Mwaka 2019 nilimpoteza mdogo wangu kwa ajali mbaya ya pikipiki. Si vema kukumbuka mambo haya maana yanaumiza sana, lakini tusipofanya hivyo, tutapata wapi pa kujifunza?
Pengine kifo kile cha mdogo wangu, muda mwingine huwa nawaza na kuamini, ndicho kilileta uhai wa fikra yangu na uzima wa macho yangu kuanza kutazama mambo kwa mboni tofauti.
Lakini kifo kile - katika mfululizo huu wa vifo nitakaokupatia hapa - naamini ndicho kilikuwa kifo cha kikatili zaidi mimi binafsi kupata kukisikia ama kukishuhudia hata sasa.
Nakumbuka siku ile, kitu pekee kilichonifanya nikatambua kuwa huu ni mwili wa mdogo wangu pale mochwari, hospitali, ilikuwa ni mabaki ya nguo na vidole vyake vya miguuni, tena mguu mmoja wa kulia pekee, ila kwengine kote kulikuwa ni nyama nyama tu, tena zisizotosha kutambua hata jinsia ya marehemu.
Hali kweli .... sisi binadamu ni kitu gani? Nilijiuliza na nafsi yangu siku ile. Yapi ni majivuno na majigambo mbele za wengine ilhali muda wowote tunaweza kufa tena kama mnyama tu wa mwituni? Nyama yako ikabanduliwa chini kuwekwa kwenye mfuko wa nailoni?
Walakini, ya msiba ule, mimi sitakaa kitako nikayasahau. Nayakumbuka vema sana kana kwamba msiba umejiri asubuhi ya leo hii.
MOSI, namna nilivyopatwa na uchungu kwa kumpoteza ndugu yangu wa damu lakini pia kwa kumpoteza msaidizi wangu mkubwa wa pale nyumbani, msaidizi ambaye nilimbembeleza sana mama yangu kule nyumbani kijijini anipatie kuja kunisaidia huku mjini kazi ndogondogo kwasababu ya hali nilokuwa nayo; ujauzito wa miezi michache na mtoto mdogo wa kiume aliyekuwa anasoma darasa la tatu.
Kwani,
Kipindi hiko, kule shuleni nilipokuwa nafanyia kazi, kwa bahati mbaya, nilihamishiwa darasa la mtihani; darasa la saba, hivyo majukumu yangu ya kazi yalipandiana na muda wangu wa kudumu kazini uliongezeka maradufu. Darasa hilo zima lilikuwa likiishi bweni; wanaanza vipindi saa kumi na mbili asubuhi mpaka kukoma kwake saa moja usiku. Hapo hujaandika na kutoa ripoti kwa mtaaluma, hujaachia pia wanafunzi kazi ya kufanya majira ya usiku, na hiyo ni lazima.
Kwasababu hiyo,
Japo nilikuwa nafundisha shule moja na alokuwa anasoma mwanangu, niliona ni stara sasa kumwachia awe anarejea nyumbani mapema kama wenzake.
Kumkalisha shuleni kama nilivyokuwa nafanya hapo awali kisha narejea naye nyumbani kwa pamoja sasa haikuwa inawezekana.
Nilijaribu kufanya mwanzoni nikaona namchosha mno, hapo ndo' nikaona umuhimu wa kuwa na mtu nyumbani, mtu wa kumkarimu mtoto na kuhudumia nyumba muda mwingi ambao mimi sipo, mathalani usafi wa mazingira, kupika, kufua na kadhalika. Mtu ambaye atayajua majukumu na kuyazoea kabla sijaanza kuchoshwa na ujauzito nilokuwa nao.
Kwasababu mimi sikuwa mpenzi sana wa kutumia 'housegirls', kwanza sikuwahi hata kuwatumia maana majukumu yangu nilikuwa nayamudu vema - naamka asubuhi na kumwandalia mume wangu na mtoto chakula cha asubuhi kisha bwana anaenda zake kwenye shughuli zake na mimi naongozana na mtoto shuleni, majira ya alasiri nisharejea na mtoto nyumbani naandaa chakula cha usiku kwaajili ya familia, kila kitu kinakuwa sawa sawia - lakini kwa muda huo sasa mimi sikuwa tena na ujanja, ratiba zinanibana na mwili unachoka mno, nikaona nimrejee mdogo wangu, Sarah, ambaye alikuwa amehitimu kidato cha nne na bado hajajipata ashughulike na nini hapo mbeleni.
Nilifanya hivyo kwa kuamini yeye atakuwa ni bora kuliko kumchukua mtu baki nisiyejua alipotokea wala namna alivyolelewa alafu kuja kumtwika majukumu yangu ya familia. Na kweli, mnyonge tukimpa haki yake, mdogo wangu aliyatwaa na kuyamudu vema majukumu ya pale nyumbani. Hili nisimnyime haki yake.
Lakini PILI, msiba ule uliniacha kwenye hali mbaya ya manung'uniko na majuto ndani yangu. Nikikaa na kuwaza, vipi kama nimgemwacha binti yule kule nyumbani kijijini? Haya yote yasingemkuta na hata mimi yale yasingenikuta. Huenda muda huu angekuwa hai akifanya kazi za nyumbani ama shambani, ama angekuwa anayajenga yeye na mama yake, kwenye vigoda vya jikoni, wakipeana hadithi na michapo ya vijijini.
Mimi kumleta huku mjini ndo' nimejiletea matatizo na kumpalilia kifo, nilijiwazia nikaumia. Tena nilimbembeleza sana yeye na mama, kumbe maskini ya Mungu najibembelezea mwenyewe tabu na nambembeleza yeye aje afie mikononi mwangu. Sasa hata ndugu zangu hawataninyooshea kidole ama kunitazama na macho ya hukumu? Sikujua, ila mimi nilijihukumu hivyo. Niliteseka na mawazo hayo, hata kama kweli hawakuniwazia vile mimi nilivyofikiria.
Yamkini nakumbuka baadhi ya majirani zangu waliwahi kuninyooshea vidole wakisema huenda mimi nilikuwa namtemdea vibaya Sarah enzi za uhai wake kwani alikuwa na makovu kadha wa kadha katika mwili wake, makovu waliyoamini yametokana na kipigo cha mikono yangu, pasipo kujua ya kwamba Sarah alikuwa akisumbuliwa na kifafa tangu utotoni.
Ugonjwa huo ulimsababishia kadhia sana kabla ya angalau kuja kupata afueni baada ya matumizi mazuri ya dawa, dawa ambazo hakutakiwa kuziacha kuzitumia kamwe kwaajili ya usalama wake. Dawa hizo zikamfanya Sarah asahau kabisa kuhusu mambo ya kuanguka chini na kukakamaa. Alikuwa mzima kama mimi na wewe.
Ni mara kadhaa, tena akiwa huko kijijini, ndo' alishawahi kuzembea na dawa akakumbushwa na kifafa kikali basi akarejea mwenyewe kwenye mstari, lakini tayari mwili ukiwa ushaachwa na alama na viraka vya majeraha.
Huku mjini, mimi mwenyewe, kwa nafasi yangu, nilikuwa najitahidi kwa kadiri ya nilivyopata muda kumsisitiza kumeza dawa na kweli alikuwa anafanya hivyo kiasi kwamba tulisahau kabisa kama anaumwa. Hata kama ungekaa naye mwaka, usingebaini kitu labda tu akusimulie mikasa ya makovu yake mwilini.
Ndo' maana,
Nilistaajabu sana kuja kusikia maneno ya dereva bodaboda aliyembeba siku ile ya ajali akieleza namna tukio lile la kutisha lilivyotokea.
Dereva huyo, almanusura wa ajali, alikuwa amelazwa Mwananyamala, mguu na mkono wake umepata hitilafu, mbali na hivyo alikuwa na michubuko tu ya hapa na pale na majeraha yanayovumilika. Alikuwa anaweza kuongea na kumtambua mtu vema pasipo shida.
Kwa maelezo ya dereva huyo, nilipomsikiliza mwanzo mpaka tone la mwisho, nilibaini Sarah alishikwa na degedege (kifafa) wakiwa barabara kuu, hali hiyo ikapelekea chombo kuyumba na hata yeye kuangukia barabarani ambapo gari mbili, dogo na fuso, zilimgonga na kumkanyaga vibaya.
Nikapata maswali, ina maana Sarah aliacha kutumia dawa? Mbona nilikuwa nikizingatia sana hili? Lakini kwanini alipanda usafiri huo ingali hali yake anaijua, kwanini alihatarisha uhai wake kiasi hiko?
Ila zaidi, alikuwa anaelekea wapi? Mbona mimi sikuwahi kumtuma popote pale mbali na nyumbani kiasi cha kupanda bodaboda na hata kushika njia kuu?
Dereva yule aliniambia, "sister, aliniagiza nimpeleke Magomeni lakini hakuweka wazi Magomeni sehemu gani. Yeye alisema atanielekeza tukifika huko."
Kunani huko Magomeni? Nikajiuliza. Na kwanini hakuniaga na hiyo safari?
Labda ningelijua majibu ya maswali hayo ni kile nilichokuja kukifahamu hapo baadae, huenda mimi nisingelithubutu kabisa kujiuliza ....
Na huenda watu wangeyajua hayo, basi wangesema bila hiyana kuwa mimi ndo' nimemuua mdogo wangu. Ila mpaka haya yanatokea na mwili wa mdogo wangu unaingia ardhini na kufukiwa, ni mume wangu, 'kijana mmoja' na kuta za nyumba yangu, ndivyo vitu pekee vilivyokuwa na huo ufahamu.
'Kijana' huyo, ndo' TATU ya msiba huu ...
Lakini pia kijana huyo ndiye MOJA ya vifo vitano vilivyotokea ikiwemo kifo cha kikatili cha mdogo wangu, Sarah, na vinginewe vinne kwa kila moja na kisa chake, mimi nikiwa katikati ya visa vyote hivyo.
Kijana Amiri alijua kunipakaza damu ya wenye hatia na wasohatia katika viganja vyangu.
Na haya ni maisha yangu. Sina tofauti na binadamu wengine. Sisi sio malaika na hivyo basi nina pande mbili za shilingi; mabaya kwa mazuri pia. Hivyo kama wewe ni msafi tu, umeishi mpaka sasa pasipo doa lolote lile, basi karibu uwe wa kwanza kuokota jiwe na kunirushia ...
Mbali na hivyo,
Ngoja nikueleze sasa, ni wapi mambo haya yalipoanzia mpaka kukomea kwenye makaburi matano niliyopamba kwa shada za maua ...