Fumanizi husababisha hisia zenye maumivu, hasira, kutokuaminiana, woga, aibu na kujilaumu. Lakini kufumania au kufumaniwa hakupaswi kuwa sababu ya kuwa mwisho wa ndoa yenu, ingawa kunaweza kuwa pia.
Baada ya fumanizi, inabidi ujitahidi kuelewa na kuweza kujenga tena ndoa yako, pengine sasa ikiwa ni ndoa imara zaidi. Hata hivyo hii inataka kujituma kwingi na uvumilivu na subira. Ndoa inaweza kuendelea hata baada ya fumanizi kwa kutumia ushauri, kupeana muda na kushirikiana. Kuna ndoa ambazo zimeweza kudumu zaidi baada ya fumanizi kutokea.
Pale kutoka nje kwa mwanandoa mmoja kunapogundulika hupelekea hisia kali kwa wanandoa wote, mshtuko, aibu, kujilaumu, kujiona mkosaji, hasira kali na wasiwasi. Kutokana na hisia hizi zote mara nyingi wengi hufanya maamuzi yasiyo mazuri kama kutengana au kuachana kabisa. Badala ya kufanya hivyo katika kipindi kile cha muda mfupi baada ya fumanizi, tunahitaji kuwa watulivu sana ili tuweze kuchukua hatua zinazofaa.
Kupata msaada:
Kwa uzima na afya yako mwenyewe, tafuta msaada kutoka kwa familia, rafiki, mchungaji, shekhe au mshauri yeyote unayemwamini wewe na kujihisi huru kwake. Kuongea kuhusu hisia zako kwa wale unaowapenda sana itakusaidia wewe kupunguza nguvu za hisia za maumivu ya tukio hilo. Kuongea na watu wengine kunaweza kukupa wewe uwezo wa kuelewa zaidi hisia zako na kupata mtazamo mwingine kuhusu tukio.
Pengine aliyetoka nje inawezekana hatosheki katika mahusianao katika ndoa yake au hawajibiki vizuri katika ndoa. Au pengine hawezi kudhibiti mihemko yake. Mabadiliko ya maisha kama kuzaliwa mtoto au upweke wa aina fulani, unaweza kuwa ndio sababu ya kutoka nje. Inabidi haya yatazamwe kabla mtu hajaamua lolote.
Kwa hiyo kujua sababu ya mwingine kutoka nje ni muhimu sana na hii inaweza kukupa ahueni, kwani unaweza kubaini kitu ambacho kinaonesha kwamba, kwako pia kuna matatizo. Hatua zitakazokusaidia kujenga upya ndoa yako baada ya fumanizi ni nyingi. Lakini hizi ni baadhi tu ambazo kwa mazingira yanayokukabili, zinaweza kukusaidia.
Kuacha kutoka nje ya ndoa:
Hatua ya kwanza ni kwa mwanandoa kuacha tabia ya kutoka nje ya ndoa kiukweli.
Kukubali kuwajibika:
Kama umetoka nje ya ndoa, kuwa tayari kuwajibika katika vitendo vyako.
Onyesha nia ya malengo yako:
Kuwa na uhakika kuwa wote wawili mko tayari kujenga upya ndoa yenu.
Onana na mshauri wa wanandoa:
Mtafute mshauri wa ndoa ambaye atakusaidia kujenga upya ndoa yako kama itakuwa inahitajika. Onana na mshauri wa ndoa ambaye alishawahi kukutana na kusaidia kutataua matataizo ya fumanizi. Mwepuke mshauri ambaye anaamini kufumania au kufumaniwa ndio mwisho wa ndoa yenu.
Kuchunguza tatizo:
Kufumania au kufumaniwa huzua matatizo katika ndoa. Chunguzeni kwa makini mahusiano yenu ili uweze kujua nini kilichosababisha au kilichopelekea kutoka nje ya ndoa na nini mfanye ili kuzuia kutoka nje ya ndoa tena
Kila mmoja apewe nafasi:
Kila mwanandoa anahitaji kupumzika kwa ajili ya kuondoa msongo na wasiwasi kutokana na tukio la fumanizi, hii ni kwa sababu huwa ni vigumu kusikiliza ushauri wakati mihemko iko juu sana.
Pata muda:
Epuka kujua undani zaidi kuhusu fumanizi la mwenzi wako kwa wakati wa mwanzoni. Ahirisha mjadala huo kwanza mpaka uzoee ile hali ya kumfumania mwenzi wako.
Mwisho wa ndoa au hapana ?
Siyo kila ndoa iliyoguswa na suala hili la fumanizi ni lazima imalizike kwa kutokuachana. Wakati mwingine kunakuwa na uharibifu mkubwa na wanandoa hawana budi kuachana na pia kama wanandoa hawako tayari kuwa pamoja tena.
Lakini kama wote mko tayari kujenga upya ndoa yenu, basi suala hili huwa rahisi sana na uhusiano utaendelea kuwa mzuri na wa amani zaidi.