KLHN International
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Shamsa Mwangunga amekuwa Waziri mwingine wa serikali ya Rais Kikwete kuomba radhi Bungeni kufuatia kile ambacho kimeelezewa kuwa ni kudharau Bunge kwa kuchukua maamuzi ambayo hayakuzingatia hoja ambayo iko mbele ya Bunge. Mhe. Mwangunga ameliangukia Bunge leo hii baada ya Mbunge wa Kwera Mhe. Chrisant Mzindaka kuona kuwa Waziri huyo amedharau hoja yake ambayo ilikuwa inasubiriwa kutolewa maamuzi Bungeni kuhusu suala la vitalu vya uwindaji.
Mwaka jana Bw. Mzindakaya alitoa hoja Bungeni ili serikali isitishe kutoa leseni kwa wawindaji wa nje ambao muda wao unamalizika mwaka huu mpaka taarifa itakapotolewa na Waziri juu ya mapendekezo yaliyotolewa kuboresha sekta hiyo ya uwindaji. Hata hivyo imekuja kugundulika kuwa Waziri Mwangunga ameshatoa maamuzi hayo na kuwaongezea leseni wawindaji hao kitu ambacho "kilimkorofisha" Mhe. Mzindakaya. Endapo Bunge lingeamua kupitia hoja hiyo na kumchukulia hatua Mhe. Mwangunga basi angekutwa na dharau ya Bunge (Contempt of parliament) kosa ambalo linalingana na lile la kudharau Mahakama (Contempt of court). Adhabu ya kosa hilo ni siku saba jela.
Vyanzo vyetu kutoka Dodoma vinasema kuwa baada ya kuona kuwa upepo hauendi upendo wake Mhe. Mwangunga akifuata njia iliyotengenezwa na Waziri Mkuu Pinda jana ambaye aliomba msamaha kwa wale wa Tanzania wanaoona amekosea naye mama Mwangunga aliona hana njia nyingine isipokuwa kuomba msamaha kwa Wabunge. Inaonekana Bungeni kumekuwa na hali ya huruma na baadhi ya wabunge wa CCM na hata wale wa upinzani wametangaza kumsamehe.
Hata hivyo haijulikani huko mbeleni ni kiongozi gani mwingine naye atakuwa tayari kuomba msamaha kwa mtindo huu na hivyo kukwepa kuwajibishwa. Maoni ya watu mbalimbali ambao wamekuwa wakifuatilia masuala haya wanaona kuwa itakuwa vigumu sana huko mbeleni kumwajibisha mtu yeyote kwani wotesasa watakuwa wanasimama kuomba samahani na wengine kumwaga machozi kwa "uchungu".