kmasanja20
Senior Member
- Jul 23, 2022
- 128
- 368
Kubuni na Kutengeneza Kifaa Kinachotatua Changamoto ya Malipo ya Bili za Umeme Kwenye Wapangaji Wengi.
Imeandikwa na: K. Masanja
Imeandikwa na: K. Masanja
UTANGULIZI
Sayansi na teknolojia katika Dunia ni dhana muhimu sana katika kuleta maendeleo. Licha ya kwamba katika nchi zinazoendelea kuna vikwazo mbalimbali kama kukosa mwendelezo na usimamizi, lakini kupitia taasisi mbalimbali za elimu na wataalamu hapa nchini Tanzania, watu wanaendelea kupata mwamko na kutumia ubunifu katika swala zima la sayansi na teknolojia. Makala hii inaeleza ni jinsi gani nimeweza kutumia elimu na ubunifu kutengeneza kifaa kinachotatua changamoto ya malipo ya vifaa vya umeme vinavyotumiwa na wapangajia zaidi ya mmoja mfano; Fensi za umeme, Taa za nje za ulinzi, Pampu za maji na Geti za umeme.
TAARIFA YA TATIZO
Kwa mfumo uliopo, vifaa tajwa hapo juu, vinakua vimeunganishwa kwenye mita ya mpangaji mmojawapo, swala ambalo hupelekea mpangaji huyo kudai mchango wa malipo ya umeme wa matumizi wa vifaa hivyo. Kwa sababu mbalimbalii, baina ya wapangaji wamekua wakikimbia, kuchelewesha na kupuuza mchango wa malipo hayo, kitu ambacho kimepelekea upotevu wa muda kukusanya na kudai mchango, migogoro, kutelekezwa, kuhairishwa na kuachwa kwa huduma nzuri zinazopatikana au kutolewa na vifaa hivyo vya umeme.
NJIA ZILIZOPO ZA UTATUZI WA MALIPO
Mpaka sasa kuna njia tofauti tofauti zimekua zikitolewa ili kujaribu kutatua tatizo la mgawanyo wa ulipaji bili za umeme kwenye apatimenti na nyumba za kupanga. Njia hizi zinatumia mita kama ilivyoelezwa hapa chini.
- Mita shirikishi
Hii ni njia inayotumiwa kwenye nyumba nyingi za kupanga ambayo wapangaji wote wanakua wameungwa kwenye mita moja. Hivyo ni wajibu wa mpangaji au mwenye nyumba anaeaminiwa kufanya mgawanyo na wapangaji wote kushiriki katika malipo. - Mita ndogo
Hii ni njia bora kuliko ile ya kwanza inayotumia mita ndogo ndogo zinazoweza kupima na kuonesha matumizi ya umeme ya mpangaji mmoja mmoja na malipo kupewa yule anaemiliki mita kuu. Kielelezo namba 1, kinaonesha jinsi mita ndogo inavyotumika.
Kielelezo namba 1: Mfumo wa matumizi ya mita ndogo za umeme.
CHANGAMOTO YA NJIA ZILIZOPO
Matumizi ya mita shirikishi na mita ndogo maranyingi huhusisha ukokotozi wa kutumia mikono au kichwa ambao unaathiriwa na makosa ya kibinadamu na kupelekea malipo ya bili yasiyo na uwiano hivyo kufanya njia hizi zisifikie lengo la kutatua changamoto iliopo.
KIFAA KAMA SULUHISHO LA MALIPO YA UMEME
Baada ya kuona kuwa, njia zilizopo bado hazijakidhi mahitaji ya kutatua tatizo la malipo kwa wapangaji nikaamua kubuni na kutengeneza kifaa ambacho kinasaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha malipo ya bili ya umeme. Kielelezo namba 2, kinaonesha picha ya kifaa hicho ambacho kinaitwa Kichagua umeme (APS).
Kielelezo namba 2: Kichagua umeme (APS)
TEKNOLOJIA YA KIFAA NA KILIVYO TENGENEZWA
Kichagua umeme (APS) ni kifaa ambacho moja kwa moja kitachagua nguvu ya umeme kutoka kwenye mita kuu za wapangaji, moja baada ya nyingine kwa muda fulani, ili kuhakikishwa kuwa kila mpangaji anachangia takribani kiasi sawa cha umeme kwenye vifaa wanavyochangia kimatumizi richa ya kua kila mmoja ana LUKU mita yake. Kila mpangaji atanunua umeme wake kama kawaida, wakati ule kifaa kitafanya kazi ya kuchagua umeme kutoka kila mpangaji kwa muda sawa na kupeleka kwenye mfumo wanaochangia matumizi. Kifaa hichi kimetengenezwa na sehemu kuu tatu ambazo zinashirikiana katika utendaji kazi;
Sehemu ya kwanza: Sensa, ambayo imeundwa na rezista zinazotegemea mwanga na diodi zinazotoa mwanga, hivyo kama kuna umeme, diodi zitawaka na rezistensi kwenye rezista itapungua na kuruhusu kiwango kidogo cha volti kwenda sehemu ya pili.
Sehemu ya pili: Kichwa cha kifaa, ambacho kimeundwa na kidhibiti kidogo (maikrokontrola) aina ya Arduino uno kinachopokea taarifa kutoka kwenye Sensa na kutoa maamuzi ya kuswichi yanayofanywa na sehemu ya tatu. Kinatumia lugha ya compyuta na maamuzi yanayotolewa yanategemeana na lugha iliyoandikwa.
Sehemu ya tatu: Swichi, ambayo imeundwa na rilei zinazofunga na kufungua kutokana na taarifa kutoka kwenye Sehemu ya pili. Idadi ya rilei inategemeana na idadi ya LUKU mita au wapangaji waliopo kwenye apatimenti moja. Kielelezo namba 3, kinaonesha muonekano wa kimuunganiko wa ndani na sehemu kuu za kifaa.

Kielelezo namba 3: Muonekano wa ndani wa kimuunganiko wa kifaa.
MFUMO WA UTENDAJI KAZI WA KICHAGUA UMEME KWENYE NYUMBA
Katika mfumo wa utendaji kazi wa kichagua umeme-APS, ni muhimu kuzingatia kuwa, kifaa kitahakikisha, kila mpangaji atatumia muda wa masaa 24 tu kwa kila mzunguko kupeleka umeme kwenye vifaa wanavyochangia. Hivyo kwa wapangaji watatu, watatumia masaa 72 (siku 3) kukamilisha mzunguko mmoja, yaani katika hali ya kawaida ambayo kila mpangaji atakua na umeme, mzunguko utakua; Mpangaji- A, Mpangaji-B, Mpangaji- C, kwa mzunguko wa kwanza, na mzunguko utaendelea kujirudia. Muda ambao umeme wa mpangaji husika utakua unatumika, utaoneshwa na kiashiria cha taa ndogo kama inavyooneshwa kwwenye Kielelezo namba 4, ambacho (a) ni muda wa Mpangaji- A, (b) ni muda wa Mpangaji- B, na (c) ni muda wa Mpangaji- C.
Kielelezo namba 4: Kichagua umeme kwa muda wa Mpangaji- A, Mpangaji- B, na Mpangaji- C.
Kunakipindi ambacho mpangaji husika anakua hana umeme, kipindi hiki kifaa kitachagua mpangaji anaefuata na kipindi tu umeme ukirudi kwa mpangaji ambae hakua na umeme, kifaa kitamrudia na kukamilisha muda ambao alikua amebakiza na mzunguko utaendelea kama kawaida. Kielelezo namba 4, kimetumia taa moja ya umeme lakini kichagua umeme kinaweza kutumiwa kwenye vifaa vingi kama vile; Taa za nje, Geti la umeme, na Pampu ya maji vinavyochangiwa na wapangaji kama inavyooneshwa na Kielelezo namba 5, hapo chini.
Kielelezo namba 5: Muonekano wa kichagua umeme-APS, kwenye huduma mbalimbali za umeme kwenye nyumba ya wapangaji wengi.
HITIMISHO
Kifaa hiki kipo kwenye hatua zake za awali za utekelezaji na matumizi lakini kikiboreshwa zaidi kinaweza kwenda mbali zaidi kimatumizi ya umeme ya vifaa vingi vinavyochangiwa na wapangaji na pia hata vile ambavyo havihusishi umeme moja kwa moja kama vile malipo ya bili za maji.
Ubunifu zaidi unahitajika katika sayansi na teknolojia na ubunifu huu uweze kuthaminiwa na mfumo na kupewa kipaumbele ili kuleta mabadiliko yenye tija na kwa vizazi vya baadae. Makala hii imetumika kama mfano lakini katika jamii kuna wabunifu wengi, waliosoma na ambao hawajasoma ambao wakitambuliwa, kuendelezwa na kupewa kipaumbele na Serikali pamoja na mifumo iliopo watakua na mchango mkubwa sana katika sayansi na teknolojia ya nchi yetu.

Attachments
Upvote
495