SoC03 Niende kijijini, ama nibaki mjini?

SoC03 Niende kijijini, ama nibaki mjini?

Stories of Change - 2023 Competition

Enigmatic_

Member
Joined
May 12, 2023
Posts
16
Reaction score
13
Kuzaliwa mjini, sehemu ambayo imetawaliwa na usasa inaweza kuonekana ni bahati kwa wengi. Hii ni kwa sababu ya urahisi wa kupata vitu vingi ikiwemo huduma, taarifa na kadhalika. Lakini kwangu mimi sizioni faida hizo. Kwangu kuwa mjini ni kitu kinachoitesa sana akili yangu. Sio bahati. Kabisa.

Nikiwa kama mtoto mwenye miaka 11 ninayeishi kwenye familia yenye mchanganyiko wa ndugu mbalimbali, wakiwepo baba zangu wakubwa, binamu zangu na wengine, bila uwepo wa baba na mama (ambao walitengana nikiwa na miaka miwili) Napata shida hasa linapokuja suala la namna ninavyokuzwa. Mimi, kama mtoto, najua ni kwa namna gani malezi yangu nikiwa mdogo yanaweza kuathiri maisha yangu ukubwani. Na kwa maisha ninayoishi ninaona kabisa ni kwa namna gani huko mbele maisha yangu yatakuwa. Kama kawaida, najua ulimwengu utanilaumu. Kila kona nitaonekana mbaya. Lakini ulimwengu utakuwa umejisahaulisha kuwa watoto ni kama ndoo tupu; ikijazwa maji inakuwa ndoo yenye maji. Vivyo hivyo ikijazwa maziwa!

Jamani, hapa ninapoishi matusi na maneno machafu ni kiungo kikubwa cha pishi la maongezi ya kila siku. Haiwezi kupita siku bila kutukanwa. Sehemu za siri za binadamu zimekuwa rangi nzuri na muhimu katika uchoraji wa maongezi ya kila siku. Sio baba mkubwa wala shangazi, wote ni watoaji wazuri wa kinywaji cha matusi. Hiki kitu sikipendi. Lakini nitafanyaje mimi kama mtoto, ambaye inatakiwa nitii na nisiwakosoe wakubwa zangu? Najua sawa. Mimi kama binadamu, tena mtoto, nakosea. Lakini matusi hayapaswi kuwa mshahara wa makosa yangu. Kuna njia nyingi za kurekebishana nje na matusi.

Kuna muda natamani kwenda kwa bibi, kijijini. Labda ntapata ahueni. Labda akili yangu itatulia. Lakini nawaza: nitaaga naenda kufanya nini? Naenda kukaa muda gani? Natamani nitoke hata maisha yangu yote. Nikae mbali kabisa. Nisisikie maneno machafu tena. Lakini huu ni mtihani sana kwangu. Na kuufaulu sidhani!

Kibaya Zaidi, hata mtaani, karibu kila kona ninayopita mambo ni yaleyale: si vikongwe wala vijana, wote ni watoaji wazuri wa maneno machafu. Hata hawajali kwamba wanaongea mbele ya nani. Hata hawajali, ni kwa namna gani na kwa kiasi gani wanaweza kuyaathiri maisha yangu na watoto wengine. Muda mwingine huwa natulia na kujiuliza: je ni kweli mtoto ni mali ya jamii? Jamii inawajibu gani kwa mtoto? Mtoto anawajibu gani kwa jamii yake? Lakini baadaye huwa najipa majibu kwamba jamii yoyote hutaka na huwajenga watoto kuwa watiifu kwa wakubwa, kufuata sheria, taratibu, mila na desturi za jamii yake. Lakini muda mwingine huwa naenda mbali Zaidi. Huwa najiuliza swali moja kubwa: je wajibu wa mtoto kwenye jamii inayooga kwenye dimbwi la matusi na maneno machafu kwa ujumla wake ni upi? Vipi naye akivua nguo na kuyaoga maji hayo, atakuwa sahihi? Vipi akikataa na kuwataka wakubwa (ambao inatakiwa awaheshimu na kufuata kile wanataka) waachane na hicho kitu atachukuliwaje? Nawaza!

Kinachonichanganya Zaidi labda ni shule na kile ninachojifunza. Shuleni najifunza kutotoa maneno machafu. Lakini cha ajabu, baadhi ya wanaonifundisha (yaani walimu) ni mabingwa wa kutoa maneno machafu ambayo kiujumla yanadhalilisha na kuondoa thamani ya mtu. Muda mwingine unaambiwa maneno ambayo kiujumla yanakatisha tamaa na kuona wewe si kitu mbele za watu. Yanaumiza. Yanakufanya unyong’onyee kila muda yanapojirudia kichwani. Unafanyaje kwenye mazingira kama haya? Mwalimu ni mkubwa. Siwezi kumrekebisha wala kumkosoa!

Sitosahau siku moja niliyoitwa ma‘sketi’ na mwalimu mmoja wa kike. Sio kwamba jina langu halijui. La hasha! Ilikuwa ni kebehi. Niliitwa hivyo kwa sababu navaa sketi ndefu kuliko wenzangu wote darasani. Nilijisikia vibaya sana. Lakini nilikumbuka kwamba huyu ndo yule mwalimu wa uraia. Ndo yule anayefundisha mila na desturi za kitanzania!

Safari yangu ya kwenda na kurudi shule ndio mtihani mgumu Zaidi. Kwanza nitakaa sana kituoni kusubiri daladala ambazo kwa mida hiyo (ya asubuhi na jioni) huwa zinajaa sana. Nikibahatika kupanda gari basi nakuwa nimefaulu mtihani wa kwanza. Mtihani wa pili ni kusikiliza maneno machafu yanayotoka kwa kondakta na kwenda kwa baadhi ya abiria. Huwa ni majibizano kweli. Kila mtu huwa na lake kichwani. Mwingine labda ametoka kwenye mihangaiko na mambo yameenda mrama. Basi hasira zake tutaziona tu. Mvua ya matusi itanyesha sana. Mwamvuli hauna kazi kabisa. Labda uvae yale madudu wanayovaa watu masikioni.

Muda mwingine huwa natamani niweke pamba masikioni ili nisisikie chochote nijikute tu nimeshafika ninapoenda. Lakini hata pamba nahisi kuna muda haziwezi kuvumilia kutopitisha baadhi ya matusi. Lazima yatavuja tu na kunifikia. Hapo inabidi kuwa mvumilivu kweli. Lakini nitafanyaje kwenye mazingira kama haya? Wakubwa wanaongea. Watoto yatupasa kutulia. Kimya kama hatupo. Tupo kama hatupo!
 
Upvote 7
Mjini changamoto,kijijini changamoto,chamsingi ni kukabiliana nazo na kutafuta amani ya moyo
 
Back
Top Bottom