Tuachane na kuponda kila kitu wakati huko nyuma tulikuwa tunalalamika kutokana na kuzidi kuangamia kwa shirika la ndege la Tanzania, huo sio ukomavu. Karibu mataifa mengi duniani yana shirika la ndege moja la kuaminika au zadi ya shirika moja. Hii ni kutokana na kwamba viwanja vikuu vya ndege humilikiwa na serikali, na hivyo kuwepo na shirika linalofanya viwanja vya ndege kuwa na uhai zaidi na papo kuliingizia taifa pesa badala ya kutegemea mashirika ya ndege ya nje ya nchi ambayo yapora pesa za nje kwa kuzitakatisha kihalali kutokana na mfumo wetu wa kuliyumbisha shirika la Ndege Tanzania ambalo siku za nyuma lilikuwa linakua kwa kasi ya ajabu hasa katika awamu ya kwanza.
Huduma bora na wahudumu makini ni njia mojawapo ya kuwa kivutio katika usafiri wa anga. Kwa nafasi kadhaa nilizosafiri nimeshuhudia mashirika mengi ya ndege za Ulaya hupenda kuwaweka wahudumu vijana zaidi kama kivutio kwa wateja, lakini tatizo utaona wasichana warembo hao wako kama urimbo kusahau wateja wengine na kuyumbia zaidi kwa wanaowakenulia meno yao na kuonyesha kuvutiwa na uwepo wao.
Mashirika ya ndege ya Marekani wahudumu wa ndani ya ndege ni matured ambao unaona wako makini sana na kazi yao, na hawana kitu kingine cha kuhangaika na mvuto wa mteja (abiria) fulani, ila utendaji wao, wajibu wao unaowafanya wawepo katika kazi hiyo. Zote ni mbinu nzuri ila kwa njia mbalimbali, nani ameweza zaidi katika hao wanaosafiri kwa ndege mara nyingi wanalo jibu.
Mashirika mengi ya Ulaya pombe ndani ya ndege ni mtindo mmoja, kuna wanaomaliza safari na kuteremka uwanjwa wa ndege wakiwa under influence, tofauti na ndege za Marekani marufuku pombe ndani ya ndege au ndege za uarabuni marufuku alcohol ndani ya ndege.
Kukodi ndege kwa mashirika mengi ni jambo la kawaida kutokana na gharama kubwa ya kununua ndege mpya, na pengine ndege mpya kuchukua muda mrefu kuipata kutokana na kwamba makampuni ambayo yana - assemble ndege si kwa mtindo wa magari kuwepo kwenye parking lot kusubiri wateja, bali ni kwa order tu ya wateja, na hivyo kuchukua muda kukamilika na wakati huduma inahitajika. Kuna mashirika mengi ya ndege ambayo huenda yamepoteza baadhi ya route zao na hivyo ndege zao kuwekwa kwenye list kubwa ya waiting, ni bora kukokdisha na ni nafasi nzuri kwa mashirika ambayo yanahitaji ndege za papo kwa papo kukodi ndege zao. Kwa nafasi shirika linapojaribu kusetirika kwa kutumia ndege za kukodi watakuwa na mkakati wa kuagiza ndege zao mpya.
Pamoja na uwepo wa baadhi ya mashirika Tanzania yanayohudumia usafiri wa anga, huduma yao huwezi kuilinganisha na shirika letu la ndege la Tanzania ambalo ndilo linaloweza kubeba jukumu kubwa kwa huduma na ufanisi. Mashirika binafsi yapo kwa masilahi binafsi na mashirika ya umma yapo kwa manufaa ya umma. Ndio maana mashirika mengi makubwa ya ndege ni yale yenye share kubwa na serikali za nchi na hupata unafuu kutokana na punguzo ya gharama za uegeshaji kutokana na kuwa na share hali kadhalika kivuli cha mkono wa chombo cha umma. Tusishanga mashirika binafsi kuwa na nauli kubwa tofauti na shirika la umma.
Ukisafiri nchi mbalimbali duniani utakuta kila nchi na kila kiwanja cha kimataifa kuhodhiwa na shirika la ndege la nchi kuwa kama kiwanja cha nyumbani. Hivyo nasi hatuna budi kuwa na mtazamo huo kwa vile tunao uwanja ambao hautufaidii moja kwa moja wananchi kama hatuna shirika la ndege la kitaifa. Tuwe na mtazamo wa kitafia na manufaa ya umma na taifa badala ya kuwa na mwono wa kuona tu mradi tuna ndege ziwe za shirika la umma au binafsi. Tusiwe wakandiaji tu wa kila kitu, pale wanapoonyesha dalili ya kuanza na kujipanga upya tuwatie moyo hiyo inaweza kuwa hamasa ya kujituma kufanya vizuri zaidi.
Mwezi mmoja uliopita pale Mtaa wa Samora nilikuwa natafuta ofisi ya Swiss Air, nikaamua kwenda pale ATC House nikijua wanajua iliko watanielekeza. Nilipofika pale ATC House iliniuma sana kuona jengo kubwa ambalo enzi hizo lilikuwa fahari ya shirika letu leo limebaki tupu, kwa wakati huo niliona wahudumu wawili pale ofisini na security officer, wakati enzi hizo ukifika pale palikuwa na uhai. Nawashukuru waninisaidia kunielekeza ilipo ofisi ya Swiss Air.