elivina shambuni
JF-Expert Member
- May 31, 2018
- 461
- 295
HIKI ndicho tulichokuwa tunakitaka. Ndivyo wanavyosema wakazi wa Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, wanaosema hivyo baada ya kilio chao cha muda mrefu cha kukosa majisafi na salama kupata ufumbuzi.
Wanasumbawanga na viunga vyake takribani 70,932 wanafungua maji ya bomba baada ya kazi hiyo kukamilika na Rais Dk. John Magufuli kuuzindua mradi huo hivi karibuni akiwa ziarani Rukwa.
Anawaambia serikali kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) wamechangia upatikanaji wa maji kwa gharama ya Sh. milioni 35. Wakati akizindua rasmi mradi huo mwezi uliopita Rais Magufuli, anasifu kazi hiyo na kuipongeza Wizara ya Maji kwa jitihada kubwa na kazi nzuri iliyofanyika.
Rais anawageukia wakazi wa Sumbawanga akiwataka kutunza na kuthamini huduma hiyo ili udumu kwa muda mrefu na inufaishe wateja wengi. Anaeleza kuwa serikali itaendelea kuwekeza zaidi kwenye sekta ya maji ili kumaliza tatizo la maji na kuwafanya Watanzania wafurahie huduma ya uhakika ya maji ambayo ni bidhaa ya muhimu kwa ajili ya ustawi kiafya na kiuchumi kwa kila binadamu.
TAARIFA YA MRADI
Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa, anaishukuru serikali kwa kuyapa maji umuhimu wa kipekee kwa kutoa kipaumbele cha kuanzishwa na kukamilishwa miradi mingi ambayo sasa kazi za uwekezaji kwenye sekta hiyo zimefikia zaidi ya miradi 547 ikiwamo 468 ya vijijini na 79 ya mijini. Yote hiyo ikiwa na thamani ya Sh. trilioni 3.98 na kwamba mingi ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na umaliziaji.
Waziri Mbarawa, anazungumzia mradi wa Sumbawanga akieleza kuwa ulikamilika Novemba, mwaka 2017 na kwamba muda wa matazamio ulikuwa mwaka mmoja, ambao ulikwisha Desemba 2018.
Anasema katika mradi huo mengi yamefanyika baadhi ya kazi zilizotekelezwa ni uchimbaji wa visima 17, ufungaji wa pampu kwenye visima hivyo vyenye uwezo wa kutoa maji lita milioni 13 kwa siku.
“Umehusisha pia kulaza mabomba yenye urefu wa kilometa 14.2 kutoka kwenye visima kwenda kwenye tangi la kukusanyia maji, kulaza bomba kuu za kupeleka maji mjini zenye urefu wa kilometa 21.8, kujenga mtandao wa usambazaji maji katika mji wa Sumbawanga wenye urefu wa kilometa 68 na ujenzi wa matangi ya maji sita ya kuhifadhia maji yenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 7,000.” Anasema Mbarawa.
UJENZI WA MRADI
Ujenzi wa mradi huo umesimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, Manispaa ya Sumbawanga (Suwasa) na kujangwa na kuanzia, Machi 8, mwaka 2013 hadi 2017. Akizungumzia mafanikio ya mradi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Suwasa, mhandisi Gibon Nzoa, anasema umeongeza uzalishaji wa maji kwa kiwango cha lita 7,500,000 kwa siku na kufikia lita 20,500,000 kwa siku.
Ukilinganisha na mahitaji ya sasa kwa Manispaa ya Sumbawanga ni lita 13,000,000 kwa siku hivyo kuna ziada. “Kimsingi huduma ya majisafi imeongezeka kutoka wakazi 70,935 sawa na asilimia 52 hadi kufikia wateja 106,400, sawa na asilimia 78, ukilinganisha na idadi ya wakazi katika Manispaa ya Sumbawanga ambao ni 136,414,” anasema na kuongeza: ”Ubora wa maji yanayosambazwa kwa wananchi umeongezeka na kufikia viwango vinavyokubalika kimataifa , eneo lenye mtandao wa majisafi limeongezeka kutoka kilometa 134 sawa na asilimia 52 na kufikia kilometa 240 ambazo ni asilimia 80.” Hata uwezo wa matangi wa kutunza maji umeongezeka kutoka lita 1,350 hadi 8,350, huduma bora ya maji yanayopatikana itaendelea kuchangia katika maendeleo ya sekta nyingine zinazotegemea maji kama viwanda, hoteli, utalii na usafi wa mazingira ambao umeboreka baada ya uwepo wa magari ya kunyonya majitaka na ujenzi wa mabwawa yake.”
WATEJA WANASEMAJE?
Mkazi wa Manispaa ya Sumbawanga, Halima Wangao, anakiri kuwa mradi huo ni msaada mkubwa baada kuchoshwa na magonjwa ya mlipuko yaliyokuwa yakisababishwa na ukosefu wa majisafi na salama kutokana na matumizi ya maji yasiyo salama.
Anazungumzia pia gharama kubwa za ununuzi wa maji kuwa zimepungua baada ya wakazi wengi kuunganishiwa huduma ya maji na kuanza kulipia ankara za maji kila mwezi ambazo ni nafuu ukilinganisha na bei ya maji iliyofikia Sh. 1,000 kwa dumu. “Tulikuwa tunapata shida sana wakati wa kutafuta majisafi na salama na wakati mwingine tulishirikiana na mifugo yetu lakini tuna mkombozi,” anasema Wanguo. Salum Mbalamwezi, anasema kuwa awali shida ya maji ilikuwa inasababisha migogoro katika ndoa kwani kinamama walikuwa wanatumia mwanya wa shida ya maji kukosa uaminifu.
AHADI ZAIDI
Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Aeshi Hillaly, anasema pamoja na kukamilika kwa mradi huo, serikali imeendelea na mipango iliyopo ya uboreshaji wa huduma ya maji katika Manispaa ya Sumbawanga kwa kufanya jitihada za upanuzi wa mtandao wa majisafi. “Mtandao wa majisafi umeongezeka kwa kilometa 18 na ununuzi wa dira za maji 1,200 kwa gharama ya Sh. milioni 409. “Utekelezaji wa mradi huu umewanufaisha wakazi wa maeneo ya Kisiwani, Sokolo, Majumba Sita, Kasisiwe, Katai, Muhama na Katusa.,” anasema mbunge.
Anawaambia wananchi kuwa Sh. milioni 330 zimetengwa kwa ajili ya upanuzi wa mtandao wa majisafi katika manispaa hiyo na taratibu za ununuzi wa mabomba na viungio zinaendelea. Kukamilika kwa kazi hiyo kutawanufaisha wakazi wa maeneo ya Kashai, Utengule, Energy na Kasisiwe,” anaahidi mbunge wao.