunyaufu ni kuwa haiwezekani kabisa kuwa wanafunzi 40 wote wakawa wana daraja moja ya uwezo au inayolingana kiasi ya kuwa siku zote ni Divisheni 1-2 basi tena kwa kila somo. Dhana hii potevu inapingana kabisa na tafiti kongwe za kisaikolojia ya Elimu zinazoamini kuwepo kwa ''ndividual differences'' madarasani na hata ''exceptionality'' humo madarasani. Sasa tukisema kuwa NECTA imegawa maeneo yake itakavyo na kuyafanya yote yawe ya kiwango sawa (Homeogeniouos) ili kuyata kafara kutimiza azma yao ya kisiasa hilo halina mushkeli, tusidanganyane.
Kwa mafano anuai angalia matokeo, Maeneo ya pwani yote ya Tanzania na Zanzibar yake hao ni watu wa kupata C za kuchaguwa, D rundo kwa rundo na waliobaki wote F tupu hata wakiwa vipi. Wakijua wazi mgao huu uatawapitisha Wazanzibari chini ya asilimia 20% kuendelea na masomo ya juu. Huku kwao wakitoa alama za juu kwa shule zao za Seminari na nyenginezo katika malengo yao ya milenia, darasa zima hupewa alama A tupu na waliobakia B na wasio na bahati kidogo huishia C lakini kwa ufupi hafeli mtu huko si kama huku kwetu.
Nionavyo, pamoja na sababu zote wanazozitoa kuhusu Zanzibar kuhalalisha kufanya kwetu vibaya takribani mara zote katika mitihani ya taifa, kuna hujuma na ukorofi dhidi yetu huko katika baraza la mitihani. Na ningekuwa bungeni au uwakilishini hivi sasa (Siwezi kuwa tena kwa sasa maskini) basi ningeomba iundwe tume ya kuchunguza uhalali wa matokeo baraza la mitihani la Taifa (NECTA). Kwa hili nisingekuwa na wasiwasi maana ukweli haufichiki.Tungewakamata tu maana Dr. Malima alipitia nia hii hii na hakuchukua muda aliwatia nguvuni.
Haiwezekani hata siku moja watu wa nchi Fulani wawe ni mazuzu karibu wote na wa nchi nyengine jirani wawe mahodari wote hata kama wangeumbwa na kuzaliwa tumbo moja.Vyovyote iwavyo, nasema NECTA kuna hujuma tena ya muda mrefu na sasa kama ni jipu lishawiva tulipasuwe tulitowe moyo tuuguze kidonda siku mbili ya tatu tubakishe kovu. Bila hivyo hawa watatumaliza maana wanajua wazi kutufanyia hivyo ni kunedeleza kuudumisha huo Muungano kwani tutakuwa hatuna sauti ya kuhoji na kudai haki zetu.
Muda si muda hivi, MATOKEO yameshatoka na Shule ya Biashara Mombasa ni ya pili kwa Zanzibar huku Lumumba ikiongoza na katika gredi ya taifa ni 93 nchi nzima. Hodari wetu hao wako katika nafasi hiyo. Hii ni taswira ya kututawla kisaikoljia na kutufanya tujione matobwe mbele yao siku zote. Hata ukiangalia vipindi vyao vya vituko basi dhihaka (Stereotypes) zao zote ni za kejeli tu dhidi yetu kutuona nyungunyungu au konokono asie gamba (Escargot). Ndio ukasikia mara ‘mdebwedo', ‘ami', ‘akhee', yote hii ni dhihaka ya kutuona sisi wazulufu na wabole na sio utani kama tunavyodhani.
Mpendwa msomaji na mzalendo, nikiwa naandika makala hii niko na jazba kidogo (emotional) kumradhi, lakini kwa yoyote anaetaka kujaribu kuchunguza uukweli huu, basi na iundwe tume huru kuichunguza NECTA kisha itupe majibu. Hilo moja. Pili, Zanzibar na ijitoe iingie katika mitihani ya Cambridge ambayo itatungwa na kusahishwa hukohuko Maksifodi na makambriji na huku bara nao wakifanya mitihani yao na hiyo ya Cambridge tuone. Naamini hawatapasi wanafunzi wote huku Zanzibar lakini haitakuwa dhulma kama hivi ilivyo sasa chini ya NECTA. Tuamke, tutanabahi, tufikiri namna ya kujivua na baraza hili. Bila hivyo tutakuwa vilaza wa Elimu wa Kimataifa muda si mrefu kwa sababu hiyo ndio taswira wanayoijenga NECTA mbele ya dunia.
‘Mbuyu zishakaangwa wenye meno tafuneni!'
Wakatabahu.
Nabwa!