Mama anaisuka Tanzania mpya, lakini hataki sindano iwaume sana wale "chawa" wa mwendazake, hivyo anachoma halafu anawapuliza kwa kuwaambia kuwa yeye na mwendazake ni kitu kimoja.
Wakishangilia anaongeza sindano nyingine. Wakishtuka anawaambia mwendo ni uleule alioacha mwendazake. Wanabwatuka tena kushangilia, anaongeza sindano nyingine. Yani mama ana akili sana.
#Mosi; Ameahidi kuimarisha uhusiano wa kimataifa na kufungua balozi mpya. Uhusiano wetu kimataifa uliforora kwa miaka 6 ya mwendazake. Tulifeli ktk diplomasia. Yeyote aliyekua na mawazo tofauti tulimuita beberu. Hatukutaka kuchangamana na dunia. Hata vikao vikubwa kama WEF au UN hatukutaka kushiriki. Tulikosa exposure ambazo zingetusaidia kupiga hatua.
Mama kasema hakuna tena "blahblah" za mabeberu. Tutashirikiana na wengine kwa maslahi ya nchi yetu. Dunia inasogea sisi hatuwezi kubaki nyuma. Tutashirikiana na dunia lakini kwa kulinda maslahi yetu, bila kukubali masharti yatakayoharibu utu wetu. Yeyote anayetaka kushirikiana na sisi aheshimu mila na desturi zetu.
Hiki ni kitu ambacho tumeshauri mwendazake kwa muda mrefu lakini hakutaka kusikia. Leo mama amefanya yaleyale ambayo tuliyoshauri, lakini ili kuwapooza "chawa" akasema yeye na mwendazake ni kitu kimoja. Wakashangilia.
#Pili; Mama ameahidi kukuza demokrasia na utawala wa sheria. Ili kuonesha anamaanisha AMEOMBA WATANZANIA WAIKOSOE SERIKALI. Hili ni jambo kubwa sana. Yani Rais wa nchi anawaomba mkosoe serikali. Haijawahi tokea. Mama kaweka rekodi. Mwendazake hajawahi kukubali kukosolewa, achilia mbali kuomba wananchi wamkosoe. Hiyo kwake ilikua "future imposible tense"
Ukosoaji ulikua ni dhambi kubwa hata kama unakosoa kwa nia njema. Muulize mdogo wangu Kumbusho Dawson alipokosoa "expansion joints" nini kilimtokea? Kuna watu wamefungwa, wamepigwa, na kufanyiwa vitendo vya kikatili kwa sababu tu ya kukosoa serikali.
Leo Mama kasema kukosoa ruksa, kuonesha anapenda mawazo mbadala. Wakosoaji tumepewa ruksa ya kujiachia ili mradi tusivunje sheria za nchi. Tukosoe kwa misingi ya kujenga (constructive critisism). Hii ni sindano kali kwa "chawa" lakini ili kuwapooza akawaambia yeye na mwendazake ni kitu kimoja. Wakashangilia.
#Tatu; Mama kaonesha nia ya maridhiano kwa kukubali ombi la viongozi wa upinzani kukutana nae. Hi ni habari njema kwa sababu nchi hii ni yetu sote na inahitaji mawazo ya kila upande ili kupiga hatua. Wakati wa mwendazake kuna watu walijimilikisha nchi. Wakaona wengine ni wapangaji.
Mama kasema atakutana na viongozi wa upinzani, ili tusonge mbele tukiwa wamoja. Nachowashauri kwenye meza ya maridhiano wasisahau Katiba mpya. Mchakato uendelee kwenye rasimu ya Warioba. Akifanya hivyo ataacha legacy kubwa kwa taifa hili.
Mwendazake hakutaka maridhiano kabisa na hata viongozi wa upinzani walipomuomba kukutana nae aliwapuuza. Chawa wakatukana upinzani eti mlizoea kuitwa Ikulu kwenda kunywa juice wakati wa JK lakini JPM hana muda huo, yuko busy kujenga SGR. Mama kasema SGR itajengwa na Ikulu tutaitwa. Na safari hii hatutakunywa juice tu, hadi futari tutakula. Na tukitoka tutawaambia mama na mwendazake ni kitu kimoja ili mpige nduru [emoji1787].
#Nne; Mama amevihakikishia vyombo vya habari uhuru. Mambo ya waandishi kukamatwa, kupigwa, kutekwa, yamefika mwisho. Vyombo vipo huru kuripoti habari yoyote yenye maslahi kwa taifa ili mradi vinafuata sheria za nchi. Mwendazake alizika kabisa uhuru wa vyombo vya habari, lakini mama kafungua huo mnyororo rasmi kuanzia leo.
#Tano; Mama ameahidi kuboresha maslahi ya watumishi kwa kupandisha vyeo na mishahara. Huu ni mfupa uliomshinda mwendazake. Kwa zaidi ya miaka 6 watumishi hawakupandishwa madaraja wala kuongezewa mshahara. Kila walipolalamika walijibiwa kwa kejeli.
RC mmoja akasema eti angewachapa viboko. Unamchapaje viboko mtu anayedai haki yake? Nyongeza ya mshahara sio huruma ya kiongozi ni matakwa ya kisheria. Lakini watumishi wamedhulumiwa haki hiyo kwa miaka 6 bila huruma. Sasa mama amesema imetosha. Ameamua kuwafuta machozi.
Pia ameahidi ajira mpya ambapo 6,000 ni za walimu. Hapa ningependa nimshauri kidogo. Kwanini serikali inataka kuajiri walimu 6,000 wakati mahitaji ni 40,000? Idadi ya walimu waliohitimu tangu mwaka 2015 hadi sasa ni 45,000, na deficit ya walimu ni 40,000. Sasa kwanini ajira 6,000? Si waajiriwe tu wote?
#Sita; Kuhusu uwezeshaji kwa vijana amesisitiza halmashauri ziendelee kutenga 10% ya bajeti yake kwa ajili ya mikopo kwa vijana na wenye ulemavu. Hapa kunahitaji ufuatiliaji. Halmashauri ngapi hufanya hivyo? Mwaka wa fedha 2019/20 halmashauri ya Manispaa ya Temeke ilipitisha bajeti ya Bilioni 48, ambapo Bilioni 4.8 zilipaswa kutengwa kwa ajili ya vijana. Lakini kiasi kilichotengwa hakikufika hata 200M.
#Saba; Kuhusu ATCL mama amekubali shirika linajiendeaha kwa hasara, sawa na ripoti ya CAG inavyosema. Hii ina maana zile story za mwendazake kwamba ATCL inapata faida hadi inatoa gawio serikalini zilikua drama tu. Mama ameahidi kuiongezea ATCL mtaji, na kuifutia baadhi ya madeni ili ijiendeshe kwa tija. Hii ndio sifa ya kiongozi bora. Unakubali mapungufu kisha unaweka mipango ya kusolve mapungufu hayo. Sio unatupiga sound kwamba shirika linatoa gawio wakati lipo hoi bin taabani.
#Nane; Mama amezungumzia kifo cha Magufuli. Amesisitiza tena kwamba kilitokana na tatizo la moyo na si vinginevyo. Amesema kuna watu wanaotoa taarifa za uchonganishi mitandaoni kuhusu kifo hicho. Amewataka waache uchonganishi huo au wapeleke uahahidi polisi.
Wachonganishi hao wamejirekodi sauti na kusambaza kwenye mitandao wakitunga porojo. Bila shaka watu hao ni wale waliomtumaini JPM kwa moyo na akili zao zote na kudhani hawezi kufa. Wakasahau kwamba nae ni mwanadamu kama sisi.
Kwa sasa wapo kwenye "denial" na ndio wanahaha kutunga story za kuchonganisha viongozi. Mama amewaomba waache. Kumbukeni ombi la mama ni amri. Kama hamtaki kusikia msije kujilaumu. Achaneni na hizo drama. Ukurasa wa JPM umeshafungwa na sasa ni zamu ya Samia. Tumpe nafasi.!