SoC02 Nidhamu ya Fedha

Stories of Change - 2022 Competition

Esq NeyB

Member
Joined
Mar 26, 2017
Posts
5
Reaction score
5
HADITHI YA TEKE TEKE.

Bwana Athumani. Kila ifikapo jioni, yeye na jiko lake, anawasha moto, kiupepo cha jioni kikikoleza mkaa huku cheche zikiruka huku na kule. La haula, moto umekolea vyema huku fuko la mahindi likimtazama. Anachukua hindi moja baada ya jingine na kutoa maganda, nywele za mahindi zikisambaa huku na kule. Anachoma mahindi yake huku akiyageuza geuza yasiungue, yananuki vizuri harufu ya kuiva inayowatamanisha wapiti njia.

Bwana mmoja na mkewe, wakiwa ndani ya gari yao Toyota Rav4 Old Model, kama kawaida yao, wao kila jioni wakitoka kazini, hupita kwa Bwana Athumani. Maskini! Wamekula chunvi nyingi, meno yao yamechoka, “nichagulie mahindi laini kama kawaida” alisikika Bibi huyu ambae ameketi upande wa kuume wa mumewe.

Bwana Athuman, akachukua mahindi mawili yamoto, kayafunga vizuri kwende ganda lake, kisha akapeleka kwenye gari na kumkabidhi Bibi yule. Bibi katoa hela aliyopewa na mume wake, akamkabidhi mchoma mahindi Bwana Athumani, kisha hao wakaenda zao.

Bibi…. “aah mume wangu, hindi tamu hili bado teke teke, linasukari yakutosha,”

Babu…. “nikweli mke wangu, mahindi haya ni matam sana, chukua uonje na langu”

Bibi akionja hindi la mumewe, mmmmh tamuu.

Bibi… Unajua nini mume wangu

Babu…Sijui Mkewangu, nijulishe wewe.

Bibi… Kijana huyu anaonekana kama ni muhitaji, kazi hii ya kuchoma mahindi, atakua anaifanya kwasababu amepambana kutafuta ajira bila mafanikio. Unajua ajira zimekua ngumu sana, sio kama miaka yetu, ukimaliza chuo, ajira inakutafuta.

Babu… Nikweli usemayo Mke wangu,

Bibi… Nimetafakari, nikaona tumsaidie kijana huyu kwa fedha kidogo kama sadaka ili aweze kuongeza mtaji wa biashara yake nae aweze kupambana na hali ya uchumi.

Babu… umewaza vyema Mke wangu, sadaka si lazima tupeleke kanisani tu, bali hata kuwasaidia wahitaji.

Babu na Bibi wakaanda fungu la fedha kwaajili ya kumpelekea bwana Athumani. Kama kawaida, jioni ilipofika, wakiwa kwenye gari lao wakafika kwa Bwana Athumani. Athumani huyo akijongea na mahindi mawili mkononi, la! Anaona Bibi akifungua mlango wa gari na kushuka chini, anapigwa na butwaa, anajiuliza maswali kichwani yasiyo na majibu. Anaamua kuvunja ukimya, Bibi kuna tatizo! Mara anamuona Babu nae akishuka, huyoo anasogea mahali aliposimama. Nguvu zinamuisha huku kijashochembamba kikimtoka. Mahindi mawili yakiwa mazito mkononi mwake kama kilo za mtama.

Babu…Bwana Athumani, mimi na mke wangu, tumekua wateja wako wa mahindi kwa muda mrefu. Tumeona jitihada zako katika kupambana na hali ya Maisha. Hivyo tukaona si vyema kuwa na mkono wa birika kwa mtu anayefurahisha matumbo yetu kila msimu wa mahindi. Hivyo tumekuandalia bahasha hii yenye fedha kichele ili uweze kukuza biashara yako.

Bwana Athumani akatahamaki, kisha akatabasamu! Akavuta pumzi ndeefu kisha akainamisha kichwa chini. Akifikiri kichwani mwake, yawezekana vipi mambo haya!

Babu akamshika bega Bwana Athumani, kisha akatoa bahasha mfukoni mwake ili akamkabidhi Bwana Athumani.

Bwana Athumani…aaah, nashukuru sana kwakunifikiria na mawazo mema mliyoniwazia, aaa., asanteni, lakini sitaweza kupokea bahasha hii hapa bali nina ombi moja kwenu.

Bibi… mmmh! usijali Bwana Athumani tafadhali pokea bahasha hiyo yenye fedha taslimu laki tano, usiogope, itakusaidia kukuza biashara yako.

Bwana Athumani… Ndio, nitaipokea, lakini naomba niwakaribishe nyumbani kwangu kwanza. Hivyo tubadirishane namba za mawasiliano ili tuweze kuwasiliana muweze kufika kwangu.

Babu…Ni sawa Bwana Athumani, tumedhamilia jambo hili, hatuna budi kutimiza ombi lako pia.

Ilipofika Jumamosi, Bibi na Babu walijiandaa kwaajili ya Kwenda nyumbani kwa Bwana Athumani. Safari ya kuelekea Goba ikaanza, walipokaribia, Bwana Athumani alitoka nje ili kuwapokea. Akafungua geti ili gari iweze kuingia ndani. Wageni wakatoka ndani ya gari.

Bibi… akiwaza akilini, Bwana Athumani ametukaribisha hapaaaa…mmh itakua ni mahali alipoajiriwa kwaajili ya kukata majani na kuhudumia maua au..

Bibi anashtushwa na sauti ya Bwana Athumani, karibuni ndani, mjisikie mpo nyumbani. Bibi anamtazama Babu usoni, macho yanagongana.

Ni nyumba ya Ghorofa moja iliyojengwa kisasa. Wakaingia na kufika sebureni, wanakaribishwa na marashi mazuri kutoka kwenye Chetezo. Wakiketi kwenye sofa za lether imara kabisa. Mke wa Bwana Athumani...Salaamu wageni wetu, karibuni sana, Bila kupoteza muda ni vyema kama tutajongea kwenye meza ya chakula ili tujumuike kwa karamu hii pamoja. Babu na Bibi wakajongea kwaajili ya kula. Meza yenye mboga saba, matunda, juice, vyakula vya aina tatu tofauti.

Bibi... akitafakari akilini…niyaonayo ni kweli! Au naota!......

Baada ya chakula, wageni walikaribishwa bustanini ambako waliketi na Bwana Athumani. Mazungumzo yao yalikua hivii

Bwana Athumani…Bibi na Babu, mimi ni mfanya biashara ndogo ndogo, wakati wa mahindi ninachoma mahindi na kuuzia wapita njia. Lakini nina mifugo kama kuku, bata, na kanga ambao kupitia wao nauweza kuuza mayai, nahata wao. Pia nina Sungura ambao wanapendwa sana na wazungu kuliwa kama nyama na hata kufugwa, hivyo ninatumia muda wangu mwingi katika kufuga, na kutafuta masoko ili nifikie ndoto zangu bila kusahau nidhamu ya fedha.

Babu… akiwa ameshika tama, akitafakari akilini mwake, mimi tangu nilipoajiriwa na serikali miaka ishirini iliyopita, bado nipo kwenye nyumba niliyohifadhiwa na serikali, sina hata kibanda…akishtushwa na sauti ya jogoo...kokorikooooo……kooooo. Anakaza macho kwa Bwana Athumani, mmh kijana, ni vyema sana, unajua sisi watu tulioajiriwa hatuna muda wa kuhudumia mifugo, muda mwingi tunafanya kazi za kutumia akili, na sio zile zinazohusisha mwili moja kwa moja. Naaa tukistaafu, muda wetu wa kuishi unakua mfupi sana kwasabu tulizoea Maisha ya kazi za kuajiriwa na si zile zakujiri. Ni ngumu sana kwa umri huu kuanza kufuga na kutafuta masoko. Likini kwa nyinyi mlioanza katika ujana ni rahisi sana kwasabu ya uzoefu mkubwa. Nikupe hongera Bwana Athumani, tumejifunza kitu kikubwa, nafasi bado tunayo. Tunashukuru kwa kutukaribisha nyumbani kwako. …akiwa amesimama……aa naona jua limetwaa, niwakati wa kurejea nyumbani kwetu sasa…

Bibi…akijikusanya kusanya…...

Bwana Athumani…...nikweli Babu, hivyo natumaini leo unaweza kunikabidhi bahasha yangu…

Wakatizamana. Wakacheka. Babu akajibu, nadhani hii itakua ni bahasha yangu ya mtaji.

Mwisho.
 
Upvote 3
Umenena vema sana, watumishi wengi wanapata shida sana kusimamia shughuli za binafsi, pamoja na mambo mengine, muda wa kusimamia miradi ni changamoto kubwa sana
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…