SoC04 Ni Wakati wa Watanzania kuchukua hatua

SoC04 Ni Wakati wa Watanzania kuchukua hatua

Tanzania Tuitakayo competition threads

Michael AP Mduma

New Member
Joined
Jul 25, 2023
Posts
1
Reaction score
0
Watanzania tunapopatwa na changamoto fulani, wengi wetu huishia kulalamika tu, badala ya kuchukua hatua. Hali hii imefanya watesi wetu kuzidi kutuonea Kwa sababu hata wao wanajua Kuwa hatutochukua hatua yoyote ile zaidi ya kuishia kulalamika. Jambo hili hupelekea kutokuwajibika. Na kadri mtazamo huu unavyozidi kujengeka katika fikra zetu ndivyo tunavyozidi kuona kuwa hali ya kuonewa ni jambo la kawaida tu ilhali Si kweli.

Imefika wakati watanzania tuanze kuchukua hatua pale tunapoona tumetendewa isivyostahili. Wengi wetu hatujui haki zetu na ndio sababu tunakosa kujitetea hata mahali ambapo sisi ni wenye haki.

Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo kila mtanzania ni vema akafahamishwa ili kugeuzwa na kufanywa upya fikra zake.....

1. Dereva aliyeandikiwa faini kutokana na kusahau leseni yake, asingefanyiwa hivyo kama angejua kuwa sheria ya usalama barabarani sura ya 168 kifungu cha 77 (1) sheria inasema kuwa dereva hatatiwa hatiani kutokana na kutokuwa na leseni muda huo, isipokuwa anazo siku tatu za kuonesha leseni hiyo tokea siku aliyosimamishwa. Lakini kwa kutokujua, baadhi ya madereva wamejikuta wakiandikiwa faini na wengine kulazimika Kutoa rushwa wakidhani wametenda kosa.

2. Mkopaji asingehaha kulipa riba baada ya kukopeshwa fedha na mtu binafsi ambaye hana leseni ya kufanya biashara ya fedha. Sheria inakataza watu binafsi kukopeshana kwa riba au kwa kuweka reheni mali fulani. Kifungu cha 6(1) cha sheria ya mabenki na taasisi za fedha kinasema kuwa mtu yeyote ambaye hafanyi biashara ya fedha na hana leseni hiyo Haruhusiwi kupokea reheni ama kuchukua riba kutoka kwa mtu yeyote. Lakini kwa kutokujua hili watu wengi wamepokwa mali zao na watu binafsi kwa sababu tu walishindwa kutoa riba.

Watu wanaweza kukopeshana kibinadamu kwa maana ya kusaidiana tu na sio kwa lengo la kutafuta faida. Ikiwa mtu anataka kufanya biashara ya fedha hana budi kujisajili, lakini kinyume na hapo mtu akifanya hivyo itakuwa ni kosa kisheria.

3. Sheria inaruhusu kudai zawadi ulizotoa pale uchumba unapovunjika. Vijana wengi (hasa wa kiume) wamejikuta wakifikia hatua ya kujitoa uhai kutokana na msongo wa mawazo baada ya kuachwa na wapenzi wao katika mazingira yasiyoeleweka, ukizingatia kuwa kijana huyo alijitoa sana kwa mpenzi wake kwa fedha na muda pia. Vijana wasifikie hatua ya kujiua tena kwa sababu sasa wanafahamu kuwa sheria ya ndoa iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 kifungu cha 71 kinasema mtu anayo haki ya kufungua shauri akidai zawadi alizotoa baada ya uchumba kuvunjika. Na sheria haikuishia kwenye zawadi tu bali kifungu cha 69(1) cha sheria iyo hiyo kinasema mtu anayo haki ya kufungua shauri kudai fidia kutokana na maumivu aliyoyapata baada ya mchumba wake kumwacha katika mazingira yasiyoeleweka.
Kwa Hakika vijana wakijulishwa hili, bila shaka tutapunguza wimbi la vijana wetu kujiua Kwa Sababu walau watakuwa wamepunguza uchungu.

4. Mtumishi wa umma anayehisi hakutendewa haki wakati aliposimamishwa kazi, anaruhusiwa kukata rufaa. Sheria namba 8 ya 2002, Sheria ya utumishi wa umma, iliyofanyiwa marekebisho na Sheria namba 18 ya 2007, kifungu cha 25(1) (b) inaeleza haki ya rufaa kwa mtumishi ambaye anahisi hakutendewa haki na mwajiri wake. Ni vema watanzania tukafahamishwa kuwa kukata rufaa sio ukaidi, dharau, kejeli au ukorofi kwa serikali, bali ni haki kama ilivyo haki nyingine kama kupewa mshahara au likizo.

5. Mjane asingenyang'anywa stahiki zake kama angejua kuwa kuna aina mbili za mali anazostahili. Sheria ya ndoa sura ya 29 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 pamoja na sheria ya usimamizi na uendeshaji wa mirathi, sura ya 325 inasema kuna aina mbili za mali anazostahili mjane. Kwanza, ni mali inayotokana na machumo ya pamoja (kwa maana ya wanandoa) na pili ni mali ya urithi kutoka katika sehemu ya mali ya marehemu mume wake.

Na jamii ifahamu kuwa hata mama wa nyumbani ambaye anafanya kazi kama kufua, kupika na kutunza watoto kazi hizo zinahesabika ni mchango katika kupatikana kwa mali.

6. Mke halali wa ndoa anaweza kukopa Kwa jina la mume ambaye kwa makusudi, hatoi matunzo Kwa Mke au Watoto. Tena kukopa kwenyewe si lazima amtaarifu mume husika. Sheria ya ndoa sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010, kifungu cha 64 kinaeleza jambo hili.

Na atakayewajibika kulipa mkopo huo ni mume mwenyewe kwa sababu ilikuwa ni jukumu lake kuihudumia familia sawasawa na kifungu cha 63 (a) ambacho kimempa mwanaume jukumu la kuitunza na kuijali familia yake.

7. Sheria ya mikataba sura ya 345 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009, kifungu cha 10, sheria inasema makubaliano yoyote yanaweza Kuitwa Mkataba ikiwa yamekidhi vigezo vitatu ambavyo ni Hiari, Wahusika wenye hadhi (Kwa maana Kwamba wawe na umri usiopungua Miaka 18 na wawe na Akili timamu)
Sheria Hapa haijasema Moja ya vigezo ni Kuwa Lazima kuwe na Maandishi.

Hivyo basi, Ni vema Watanzania wakafahamu Kuwa Makubaliano Yoyote Yale hata yakiwa ni Kwa njia ya mdomo tu, ikiwa yamekidhi vigezo Hivyo Hapo juu basi yataitwa Mkataba. Iwe ni Katika biashara, Kazi au pengine popote. Kusema Kuwa "hatukuandikishiana hivyo huu si Mkataba" dhana hii inapaswa kufa mara moja.

Sambamba na hayo yaliyotajwa hapo juu, pia watanzania tunapaswa kutambua haki zetu katika maeneo mbalimbali kama vile vituo vya afya, vituo vya mabasi, mahakamani, vyuoni, sehemu za ibada n.k ili kuongeza uwajibikaji kwa watoa huduma. Tunapaswa pia kubadilika na kuanza kuchukua hatua pale tunapoona sheria inapindishwa Kwa sababu mtu wa kwanza kusimamia sheria si mwingine, ni wewe mwenyewe.
 
Upvote 4
Back
Top Bottom