Tungepata uhuru 2010 kama ni kweli!?
KUTOKA JF: KUNA WATU WANAELEZA KUWA WAISLAM WALIPINGA UHURU KUPITIA AMNUT
Utangulizi
Tatizo ni lile lile kwa kukosa kuijua historia ya kweli ya TANU na historia nzima ya kupigania uhuru wa Tanganyika.
JIBU LANGU
Ndugu zangu katika historia ya uhuru wa Tanganyika kuna mambo ndani ya historia hii hayakupata kuelezwa kwa kuogopa itakuwaje historia hii ikifahamika?
Kwanza historia yenyewe yote haikupata kuelezwa kwa ukweli.
Pili ugomvi wa Julius Nyerere na Sheikh Suleiman Takadir mwaka 1958 haukupata kuelezwa.
Historia ya AMNUT haikupata kuelezwa kwa ukweli wake.
Nimeona John Iliffe amenukuliwa kuhusu AMNUT.
Bahati mbaya sana John Iliffe juu ya kufanya kazi kubwa kuitafiti historia ya Tanganyika kuna baadhi historia zimemponyoka hakuzieleza kwa ithibati iliyostahili.
Mfano ameandika paper nzima ya historia ya Dar es Salaam Dockworkers Union (1970).
Mambo mengi muhimu hakuyaeleza na aliyoyaeleza hayako sawa.
Halikadhalika hili la AMNUT Iliffe kakwepa kueleza chanzo chake.
Chanzo cha AMNUT ni Uchaguzi wa Kura Tatu na ugomvi uliotokea baina ya Sheikh Suleiman Takadir Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU na Julius Nyerere Rais wa TANU.
Baada ya ugomvi huu ambao Sheikh Takadir alitoa shutuma nzito sana dhidi ya Mwalimu Nyerere Sheikh Takadir alifukuzwa TANU.
Baada ya haya kutokea ndipo AMNUT ikaundwa.
Maneno aliyosema Sheikh Takadir ni mazito sana sina ujasiri wa kuyaweka hapa hadharani.
Haya maneno ni mazito sana kiasi TANU wenyewe mpaka chama kinageuka kuwa CCM haikuwa na ushujaa kueleza Sheikh Suleiman Takadir alisema maneno gani.
TANU kwa hofu ya kauli Ile ya Sheikh Takadir ikamfuta katika historia yake ikawa kama vile Sheikh Takadir hakupata kuwepo.
Historia hii niliyoitaja hapo juu yote mimi nimeitafiti na nimeandika imo katika kitabu cha Abdul Sykes.
Ndani ya kitabu hiki nimemlaumu John Iliffe kwa kutokuwa mkweli.
Iliffe alinijibu kwa ukali sana katika review yake ya kitabu changu iliyochapwa katika Cambridge Journal of African History.
Hitimisho
Baada ya jibu hili waliokuwa wanakejeli Waislam kuwa ati walipinga kupatikana kwa uhuru wametoweka uwanja wa mapambano.
Hawaonekani sasa kutwa nzima jua linakaribia kutua.
Sijakata tamaa bado In Shaa Allah nawasubiri.