Niliweka shada za maua kwenye makaburi matano ya watu wangu wa karibu

Sehemu ya Kumi na Mbili:


Yule alikuwa wa pili katika orodha.

Orodha hii ya vifo vitano, kila kifo na mkasa wake.

Nilivyopokea habari ya msiba wa Anwari, sasa ikanibidi nisitishe habari za kwenda kuonana na Zai kwaajili ya tiba yake kule kwa mama Miraji.

Nilichokifanya nilipiga simu kwa mama Miraji nikampa taarifa ya udhuru, sasa taarifa hii ikiwa ni ya pili kwa udhuru, kila tukiyapanga, mambo yanatibuka, mambo yanaibukia kasi ama kusi, yakiambatana na mawimbi yake.

Mama yule aliniambia basi hakuna tabu, tufanye tu siku nyingine lakini ni mpaka atakaponiambia maana ana safari karibuni akienda kwao Mtwara, mimi nikaona kheri.

Baada ya hapo, nilimtafuta Zai pia naye nikampa taarifa ya msiba, kweli akapokea taarifa hiyo kwa uchungu mrefu na mpana, akauliza ana nini ana nini, mbona kuandamwa na taarifa mbaya kila kukuchwa kwa jua?

Aliumia sana, Anwari kwake alikuwa zaidi ya shemeji tu, alikuwa ni mtu anayemkirimu na changamoto zake kila anapomuhitaji, hivyo kumpoteza haikuwa kama jani kuning'inia mtini tu, bali pengo kubwa lililoachwa kinywani kwa kuondolewa jino muhimu.

Nilimpa habari tukutane sehemu fulani ili tuongozane kwenda msibani, akaridhia, japo kwa kwikwi nyingi na mafua mepesi ya kilio, nilipomalizana naye nikaenda ofisini kutoa taarifa ya msiba huo, nikiomba udhuru wa siku kama mbili hivi kuhani na kukirimu msiba wa mtu wangu wa karibu.

Kwasababu ya urahisi, kukwepa maelezo mengi na taratibu lumbesa za kiofisi, nilienda moja kwa moja kuonana na meneja Salum.

Nilijua jambo hilo lingeleta utata kwa mkuu wa shule lakini kweli sikujali, mimi nilitaka kutimiza adhma ya kuharakisha shughuli yangu tu, hayo yaliyo kwenye makapu mengine sikuyatilia maanani wala sikutaka hata kuyachungulia.

Nilibisha hodi mara moja mbele ya mlango wa mkurugenzi kabla ya kuingia na kuwa na maongezi naye mafupi.

Nilimweleza haja yangu, haja ilonileta pale, naye akanieleza haja yake akinikumbushia mambo ambayo alinieleza kwenye makutano yetu ya mwisho.

Alisema, "mimi sina shida na hilo madam Magreth, take your time, shida mimi nilonayo unaifahamu na bado nangojea utatuzi wake."

Nikamwambia haina tabu, ngoja kwanza nikabiliane na hili lililopo mbele yangu kisha tutayaganga yanayokuja.

Hivyo tu, nikaondoka zangu kukutana na Zai kisha kiguu na njia mpaka nyumbani kwa Anwari. Huko tulikutana watu baadhi, watu wa karibu na bwana huyo marehemu, hawazidi kumi kwa idadi, wakatueleza yanayojiri na yalokwishajiri.

Mosi, mwili wa Anwari ulikuwa tayari hospitalini kwaajili ya hifadhi, pili, ratiba ya msiba katika siku hizo za maombolezo pale nyumbani, tatu, siku wanayoenda kuupumzisha mwili na utaratibu wake.

Mimi na bwana Adrian tulisonga kando kwaajili ya kupeana mawili matatu, ilinipasa kujongea huko na Zai lakini hali yake haikuwa nzuri, tangu nilipokutana naye na zaidi tulipofika eneo la msibani, hakuwa kwenye mandhari njema kabisa, alikuwa anahema juu juu akidai pia anaishiwa na nguvu mwilini.

Yote hayo ni sababu ya ugonjwa wake unaomsibu, ugonjwa wa presha ya kupanda ulopeleka moyo wake kutanuka.

Adrian alinieleza namna alivyomkuta Anwari pale nyumbani baada ya kumtafuta mara kadhaa kwenye simu pasipo kuzaa matunda.

Alipomkosa ndipo akatia shaka, shaka kwasababu ya yale yalotukia vile karibuni, na kwavile alikuwa akikatiza maeneo ambayo si mbali sana na makazi ya Anwari basi akaona ni vema sana apitie hapo kumjulia hali bwana huyo.

Kufika kuhamaki,

Pale sebuleni, juu ya makochi, bwana Anwari alikuwa amelala mfu. Mwili wake hausemi, mwili wake hausogei.

Mwili wake umedaka na kushika baridi, baridi la kifo.

Mkononi sindano iliyotoboa mwili wake inaning'inia. Sindano iliyomnyang'anya pumzi yake.

Alinambia baada ya siku ile, mimi na yeye kumkuta Anwari akiwa hajitambui sababu ya kujidunga madawa mwilini, aliweka nadhiri na bwana huyo, kule hospitalini, ya kwamba hatokaa akarejea tena kwenye ule uraibu.

Uraibu huo unamtesa.

Atatafuta namna nyingine ya kukabiliana na msongo wa mawazo na changamoto zake za maisha mbali na kuweka kemikali haribifu mwilini.

Kemikali ambazo zinampa ahueni ya masaa tu kisha anarejea tena, mikono nyuma, katika dimbwi lake la matatizo.

Lakini bado ... bado hakushinda pambano hilo.

Adrian aliniuliza kama nafahamu chochote kile kilichokuwa kinamsumbua Anwari kipindi hiko kifupi kabla ya umauti wake, mimi nikaapa sijui, kwanza sikuwa nawasiliana naye mara kwa mara tangu tuyavunje mahusiano yetu zama za pontio pilato.

Siku ile kunikuta pale nyumbani kwake ni kwasababu ya Zai tu, si kingine. Nilimwambia ni muda mrefu sana ulipita bila kuonana na bwana huyo.

Uongo uongo mtupu ...

Nayasema hayo lakini ndani yangu najua kweli yote na kweli hiyo inanisuta kifuani mwangu.

Lakini nifanyaje sasa? Ebu sema.

Nimwambie Adrian kuwa mimi ni miongoni mwa watu walomtia Anwari msongo wa mawazo kwa kumnyima kumwona mwanae?

Nani anataka kadhia hiyo? Anwari inabidi aende na siri hiyo kwenye kifua chake.

Kifua cha marehemu.

Kifua hicho hakihemi wala hakitoi maneno, nami nitabaki kuwa salama na familia yangu. Familia ambayo furaha yake imeanza kumea kwa mbolea ya kifo cha Mama mkwe.

Basi baada ya maongezi hayo na Adrian, tulirejea kuungana na wengine katika sakafu ya msiba, hapo tulikaa mpaka majira fulani ya jioni ndipo tukaondoka baada ya kushughulika na kukamilisha kila kitu pale msibani ikiwamo pia kupika chakula.

Keshokutwa yake, mapema tu, mwili wa Anwari ulifika pale nyumbani kwaajili ya kumuaga, siku hiyo watu walikuwa lukuki ukilinganisha na siku zingine, na siku hiyo, naikumbuka vema kabisa, mimi kuja kuisahau itaniwia ugumu kweli, nilikumbwa na matukio mawili matata, kila tukio na kijimambo chake.

Siku hiyo, Zai alizirai kama mara tatu hivi, yani kuona jeneza tu linaingia akazirai, kuona tena mwili kwenye kuaga, akazirai. Kuona jeneza linashuka ardhini, puh, akazirai tena.

Yani nilipata taabu kwelikweli maana niligeuka kuwa mtumishi wa msalaba mwekundu pale msibani, kuokota mtu na kupepea, kuokota mtu na kupepea.

Sijasahau siku ile,

Ndo' ilikuwa siku yangu niloweka shada langu la maua juu ya kaburi la Anwari, shada lililoandikwa kwa maneno makubwa meupe: RAFIKI.

Shada hilo nililiweka nikiongozana na watu kama wanne hivi, nao wakiwa wamebebelea ya kwao.

Lakini kubwa zaidi siku ile, mimi Magreth, nilijikuta napatwa na jaka kubwa la roho pale ndugu yake na Anwari aliposimama mbele ya waombolezaji kusoma wasifu ule wa marehemu.

Mimi sikuwa na shida na elimu ya Anwari, elimu iliyosomwa kwenye wasifu wake, wala sikuwa na shida na kazi yake aliyokufa huku akiifanya wala historia ya maisha yake aloyaishi, mimi nilishtuka tu pale msomaji aliposema marehemu Anwari ameacha mtoto mmoja wa kiume, tena mtoto huyo akitajwa na umri wake ambao unawiana vema na wa mwanangu.

Nikajiuliza haya ni masikio yangu ama ya jirani kaniazima tu kwa muda? Nilichosikia nimesikia ama nimeshikia? Sikuelewa.

Tokea hapo akili yangu ikawa kama imeacha mwili hivi, nipo hapo kwenye msiba kama kivuli, kichwani kuna mtafaruku wa mawazo na marejelea.

Baadae nilimuuliza Zai, tukiwa tunarejea kutoka maeneo ya mazishi, yule mtoto wa Anwari aliyetajwa pale kwenye wasifu anamfahamu? Zai akanambia hamjui, nami nikaona nisimsumbue sana maana hakuwa katika hali nzuri, ila mimi ndani yangu nilikosa raha kweli.

Nilienda nyumbani na niliishi na mawazo hayo siku nzima, kuna muda nilikuwa napata maruweruwe kabisa nahisi kuna watu wanabisha hodi lakini nikitazama simwoni mtu.

Bwana Mgaya alinikuta katika hali hiyo, hali ya sintofahamu, akahisi nipo katika maombolezo ya kumpoteza rafiki, akae asijue namwaza baba wa mtoto tuliye naye ndani.

Mambo mengine ni kheri yakabakia kizani milele, inabidi yawe hivyo kama gharama ya kudumisha amani. Si kila kitu cha kufahamu, Mgaya, na sijali nitatembea kilomita ngapi kukufanya usijue hili, mimi niko radhi na moyo wangu wote.

Basi usiku huo, nilimpigia Zai kumuuliza hali yake, aliponieleza nikamuuliza tena kuhusu mtoto yule, yule aliyetajwa kwenye wasifu, je, amjua? Zai akakataa kwa mara nyingine, hamjui mtoto huyo, ila hapa akaniuliza mbona nataka sana kufahamu hilo, sikumjibu cha maana tukahitimisha maongezi yetu.

Siku iliyofuata niliripoti kazini kama kawaida, lakini kabla sijaanza majukumu yangu, mwalimu mkuu alinita ofisini kwake, kwenda ananiuliza nilikuwa wapi siku zile za kazi na ingali sikupata ruhusa?

Nilipomwambia meneja alinipatia ruhusa hiyo nikawa nimetia chumvi kwenye jeraha bichi, aliniwakia na kunimwagia maneno kweli kweli kiasi kwamba nikashangaa, katika maneno yote hayo, hili nililishika zaidi.

Alinambia: "nitakuonyesha kati yako na mimi nani alimkuta mwenziwe hapa, na n'takuonyesha nani ni mkuu wa shule hapa!"

Mie baada ya kushindiliwa maneno hayo nikaenda zangu, wala sikurudisha hata nukta, nikaendelea na majukumu yangu mpaka jioni nilipofunga na kurejea nyumbani pamoja na mwanangu.

Kesho ama keshokutwa yake, Zai alinipigia simu kunambia ana shida ya kuonana na mimi, shida ya dharura, kama nikipata muda basi nifanye kuonana naye kesho yake baada ya kutoka kazini.

Kweli nikafanya hivyo, nilimtafuta mara moja baada ya kumaliza kazi zangu, tukakutana mgahawa fulani ambapo mimi nilisimamia kila kitu kwasababu hali ya Zai kiukweli haikuwa nzuri, sio tu kiafya bali pia kifedha.

Pesa zake za akiba alikuwa amezimaliza kwenye matibabu alafu kurudi kazini anafukuzwa, na mpaka muda huo tunakutana, hakuwa amepata ajira popote pale, bado alikuwa anabangaiza.

Hata kula yake tu ilikuwa mushkeli.

Siku hiyo tuliongea mambo kadhaa, yote muhimu, kuanzia utafutaji wake wa ajira akinisihi nimsaidie kutafuta fursa, pia hali yake ya afya ilivyokuwa muda huo, na vilevile habari za ndugu yake kule anapoishi mpaka kufikia kwenye kitovu cha wito wake ambao ulimsukuma yeye kuniita pale.

Alinambia, siku hiyo mapema asubuhi, mama yake Anwari alimpigia simu akimtaka waonane mahali fulani siku za usoni kwani ana mambo machache wanataka kuzungumza.

Hajui mama huyo alitoa wapi namba yake na kwanini amemtafuta lakini yeye anahisi jambo hilo ni muhimu kunishirikisha, na swala lililomfanya akahisi kuna ulazima huo ni kitendo cha mama huyo kumwambia swala lake hilo ni nyeti sana na endapo akimsaidia basi bila hiyana atamkabidhi donge nono la pesa.

Sasa swala hilo ni lipi? Linamhusu vipi marehemu Anwari? Na lina mahusiano gani na yeye? Hapo hakutambua.

Mimi aliponieleza hayo, moja kwa moja kichwani mwangu nilona sasa ni muda mwafaka wa kumsogeza Zai karibu zaidi na mimi.

Nilianza kuamini umbali wetu unaweza geuka kuwa silaha ya kuangamiza uhai wa familia yangu, kwahiyo basi nillitumia mwamvuli wa ugonjwa wake, ukata unaomkumba kwa muda huo na hitilafu iliyopo baina yake na ndugu yake kumshawishi kuja kwenye makazi yangu na swala hilo likafaulu vema.

Kuhusu habari ya kumweleza mume wangu, bwana Mgaya, kamwe haikuwahi kunipa shida, upendo wake na uaminifu wake kwangu ulikuwa ni nyenzo yangu muhimu, na mimi niliitumia ipasavyo kwenye kukamilisha lengo langu.

Kwahiyo,

Siku ya siku Zai akahamia nyumbani kwangu, chumba chake kilekile alichokuwa analalia mama mkwe wangu, chumba cha wageni.

Hivyo,

Mimi nikawa nimenasa kwenye mtego wake wa uongo na unafiki, na yeye akajikuta amenasa kwenye kwenye mtego wangu wa kifo.

Kifo kile cha Zai kikiwa ndo' kifo kilichoniweka matatani zaidi kuliko vifo vingine vyote.

Kama vidole na macho vingekuwa vinaua basi nisingeishi kuja kuhadithia kisa hiki hapa.


****
 
Ya motoooo
Mkuje kabla haijapoa

Cc dega binti kiziwi Shunie Dr Restart Numbisa Half american Analyse
Gily charrote Darlin
Angel Nylon Amehlo
 
[emoji91][emoji91]
 
Anokumbuka Ahadi ya mkurugenzi na mage anikumbushe iloongelewa kwenye part hii
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…