Sehemu ya Pili:
Binafsi sijawahi kukaa kuwa mama wa nyumbani, hata mume wangu yule, bwana Mgaya, niliyeishi naye miaka kadhaa na kupata naye mtoto wa kiume, nilimpatia katika eneo langu la kazi; shule yangu ya kwanza kufundisha kabla ya kuja kuhama kutafuta shule nyingine.
Nikiwa huko, nilimwona bwana huyu, siku ya kwanza kabisa, akiwa amekuja na bajaji kumchukua mwanafunzi wa darasa langu. Bwana huyo alinisalimu kisha akaniulizia mtoto huyo alokuja kumfuata, baada ya hapo akaondoka zake, yeye pamoja na mtoto.
Kuja kwake hapo shuleni mara kwa mara ndo' kukanifanya nizoane naye kiasi kwamba nilichukua namba yake nikawa nautumia usafiri wake pale nilipokuwa na mahitaji.
Nilizoeana naye, nikazoeana naye tena, hatimaye akaja kuwa mpenzi wangu baada ya miezi kadhaa, miezi michache tu tangu nilipoachana na mpenzi wangu wa nyuma, bwana Anwari, baada ya kumfumania na mwanamke mwingine nyumbani kwake, mwanamke ambaye hakuweza kunipa maelezo ya kueleweka alikuwa ni nani yake na pale nyumbani kwake alikuwa anafanya nini.
Kama waswahuli wasemavyo; vita ya panzi furaha kwa kunguru, ndivyo kunguru huyu, yaani bwana Mgaya, alivyofaidika na kadhia ile ya mimi na Anwari, akajiweka katikati yetu.
Sikupata hata muda wa kuwaza, muda wa kujitafakari na kujipanga, hasira na maumivu yangu yalinitia upofu nikatafuta afueni ya harakaharaka kuponyesha majeraha yangu, afueni huyo ndo' ikawa kuangukia kwenye mikono ya dereva yule wa bajaji.
Naye dereva huyo, asifanye ajizi, akayapeleka mambo upesiupesi nikajikuta kwenye ndoa, yani kama kufumba na kufumbua, yani kama hadithi fulani yenye mtiririko wa upesi sana, nami nikienda nayo tu kama mlemavu, nashuka nayo mithili ya gari bovu kwenye korongo kali.
Nami sikujali,
Kitu pekee nilichokuwa nacho moyoni, ni kumwonyesha Anwari kuwa embe aliloona lina funza akalitupa, mwingine kaliokota akaliweka kapuni.
Nini raha kama kumrusha roho 'ex' wako? Tena sio kwa tambo za mpenzi mpya, la hasha, bali tambo za mume kabisa wa ndoa, na picha nikiwa ndani ya gauni jeupe linalometameta na pete ya ndoa ipo kidoleni?
Hakuna!
Kweli nilihisi raha sana, tena raha iliyokufuru pale shoga yangu, Zai, alipokuwa ananipa taarifa za Anwari. Nami nilikuwa nikifanya hila kumwambia Zai kila jambo lililokuwa linaendelea kwani nilijua fika atayafikisha kama yalivyo kwenye masikio ama macho ya Anwari maana alikuwa amezoeana naye sana na pia anawasiliana naye huko mitandaoni.
Nami nilitaka Anwari ajue. Nilimtaka aumie kama mimi nilivyoumia au kama inawezekana basi iwe maradufu ya yale maumivu yangu.
Basi furaha yangu ya kwanza nikaja kuipata pale Zai aliponambia namna Anwari alivyoupokea ujumbe ya kwamba mimi nipo kwenye mikakati ya kuolewa.
Kwa maneno ya Zai, Anwari alilalamika sana kunipoteza. Alijilaumu na kujitusi. Alimwambia Zai namna mimi nilivyompenda lakini hatimaye akanilipa maumivu. Lakini zaidi lililonifanya nikaamini Anwari alikuwa ameumia, ni namna alivyoapa kwa Zai kuwa mimi sitakuja kuolewa na mwanamume mwingine isipokuwa yeye. Hapa nikacheka mpaka gego la mwisho.
Moyoni mwangu nikisema "huo ndo' kwanza mwanzo, funga mkanda, Anwari. Mengi yanakuja."
Furaha ya pili, ikawa ni pale nilipofikisha kadi ya mwaliko kwenye mikono ya Zai, kadi mbili kwa idadi, moja nikiandika jina la rafiki yangu huyo na pili nikiandika jina la Anwari, tena majina yake yote matatu.
Nikamwambia Zai, sikutaka bwana huyu anichangie harusi yangu lakini hili la kuhudhuria halina tabu, anakaribishwa kuniona katika siku ya furaha yangu, Zai akanambia si vizuri vile nilivyokuwa nafanya lakini mimi hakuna nilichokuwa najali isipokuwa jambo moja tu, nalo ni kumuumiza Anwari pekee!
Niliamini kadi ile itakuwa ni ujumbe tosha kuwa kweli nilimaanisha. Na kweli Zai alipompatia taarifa ile alipapatika, hakuamini macho yake, alidhania utani lakini ilikuwa kweli mimi nilikuwa naolewa.
Mara kadhaa ningekuta ujumbe wake katika simu yangu ama 'missed calls' wala nisihangaike kujibu. Mwisho wa siku nilimtumie ujumbe:
"Usije ukaniharibia ndoa yangu." Alafu nikam-block asinipate kabisa hewani. Kama haitoshi, nilibadili kabisa namba yangu tena nikimwonya Zai asije akampatia, yeye kazi yake awe ananisikia kwa mbali maisha yangu yakipepea bila yeye.
Furaha yangu ya tatu ikawa ni siku ile ya harusi, nilipopepeza macho kuangaza ukumbini kama nitamwona Anwari. Sikumwona. Nikatabasamu na moyo wangu nikijua kabisa huko aliko, hata kama hajaja pale, atakuwa anajua fika kuwa siku hiyo nafunga pingu za maisha na mwanaume mwingine, mwanaume aliyethamini pendo langu akanisitiri.
Hilo kwangu lilikuwa ni faraja tosha, achilia mbali kujumuika pamoja na familia, marafiki, ndugu na jamaa zangu katika ukumbi ule kwasababu ya sherehe yangu. Niliamini picha ya yale yote yalojiri ingemfikia Anwari, na kweli sikukosea hata chembe, nilikuja kubaini hilo baadae hapo mbeleni.
Lakini furaha yangu hiyo, nasikitika, ilikuwa ni mbio za sakafuni, haikupata kudumu bali kuja kuishia ukingoni muda si mrefu tangu nilipoingia ndani ya ndoa na kuishi na bwana Mgaya.
'Hangover' yangu ya maumivu yaliyosababishwa na Anwari ilikuja kukoma na sasa nikaanza kuuonja uhalisia mchungu ambao niliupika kwa mikono yangu mwenyewe, uhalisia ya kwamba bwana yule hakuwa moyoni mwangu kabisa bali ni maamuzi yangu ya pupa nilofanya baada ya kuumizwa.
Lakini sikuwa na budi tena, nilimwonyesha mapenzi yangu bwana Mgaya kwa kadiri nilivyoweza, naigiza na kutenda, nikiamini hapo mbeleni nitakuja kuyasahau ya nyuma na yeye ataniingia moyoni mwangu mzima mzima.
Hatimaye siku, miezi na mwaka ukapita.
Mimi na bwana Mgaya tukaona sasa ni muda muafaka wa kupata mtoto baada ya mipango yetu kadhaa ya maisha kwenda sawa.
Bwana huyo aliachana na kuendesha bajaji, sasa akawa anaendesha gari za kampuni zinazopokea wageni pale uwanja wa ndege, kwa kipato chake pamoja na changu, tukapandisha jengo katika 'site' fulani, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam, tukahamia huko pasi na kujali ujenzi haukuwa umekamilika.
Kwani
Tulijiskia fahari kuishi mahali tulipopaita nyumbani kwetu, hayo mengine yalikuwa ni ziada tu.
Eneo lile lilikuwa ni kubwa na tulivu, lina nyasi na miti mingi. Mume wangu, bwana Mgaya, aliniambia alilipata eneo lile zamani kidogo kwa pesa ya kutupa, na alivutiwa na eneo hilo kwasababu ya ndoto yake ya mbeleni ni kuja kuwa na mifugo kadhaa.
Tulikaa hapo huku ujenzi ukiwa unaendelea taratibu taratibu mpaka nyumba kukamilika kabisa: nyumba ya vyumba vinne na uzio wetu wa michongoma.
Maisha ya huko, changamoto yake ikawa ni umbali wa mimi kufika kazini, mara kadhaa mume wangu angenipeleka na gari yake ya kazi lakini mara nyingi pia asingeweza kwasababu alikuwa anashinda usiku huko kwa kazi zake za kule kiwanjani.
Hapa sasa ndo' nikaona kuna haja ya kuhama mazingira ya kazi, taratibu nikaanza kutafuta shule mbadala huku na kule katika maeno ya karibu, nikaja kupata mahali fulani, karibu kweli, lakini maslahi yake hayakuwa mazuri, nikaendelea kutafuta huku napambana na kule nilipo, bahati nikaja kupata shule, japo haikuwa karibu kama nilivyokuwa nimepanga mimi ila ilikuwa angalau ukilinganisha na ile ya mwanzo.
Nikiwa katika shule hiyo sasa, ndo' nikapata ujauzito wangu wa kwanza, ujauzito wa mtoto yule wa kiume. Ujauzito huo ukanikutanisha uso kwa uso na mama yake Mgaya, yaani mama mkwe wangu, kwa ukaribu wa zaidi, sio ule wa kupigiana simu kujuliana hali bali sasa wa kuishi nyumba moja, tunakaa sebuleni na tunapishana koridoni.
Mama huyo alikuja nyumbani kunihudumia kwasababu ya ujauzito nilokuwa nao ulikuwa unaelekea ukingoni, muda si mrefu ningejifungua, na hakukuwa na mtu wa karibu kuniangaliza.
Lakini maisha yale na mwanamke yule, chini ya paa moja, yalikuwa magumu sana. Maisha ya kikoloni na kusontwa kila mara, aidha kwa hiki ama kile. Yalikuwa ni maisha ya maigizo mbele ya mume wangu lakini nyuma ya mlango nalia na ya kwangu. Niliogopa kama ningemshirikisha mume wangu kwenye visa vile, angedhania simpemdi mama yake na mimi sikutaka niwe nyundo ya kuvunjia familia yao.
Nilikaa nikaamini labda ile ni mimba tu, Zai pia alikuwa akinishauri hivyo, punde nitakapojifungua naweza nikayaona mambo kwa namna tofauti.
Basi nikayabeba.
Nikaja kujifungua salama, nashukuru Mungu, lakini ajabu chuki yangu kwa yule mama haikwenda popote pale, iliendelea kuniganda kama nzi anayemendea kidonda kichafu, lakini nikapiga moyo konde, mathalan nimejifungua, mama yule asingekaa muda mrefu pale atarudi nyumbani kwake.
Nikavumilia amri na shurba zake, nkihesabu siku na majuma. Nayo nayaona hayasogei, yanajivuta mno. Mpaka mtoto wangu kuja kufikia hatua ya kumsimamia mimi mwenyewe kiukamilifu, hakuna rangi niliyoacha kuona. Hamna jambo lilikuwa jema kwake akaniacha nikahema.
Nilishawaza hata mara mbili, kama ningekuwa na uwezo, ningemtokomeza mama yule nirejee kwenye amani.
Amani ya moyo.
Nilimwona ananikosea sana na anastahili adhabu. Si bure, alikuja kuwa mtu wa kwanza kumzika na kuweka shada langu juu ya kifusi cha kaburi lake. Uso wangu ukiigiza huzuni mbele za watu, huku moyo unapondeka kwa furaha.
Furaha kuu.
**