Soma taarifa hii ni ya kweli:
'Katika kijiji kimoja alitokea kijana mmoja ambaye aliongea na wanandoa wawili kama ifuatavyo: Alipomwendea mke alimwambia kuwa mumeo anao mkia sehemu ya nyuma pale makalio yanapopakana, endapo unataka kupata ukweli mtakapokuwa kwenye mechi peleka mkono wako mahali pale nawe utajiridhisha. Muda mfupi baadaye akakutana na mume naye akamweleza vivyo hivyo. Kila mwanandoa akaamini kwamba mwenzake anao mkia huko nyuma. Kwa bahati mbaya mke alikuwa wa kwanza kupeleka mkono kwenye makalio ya mume; mume aling'aka na kumwuliza kwa nini unapeleka mkono wako huko? Mke hakujibu, ndipo mume naye alipojitosa kupapasa eneo la makalio ya mama, mke naye aling'aka vile vile ndipo walipoulizana kwa upole kwa nini kila mmoja alitaka kumpapasa mwenzake ndipo ilipofahamika kuwa kila mmoja alikuwa na taarifa za mwenzake kuwa na mkia. Walijikuta wote wawili wamedanganywa na mtu yule yule kwa vile alitaka kuvuruga uhusiano wao wa ndoa.
Nionavyo mimi, inakupasa ufanye utafiti wa kina sana kupata ukweli wa huyo mchumba wako kama kweli familia yake ni ya wachawi, inawezekana mtu aliyekuambia anayo nia ovu kama taarifa hiyo hapo juu inavyojieleza. Kama mtoto ametulia utayasikia mengi sana mfano ukoo wake una magonjwa ya kurithi kama ukoma na mengineyo. Kuwa makini sana katika kipindi hiki unapoelekea kujipatia jiko.