Niliweka shada za maua kwenye makaburi matano ya watu wangu wa karibu

Niliweka shada za maua kwenye makaburi matano ya watu wangu wa karibu

Nimechukia Anwari kufa kwa madawa.

Nilitamani Mage amuue kwa mikono yake mwenyewe kama Mama Mgaya kwa nguvu za Amiri wa Amiri
 
Sehemu ya 11:


Nilifanya namna ya usafiri mpaka kufika kwenye makazi ya Anwari, huko nilikuta geti lake limefungwa na hata nilipobisha hodi kiasi chote kile, hadi kuokota jiwe na kugonga chuma la geti, hakuna mtu aliyekuja kunifungulia kamwe, sasa nikawa nimekwama hapo, sina la kufanya.

Nilichungulia getini kwenye mpenyo mdogo, nilichungulia kuona kama ndani kutakuwa kuna usafiri wa Anwari ule n'louzoea, kweli pale mbele ya nyumba yake nikaliona gari hilo, hapo nikapata uhakika Anwari atakuwamo ndani, shida ikabakia naingiaje humo?

Siku ile ndo' ile niliona umuhimu wa kuwa na mlinzi, hata kama ni mzee tu aiyejiweza kwani laiti angalikuwapo basi angalikuwa msaada mkubwa sana kwetu.

Nilijiuliza sana siku hiyo, hivi Anwari na nyumba yote ile anakosaje kuwa na mlinzi? Ni kwamba anajiamini sana ama ni kitu gani?

Niliongea mwenyewe, nililaani mwenyewe, nililaumu mwenyewe. Hamna kilichosaidia.

Ni baadae ndipo akili ilinijia nikatazama simu yangu kwenye majina nilohifadhi, humo nikampata bwana mmoja anaitwa Adrian, bwana huyo niliwahi kupata namba yake kipindi cha nyuma sana ingali nikiwa kwenye mahusiano na Anwari.

Kipindi hiko nilitambulishwa kwa Adrian kama rafiki wa mpenzi wangu, naye nikamjua na kuishi naye vema, lakini urafiki ule baina ya mabwana hao wawili haukudumu sana tangu mimi kutambulishwa kwao, wakatengana.

Anwari alinambia, kwa maelezo ya juu juu tu, kwamba Adrian hakuwa rafiki wa kweli wa maisha na hivyo wametengana, mimi sikupeleleza wala kusumbuka sana, niliamini wanaume hao wanajuana wenyewe kuliko mimi ninavyowajua kwahiyo maisha yakaendelea kama kawaida.

Lakini leo hii, katika simu yangu nzima, sina mtu yeyote ninayemjua kama mtu wa karibu wa Anwari isipokuwa Adrian, rafiki wake wa zamani, angalau nikaona hapo ndo' sehemu ya kuanzia.

Nilimpigia bwana huyo nikiomba awe anapatikana, bahati kwangu akapatikana na simu akapokea.

Nilimweleza kila kitu, hali niliyomo na namna ninavyomhitaji anisaidie, akanisikiliza na bahati tena akasema anakuja muda si mrefu pale nilipo.

Kweli, kama baada ya robo saa hivi, bwana huyo akafika hapo, tuliongea kidogo akakata shauri ya kukwea kuingia ndani akitumia mgongo wa gari yake.

Alipoingia alinifungulia geti kisha tukazama ndani ya jengo la Anwari tukiwa tunaita, uzuri milango ya ndani haikuwa imefungwa hata mmoja kwahiyo hatukupata tabu kuingia ndani.

Kule chumbani, tukamkuta Anwari akiwa amelala chini, hajitambui, ametokwa na mate sijui povu mdomoni mwake, kwenye kiganja cha mkono wake wa kuume kuna sindano, sindano ambayo Adrian aliichukua akaishika na kuitazama.

Aliitazama sindano hiyo akaguna kisha akanambia habari ambayo kwangu ilikuwa ngeni na ya kushtua, ati ya kwamba sindano ile ilikuwa ni ya madawa.

Madawa aina ya heroin.

Kwasababu hiyo, tulimkimbiza Anwari hospitalini, anahema kwa tabu, njiani tukawa tunaomba tufike naye salama ili wataalamu wamsaidie.

Siku hiyo ndo' nikajua kwanini urafiki wa Adrian na Anwari ulivunjika, Adrian alinambia punde Anwari alipoanza kutumia madawa ya kulevya walikosana kila mtu akashika njia yake.

Wala hakukuwa na sababu nyingine isipokuwa hiyo.

Jambo hilo kweli likanishangaza, yani muda wote huo nlokuwa kwenye mahusiano na Anwari sikuwahi kuhisi kitu chochote kuhusu matumizi yake ya madawa?

Aliwezaje kujihifadhi kiasi hiko? Sikupata majibu.

Niliwaza pia na mimi nilivyoleweshwa siku ile mpaka akanipeleka kwake na kuamka asubuhi, nikajiuliza ina maana alin'tilia madawa haya ya kulevya? Napo sikupata majibu.

Tulimfikisha bwana huyo hospitali, ileile ambayo Zai alikuwapo, akapatiwa huduma ya upesi na ya dharura.

Daktari alisema ilikuwa ni 'heroin overdose', tumpatie muda kidogo atarejea katika hali yake.

Tulirejea kule kwa Zai, Adrian akanisaidia kiasi fulani cha pesa, nilipojumuisha na cha kwangu na cha Zai pesa ikatoshea kulipia bili, uzuri kumbe Zai alishawasiliana na ndugu zake kadhaa wakamwezesha kwa kadiri walivyojiweza hivyo zoezi lake likawa limetamatika kwa mafanikio.

Kesho yake, Anwari aliamka akiwa na unafuu, dawa za kumwondolea sumu mwilini zilimsaidia sana angalau akarejea katika ubinadamu wake, japo bado alikuwa anasema anahisi kizunguzungu kwa mbali na kichefuchefu vilevile.

Baada ya siku tatu, Anwari alipona kabisa, hata Zai naye alikuwa anaendelea vema hivyo ikawa ni heri maana kila mtu aliendelea na shughuli zake kama kawaida.

Baada ya siku kama mbili hivi, Zai alinipatia taarifa ambayo haikuwa nzuri kiasi kuhusu kule kazini kwao, Zai alisema menejimenti ya shule ilikaa ikafikia maamuzi ya kumfukuza kazi, hivyo ndo' namna mkuu wa shule alivyomwambia.

Na sababu yake kufukuzwa kazi ni mbili; moja ameonekana ni hatari kuwa katika mazingira yake ya kazi lakini pia kushindwa kumudu majukumu yake kwasababu ya kukosekana eneo lake la kazi mara kadha wa kadha.

Kwakweli swala lile lilimgusa sana Zai, aliniambia kwa sauti ya kulia na mimi nikaguswa sana ukizingatia mwanamke yule alikuwa ametoka kwenye majanga muda si mrefu.

Kwaajili ya kumfariji, nikamwambia tuonane kesho yake tupate kuzungumza, na hapo ndo' ukawa mwisho wa maongezi yetu tuliyoyahitimisha kwa kuonana lakini pia kwa kutafuta tiba ya tatizo letu kule kwa mama Miraji.

Lakini cha ajabu, siku hiyohiyo, nikiwa nimerejea nyumbani, sina hili wala lile, nafanya shughuli zangu za nyumbani, mara Amiri ananifuata jikoni na kunambia nina mgeni.

Hapo nikastaajabu kidogo maana sikuwa na miadi na mtu yeyote yule, nikamuuliza Amiri mgeni huyo ni nani, naye akaniambia hamjui, lakini aliponishtua ni kuniambia mgeni huyo ni mwanaume.

Kweli hapo moyo wangu ukapiga fundo kubwa.

Nilitoka upesi kwenda kutazama, hamaki kule njenya geti nikaliona gari la Anwari! Hapo nikahisi miguu yangu inatetemeka kwa woga na hasira, huyu bwana ananitaka nini?

Sasa ameona aje kwangu kabisa?

Kabla sijamfuata kumbe naye alikuwa tayari ashatoka kwenye gari lile, nahamaki mtu huyu hapa pembeni yangu ananisalimu na kuniomba aingie ndani tukaongee.

Nikamtazama bwana huyo, sikuamini kama kweli yuko sawa kichwani, mtu mzima hawezi fanya vitu kama vile wallahi!

Nilimwambia Anwari aondoke upesi kabla sijamuitia mwizi, ajabu bwana huyo hakuogopa, akasema ita tu, na alisema hivyo maana anajua nisingeweza kufanya hiko kitu.

Mwishowe sasa ati akanipa sharti, kuondoka kwake pale ni mpaka atakapomuona mtoto wake.

Kweli kitendo kile cha kusema mtoto kikanipasua moyo na kichwa kwa mkupuo!

Nilitazama kando zangu kama kuna ambaye amesikia kauli ile, nikaona hamna, nikamrudia Anwari kwa jicho langu lote la ukali, nikamwambia kwanguvu sana, ondoka ondoka! Ondoka kwangu upesi.

Bado akasema haendi. Hatoki hapo labda amwone mwanaye au aongozane na mimi.

Nikiwa nazoza hapo, nabweka tu lakini cha kufanya sina, ndipo akatokea Amiri nyuma yangu.

Kijana huyo alisimama kando yangu akaniuliza kuna tatizo? Nikamwambia si huyu bwana hapa, amenisimamia mbele ya nyumba yangu ananifanyia vurugu.

Basi Amiri hakuuliza tena, alimjongea bwana Anwari mpaka mbele kabisa ya uso wake, akamwambia: "Tokomea hapa upesi!"

Anwari akatabasamu, kweli hata ingekuwa mimi ningelitabasamu maana kwa umbo la Amiri ukiliwanisha na Anwari ni kama vile kuku na kinda lake, nilishangaa kujiamini kule alikutolea wapi?

Tena mbele ya mbaba mpana kama yule.

Anwari aliuliza kwa kebehi, "ala! Na huyu kunguru ndo' nani?"

Amiri akamjibu ...

Akamjibu jibu ambalo mpaka leo hii nalikumbuka vema sana, alimwambia; "kunguru huyu ni Amiri, Amiri asokuwa na baba wala mama, kwahiyo unaweza ukaniita Amiri wa Amiri wa Amiri."

Kisha akamuuliza Anwari, "utaondoka hapa ama lah?"

Nikamwona Anwari kama amepigwa na bumbuwazi hivi, bumbuwazi la kumtazama Amiri, hakubisha tena bali akanitazama kwa macho ya ahadi kisha akalifuaga gari lake, hapo ndo' na mimi nikamsindikizia na maneno: "madawa yanakupelekesha wewe. Yatakuua usipate wa kukusaidia tena!"

Niliposema maneno hayo aligeuka akaniambia wewe si upo, hofu ya nini? Sikusema tena kitu, akawasha gari lake na kutokomea.

Nilimshukuru Amiri kwa kunisaidia, naye akaniahidi bwana yule hatokuja kunisumbua tena, wala nisijali. Basi nikamshukuru zaidi na zaidi.

Kama bahati, hatujakaa vema wala bado hatujarejea ndani ya uzio, gari la bwana Mgaya linatokea kwenye kona.

Bwana huyo anatusalimu na kisha anauliza mbona ameliona gari fulani hapo nyuma ya njia? Alikuwa ni nani yule?

Kwakweli mimi sikuwa nimejipanga na wongo wowote ule, pale nilikuwa nimeshtukizwa, ajabu nikiwa najitafuta Amiri anaingia na kusema bwana yule ni mteja maziwa, amekuja kuulizia bei zetu ili zitakapompendeza basi tufanye biashara.

Mgaya akafurahi sana.

Alimpongeza Amiri na hata mimi pia, hapo mambo yakageuka, tulitoka ndani kwa taharuki lakini sasa tunarejea kwa mbiu ya ushindi.

Ushindi wa kishindo.

Ushindi wangu na Amiri.

Lakini niliwaza ushindi ule ungedumu kweli? Nilisema na sauti zangu kichwani.

Hamna anayejua siku wala saa ya bwana Anwari kuibuka tena getini mwangu kugonga. Laiti ningelijua kuhamisha makazi yangu nikayapeleka mahali salama basi ningelifanya hivyo.

Hofu yangu hiyo ikaninyima raha.

Nilisahau kijana Amiri aliniahidi jambo lile halitatokea tena, na pengine hata ningelikumbuka nisingelitilia maanani, ningelidhani ni maneno tu ya kamusi, maneno yasoweza hata kutikisa jani la mtini, lakini kumbe nilikuwa nimekosea.

Amiri hakuwa mtu wa kupuuza yale yamtokayo kinywani. Nilikuja kujifunza hili baadae sana.

Ningalijua mapema huenda ningelichunga ndimi yangu kuwa mbali na maafa.

Kesho yake, nilidamka mapema kama ilivyo kawaida nikaongozana na mtoto kwenda shule, majira ya mchana nikiendelea na majukumu yangu yanayoelekea ukingoni, mara napokea simu ya bwana Adrian, rafiki yake na Anwari.

Bwana huyo alinisalimu vema kisha akaniuliza kama nimeongea na Anwari siku hiyo, nikamjibu hapana, kwanza nilikuwa nimem-block palepale jana yake alivyokuja kunisumbua nyumbani maana alienda kinyume na makubaliano yetu, hayo niliyasemea moyoni mwangu, yeye nikamwambia tu kuwa sijawasiliana na huyo bwana.

Basi nilivyompa hayo majibu akakata simu na mimi nikaendelea na shughuli zangu, baadae kidogo natoka shuleni, sasa nielekee kule kwa Zai kama nilivyopanga, simu yangu inaita tena na mpigaji akiwa ni yuleyule, yaani bwana Adrian.

Bwama huyo mara hii haulizi tena kama niliongea na Anwari bali ananipa taarifa ya msiba.

Msibwa wa Anwari.

Amemkuta bwana huyo kama kawaida chumbani mwake akiwa amejidunga na kujizidishia dozi. Mara hii hajanusurika tena, ameenda njia moja isiyokuwa na pa kutokea!

Amekufa kama vile n'livosema.

Amekufa kwa madawa.

Sasa ni kweli hatonisumbua tena kama alivyosema Amiri.

Sasa hamna atakayejua kuwa nimezaa naye. Hamna atayejua mtoto yule ni wa kwake, ameenda na jambo lake kifuani, hapana, hapo nilikumbuka kitu, Anwari hajaenda na jambo lake, Zai anafahamu siri hii.

Siri ya nguoni.

Lakini hakuna mtu yeyote aliyekuwa anafahamu, hata mimi mwenyewe vilevile, ya kwamba muda huo nilikuwa tayari nina kiumbe kingine tumboni.

Kiumbe cha marehemu.

Na hapa ndipo mkasa wa Zai na kifo chake unapoanzia...
Ahsante sana mkuu

baby zu Bantu Lady Antonnia Firdaus9 Dr Restart
Njooni tupitie huku
 
Back
Top Bottom