Nilivyonusurika Kifo baada ya Mzee kunitimua nyumbani - 17.
Mtatiro "Mwanangu mimi unadhani kwanini sitaki kukaa kwa ndugu!"
Aliendelea "Tatizo ukiongea unaweza kuonekana mbaya wakati unadai chako"
Mimi "Nakomaa sana mwanangu na huku kuna baridi kishenzi,lakini jamaa hilo halioni"
Mimi "Ngoja niangalie hali itakavyokuwa nikiona miyeyusho nachafua!"
Mtatiro "Wewe ukiweza njoo tukapambane minadani mwanangu!"
Aliendelea "Kuna hela nasubiri braza anipe nianze kukimbizana minadani!"
Aliendelea "Kwani ule mzigo uliisha kabisa?"
Mimi "Bado upo kaka lakini kidogo"
Mtatiro "Kama ngapi imesalia!"
Mimi "Ipo kama laki 6"
Mtatiro "Hapo ukichenji utabaki na kasalio kidogo,hebu ngoja wiki hii nicheki braza akinitumia tuangalie tusepe wapi!"
Mimi "Poa mwanangu!"
Yalikuwa ni maongezi kati yangu na rafiki yangu wa damu Mtatiro,huyu jamaa alikuwaga zaidi ya ndugu,mambo yote muhimu nilikuwa nikimshirikisha na yeye pia alikuwaga akinishirikisha mambo yake,nilipokuwa nafeli aliumia sana kama ndugu kwasababu tulipendana sana!.
Basi niliamua kupambana na ile kazi ya uvuvi lakini ilifika mahali nikakata tamaa kutokana na kutopata malipo,niliendelea kusubiri uenda ningepewa ile kazi ya usimamizi kama nilivyokuwa nimeahidiwa lakini ikawa hola,niliamua kuwa mvumilivu maana ndani ya mwezi huo rafiki yangu Mtatiro yeye alianza kazi ya kuuza mitumba huko minadani lakini mimi nikamwambia ngoja kwanza nisikilizie hali itakavyokuwa.
Sasa nakumbuka siku moja nikiwa hapo ziwani nimepauka sina hili wala lile,simu ya Mtatiro iliita nami nikaipokea!.
Mtatiro "vp mwana?"
Mimi "Shwari mwanangu"
Mtatiro "Bado upo mwaloni?"
Mimi "Bado nakomaa mwanangu!"
Mtatiro "Mwanangu leo Gabriel amenipigia simu!"
Mimi "Acha utani mwanangu!"
Mtatiro "Kweli mwanangu kwanini nikutanie!"
Mimi "Duuu!,jamaa yupo uraiani?"
Mtatiro "Kwanza anakuulizia kinoma!"
Aliendelea "Nimemwambia uko Mwanza na anasema anakutafuta sana upatikani,nikamwambia Umughka alishabadili namba siku nyingi"
Mimi "Jamaa anasemaje sasa"
Mtatiro "Hatujapiga sana stori maana alikuwa anakuulizia sana,ila ameniambia anakuja Mwanza na amesema tufanye juu chini tuonane!"
Aliendelea "Mwanangu leo nipo hapa Katoro nilikuja kuleta mzigo ila jioni nageuka Mwanza!"
Mimi "Vipi kazi inalipa!"
Mtatiro "Watu wa huku wanavaa sana maspesho mwanangu,yaani najilaumu kuchukua hii mitumba!"
Aliendelea "Ila wapo wanaonunua tu kiaina!"
Aliendelea "Nikirudi jioni Mwanza nitakucheki"
Mtu niliyekuwa nikiunga bando napiga nae stori nyingi alikuwa ni mshikaji wangu Mtatiro pamoja na wanangu wa Tarime!.Kiukweli baada ya kuona mambo hapo mwaloni yanakuwa magumu niliamua kuondoka kurudi kwa sista ili nione la kufanya,sikutaka kuendelea kukaa sehemu ambayo nilikuwa nikifurahia kula samaki na ugali wakati mfukoni hakuna chochote,nilishazoea kushika hela kwa sana tu kwa wakati huo,kile kitendo cha shemeji kunifanyisha kazi ya uvuvi kwa takribani miezi mitatu pasipo malipo sikukiafiki hata kidogo.Nilipofika kwa sista sikutaka kumwambia kwamba mumewe alikuwa hanilipi ili kujiepusha na uchonganishi,nilifahamu uenda ningemwambia pengine angenihisi mimi ni mvivu tu ambaye sipendi kufanya kazi na nishazoea kuzurura!,hivyo nikaamua kupiga kimya!.
Nilipotoka kule mwaloni Magu niliondoka tu kama naelekea mjini Magu na ningerudi baadae lakini haikuwa hivyo,hakuna mtu niliyemuaga maana wao walidhani nafika tu mjini halafu ningerejea!.Sasa kuna muda shemeji alikuja pale nyumbani kutoka huko kwenye shughuli zake na akashangaa kuniona pale akidhani uenda muda ule ningekuwa mwaloni!.
Hiyo ilikuwa ni baada ya kupita siku 3 baada ya mimi kutoka huko!,jamaa alikuwa amechukia sana lakini nahisi alishindwa kuongea sababu ya mkewe,mimi ile hali niliiona na kwasababu nilikuwa mtu mzima niliamua kujiongeza ili kuepusha mambo mengi!.Haiwezekani nikufanyie kazi miezi yote hiyo ushindwe kunilipa halafu bado niendelee na kazi!,yeye alidhani mimi kwenda kwake ndiyo sasa aanze kunitumikisha kama punda,nilikuja kugundua kumbe hata lile suala la kumwambia sista kwamba kuna muhindi alikuwa akihitaji usimamizi kwenye mitumbwi yake zilikuwa ni fiksi tu,hakukuwa na muhindi wala bibi yake na mihindi!.
Nadhani mwanzo kama mtakumbuka nilisema ya kwamba,ninao ndugu kibao tu hapa mjini Dar es salaam lakini huwa nawapotezea kwasababu wengi wao wanajifanya matawi ya juu huku wakiwa na nyodo pamoja na dharau kibao!.,Huyo shemeji na dada yangu kwasasa wanaishi Dar es salaam lakini sijawahi kuthubutu kukaanyaga kwao kwasababu jamaa ana roho mbaya mno!,simsemi vibaya lakini hapendi ndugu wa mwanamke!,Maza mwenyewe alishakata miguu kuja kwa binti yake baada ya kuona hali ya jamaa anavyokuwa akitembelewa na ndugu wa mke!.Mimi nampenda sana jamaa kama navyowapenda watu wengine na namuheshimu lakini sitaki kabisa kujishobokesha,napambana tu kivyangu,nikiwaga nina shida za hapa na pale huwa nina wasiliana na sista basi inatosha!.
Basi baada ya kuona yale mazingira sitoyaweza,nilimwambia dada yangu kuna mahali nimeona nikajaribu maisha kwasababu yale maisha ya kisiwani yamenishinda!.Dada aliamini ni kweli maisha ya kule yamenishinda lakini kiukweli haikuwa hivyo!,niliamua nifunike kombe mwanaharamu apite!.
Kweli!,Dada yangu nakumbuka alinipatia shilingi laki moja na akaniambia nikiwa napata tatizo niwe namjulisha!.Nilimpigia mshikaji wangu Mtatiro akawa ameniambie nipande gari za kuelekea Usagara nitamkuta ananisubiri maeneo yale!.
Nilifanikiwa kufika na nikamkuta Mtatiro ambaye tuliongozana nae mpaka kwenye nyumba ya kaka yake aliyokuwa akiishi yeye na familia ya kaka yake tuliyemuacha Bunda akikomaa na madini!.Ile nyumba ilikuwa na braz ake aliyekuwa mwanajeshi wakati huo huko Kigoma!.
Siku nazo hazikuganda zikawa zinapepea kama upepo,sasa nakumbuka siku moja tukiwa katika mihangaiko mnadani kwenye kijiji kimoja kilichopo huko Geita kinachoitwa Nzera,nikapigiwa simu na mshikaji wangu Magesa ambaye aliniambia ya kwamba,yule mzee aliyekuwa akimiliki ile nyumba niliyokuwa nimepanga pale Sirari amekuwa akienda pale kijiweni kunitafuta bila mafanikio,sababu ya yeye kunitafuta ilikuwa ni kuhusu kodi yake ya nyumba,nilichofanya nilimwambia Magesa kama anaweza aende anihamishie vile vitu na ningevikuta kwake kwasababu yeye alikuwaga amejenga japo nyumba ilikuwa kama pagale tu maana kuna vyumba vingine vilikuwa havijaisha!.
Mimi "Mwanangu nitakutumia hela ya kubebea wewe nisaidie nitavikuta kwako!"
Magesa "Kwani huko ulipo utachukua muda mrefu?"
Mimi "Naweza kuchelewa kaka,ndiyo maana nakuomba unisaidie!"
Mimi "Unavyoweza kuvitumia wewe tumia kaka ilimradi visiaribike tu!"
Magesa "Sawa haina noma,we kama itawezekana nitumie hela ya usafiri nitavifata!"
Baada ya yale mazungumzo niliendelea kupiga mwano kuita wateja wa kununua mavazi pale mnadani!.
Sasa baada ya mwezi kukatika baada ya mimi kuanza kuifanya ile shughuli ya uuzaji wa mitumba huku mimi na Mtatiro tukiendelea kuzunguka katika minada mbalimbali huko vijijini,siku moja Gabriel alimpigia simu Mtatiro na akawa amesema inapaswa tuonane haraka!.
Kweli,baada ya kutoka kwenye mnada mmoja huko Sengerema tuliamua kesho yake hatutoenda mnadani bali tungeenda kumuona Gabriel.Kesho yake mida ya saa 4 asubuhi tuliondoka kuelekea Nyakato ambako Gabi alikuwa amemwambia Mtatiro tukifika hapo tumwambie!.
Tulipofika Mtatiro alimpigia simu Gabi akawa amemwambia tumefika hapo Nyakato,jamaa alimwambia tusubiri hapo kuna gari ilikuwa inakuja kutuchukua.
Hazikupita hata nusu kuna jamaa akawa amempigia simu Mtatiro akimuomba amuelekeze mahali tulipokuwa tumesimama ili asogee kutuchukua,baada ya maelekezo tukaona Gari land cruiser hard top la njano likiwa na vioo vyeusi likisimama na dereva akitufanyia ishara ya kutakiwa tupande tuondoke!.