Niliweka shada za maua kwenye makaburi matano ya watu wangu wa karibu

Niliweka shada za maua kwenye makaburi matano ya watu wangu wa karibu

Ila wabongo ni konyo sana, imagine mtu kaanzisha simulizi kwa hiyari yake, kosa lake kuchelewa kupandisha mwendelezo tu kakutana na matusi na vichambo vya kila aina. Huwa nacheka sana nikiufungua huu uzi. Watu hata hawajal alikua anakutana changamoto gani
Wamemkanda hadi sio poahh 😁!
 
kuna malalamiko kuwa wanachama wanasema unawacheleweshea story.. kama vipi kaa chini tunga maliza ndo uje upost kuliko kuwacheleweshea. tutaanza kugombana mimi na wewe. mimi nasimamia sana ustawi wa wasomaji. sipendi wawe na hasira au manung'uniko. kama umeshindwa kazi acha siyo kutaka waanze kukubembeleza. hadithi nyepesi kama hii unashindwaje itunga kwa haraka tu ukamaliza? angalia sana dogo usije sema mimi mbaya hakikisha kila siku unaleta episodes za kutosha.
Jamaa jinga wewe[emoji1787][emoji1787][emoji1787]
 
Sehemu ya Nane:

Macho ya Zai yalikuwa yanasema jambo.

Jambo lililonitisha.

Si bure alikuwa anafahamu kitu na kitu hicho kilinifanya nitetemeke kwa hofu. Nilitaka kuendelea kuwapo hapo ili anieleze ni nini anajua lakini sababu ya muda nililazimika kuondoka, labda nirejee tena muda mwingine.

Kama si yule mwalimu mkuu kunikawiza kule shuleni, huenda siku ile ningeyasikia yote toka kwenye kinywa cha Zai.

Niliondoka zangu lakini kichwa nilikiacha palepale hospitali kwa mawazo, kweli sikwenda nacho, kuanzia kwenye daladala mpaka nyumbani kwangu nilikuwa nikiyatafakari yale nilosikia, hata chakula sikuhisi ladha yake.

Nilifungua simu yangu nikampigia Anwari, kwasababu nilikuwa nimemblock, ilibidi nimu-unblock kwanza kisha ndo' nifanye zoezi langu, kidogo simu kuita bwana yule akapokea, hakujua kama ni mimi maana namba ilikuwa ngeni lakini aliponisikiliza nilipotamka maneno mawili aliita; "Magreth!"

Sikumwitikia, nilimuuliza moja kwa moja ni nini amemwambia Zai, hapo akakwama kusema, hakutaka kujibu, badala yake aliniomba tuonane mahali ili tupate kuyajenga. Muda na siku nipange mimi mwenyewe.

Aliniambia,

"Nimekutafuta mno lakini sikufanikiwa, hakukuwa na haja ya kufikia huku, mpenzi."

Hilo neno 'mpenzi' kweli likanikera, sijui kwanini lakini lilininiga koo, ujumbe huo nikaufuta papo hapo nisipate kuuona tena. Baada ya hapo niliendelea na maandalizi yangu binafsi, kuandaa chakula cha nyumbani na kufanya kazi zingine ndogondogo, lakini niwe mkweli, hamna nilichofanya nikafanya vema, kuna muda nilihisi mikono yangu inatetemeka kwa kuwaza dhambi nilofanya.

Dhambi nilofanya na Anwari.

Vipi yale ya gizani yakaja mbele ya mwanga tele? Nitachimbia wapi uso wangu kujificha nisishikwe na haya hii? Wapi nitakatiza nisigeuke kuwa mada?

Hilo lilininyima raha.

Baadae mume wangu alirejea nyumbani, mapema ya saa tatu, na siku hiyo alirejea pamoja na vitu tele, vitu vya nyumbani na zawadi zangu binafsi.

Nakumbuka aliniletea chupa kadhaa za marashi ya ghali, viatu bila kusahau magauni, hakumsahau mtoto, naye alimletea nguo kadha wa kadha akijigamba na kujivunia ya kwamba mtoto yule ni 'jembe' lake.

Siku hiyo bwana alikuwa na furaha sana, alitabasamu kila mara, akacheka na kunikumbatia, ni baadae ndo' akanieleza ya kwamba kule kazini amepandishwa nafasi, sasa hatokuwa anaendesha tena watu huku na kule bali atakaa ofisini kuwasimamia madereva wenzake.

Madereva hao sasa watamwita 'boss' naye atawaita vijakazi. Maisha yamebadilika.

Basi siku ile tukala na kunywa vema, tulifanya hivyo kuyasheherekea mafanikio ya bwana Mgaya, kila mmoja wetu alijumuika mezani ikiwamo kijana wetu, Amiri, mimi kazi yangu ikawa kuigiza furaha nisokuwa nayo, kukenua meno na kujichekesha huku ndani yangu nawaza mambo mengine.

Nawaza furaha ya yule bwana. Nawaza furaha ya familia yetu. Furaha ambayo ndo' kwanza ilikuwa inachipukia baada ya mapito kadhaa.

Bwana Mgaya alifungua chupa kadhaa za ulabu, chupa alizokuja nazo na zingine zilizokuwamo katika jokofu, akanywa kwa kujipongeza.

Alipiga mafundo kadha wa kadha akisindikizia michapo ya hapa na pale, baada ya muda pombe ikaanza kumpangia cha kusema na kumwongoza namna ya kutenda, akaanza kusema namna gani anavyonipenda, namna gani atakavyonipambania.

Aliyasema mambo lukuki lakini pombe haikumpa akayamaliza, punde akapitiwa na usingizi mzito. Alijilaza kwenye kochi akiwa hana hili wala lile.

Hapo Amiri alinisogelea akaniuliza kwa sauti ya chini, "uko sawa kweli?"

Nikamtazama, kisha nikamtazama mume wangu alokuwa amelala kama mbwa alochoka pale kwenye kochi, hamna habari alonayo, nikamrejea kijana Amiri na kumuuliza kunani akaniuliza hivyo?

Amiri akasema sina furaha, ni kweli sikuwa nayo lakini alitambuaje? Siku ile sikulia na nilijitahidi kadiri ninavyoweza kuigiza furaha usoni mwangu mbele ya mume wangu, yeye katambuaje?

Wakati nikijiuliza hayo kichwani, aliniongezea swali jinginewe, "kitu gani kinakusumbua au umemkumbuka mama mkwe wako?"

Nikamshukuru kwa kujali lakini nikamsisitiza hamna jambo lolote lile, tule na tunywe kusheherekea mafanikio ya bwana Mgaya, tusiharibu tafrija yetu kwa kuleta mawazo hasi yasokuwa na faida.

Basi baada ya muda kidogo, Amiri akaniaga na kwenda zake nje, alinambia anaenda kukagua na kutazama mifugo kabla hajaenda kulala, alipotoka nikabaki mwenyewe sebuleni kama mtu mwenye ufahamu, nilimalizia kinywaji changu nikamsindikiza bwana Mgaya kwenda chumbani kupumzika.

Nilipomlaza nikaanza kujishughulikia mwenyewe mahususi kwaajili ya kulala maana asubuhi nahitajika kudamka mapema na jua.

Jambo la kwanza nilofanya nilitoa pedi yangu nilovaa tangu mchana, nilikuwa kwenye siku zangu siku hiyo nikianzia tokea majuzi yake, nikaiweka pedi hiyo pembeni kisha nikaoga na nilipomaliza nikaichukua kwenda kuihifadhi kwenye 'bin' maalum tunapowekea taka.

'Bin' hiyo ilikuwa nje ya nyumba kwenye kibaraza cha mlango wa nyuma.

Nikiwa na taulo langu kifuani, nilielekea huko na nikafanya kile kilichonipeleka, lakini kabla sijafunga mfuniko wa ndoo ile maalum ya taka, niligundua jambo fulani lililonichukulia muda wangu.

Kwa mara ya kwanza kutazama, sikuamini, lakini nilivyopepesa macho kukagua nilihakikisha nilichokiona kilikuwa sahihi.

Pedi zangu za nyuma, takribani tatu kwa idadi, hazikuwamo mule ndani! Sikujua zimeenda wapi na nani kazichukua.

Nikiwa hapo, bado nabung'aa, mara nikasikia sauti za kuku kule bandani, kuku walipiga kelele kana kamba wamekurupushwa na kitu fulani, nikapaza sauti kuita;

"Amirii!"

Kimya.

"Amiri ... ni wewe?"

Sikujibiwa.

Kuku wakapiga tena kelele, kwaaakwakwakwaaa! Moyo wangu ukalipuka na wasiwasi, niliwaza pengine kuna mnyama ama mdudu hatarishi ameingia kwenye banda la kuku, nikasogea taratibu nikiendelea kuita Amiri Amiri, ni wewe uko bandani?

Nilisogea mpaka kwenye uzio wa mabanda, nikasimama na kutazama, nilitamani kuingia humo ndani lakini niliogopa sababu ya kiza, kule mabandani hapakuwa na taa, mtu angeingia kwanza ndani kisha ndo' aichukue kurunzi iliyokuwa inang'ining'inia kwenye kuta ya ng'ombe kwaajili ya kujipatia mwanga.

Mimi hata kuingia humo sikutaka kabisa.

Nilisimama nikisikia kelele za kuku pasipo kuwa na msaada, sauti hizo hazikudumu muda mrefu kukawa shwari, hapo ndipo mimi nikarejea ndani kwaajili ya kupumzika.

Mpaka naingia ndani ya chumba changu sikupata kumwona kijana Amiri. Nilijiaminisha labda alisharejea chumbani kwake na sasa ameupumzisha mwili wake kitandani. Kitu kilichonifanya nikaamini hivyo ni ule mlango wa grill.

Niliufunga mlango huo na hakuna aliyeugusa mpaka asubuhi nilipoamka.

Kesho yake baada ya kumaliza majukumu yangu kazini, niliwasiliana na Anwari nikimtaka tuonane pahali fulani.

Kwasababu ya kujiweka salama, nilimuelekeza aje mgahawa mmoja hivi ambao haukuwa mbali sana na shule ninapofanyia kazi, faida yake haitanichukua muda mrefu kumpitia mwanangu niliyemuacha shule, nikimaliza tu maongezi basi dakika chache tunajiondokea kwenda zetu nyumbani.

Kweli, ndani ya muda mfupi, Anwari aliwasili kama vile tulivyowekeana miadi.

Bwana huyo alikuja hapo na gari yake akanipendekeza tuongelee mambo yetu ndani ya gari badala ya pale mgahawani, hoja yake mule ndani ya gari ni salama zaidi kuliko mbele ya macho ya watu, mimi pia nikaona wazo hilo ni jema basi nikaliheshimu.

Niliingia kwenye gari maongezi yetu yakaanza kwa mimi kuuliza maswali mengi yenye pupa na hasira, maswali juu ya makubaliano yetu tuloweka, makubaliano ya siri, nikauliza makubaliano hayo yamefikaje kwenye masikio ya Zai?

Naye akaniuliza, "ulitaka mimi nifanye nini kama sikupati kwa kila njia? Namba yako haiiti, unapofanyia kazi sipafahamu, ningefanyaje?"

Kweli lengo langu lilikuwa ni kumpoteza bwana huyu katika ramani ya maisha yangu, na niliyapanga hayo pasipo kumshirikisha mtu yeyote yule kwani Anwari kwangu nilimrejea kwaajili ya jambo moja tu, kunisaidia pale nilipokuwa nimekwama, kwahiyo baada ya kupata msaada huo kwangu hakubaki na tija tena, nilitamani nifute kurasa yake lakini nafuta nini?

Naufutaje?

Na hapo nilipokuwa namsikiliza ndo' nikaamini kabisa kuwa kipande cha Anwari hakikuwa ukurasa mmoja bali ni kitabu kizima!

"Lakini Anwari," nilisema naye kwa mkazo, "ni nani aliyekwambia mimi nina mtoto? Na ni nani aliyekwambia kuwa mtoto yule ni wako? Au umekaa tu ukaanza kuyatengeneza maghorofa yako kichwani?"

Niliuliza huku nafsi yangu ikinisuta maana nilijua kabisa najidanganya mwenyewe. Ukweli ndani yangu unanizodoa. Ukweli ambao hapa najitahidi kuuficha kwa nyavu nikiamini hautaonekana mbele za watu.

Miaka miwili na miezi kadhaa nyuma, mimi mwenyewe, wala si kwa kusingiziwa wala kusemewa wongo, nilirejea kwenye mlango wa Anwari baada ya kushindwa kuhimili presha kuwa kubwa kutoka kwa mama mkwe wangu.

Mama huyo alianza kuninyooshea kidole, miezi michache tu kupita baada ya kufunga ndoa na bwana Mgaya, akisema mimi ni mgumba nisiyeshika mimba.

Mama huyo hakutambua wala hakujali ni namna gani tulijaribu kutafuta mtoto mimi pamoja na mwanaye, nikicheza na kalenda yangu kwa ustadi mkubwa, lakini hatukupata matunda.

Swala hilo likanifanya nihofie kumpoteza mume wangu kwa wanawake wengine, wanawake wenye mayai yao, punde watakapomfanikishia kumpa mtoto basi kwangu itakuwa ndo' kwaheri ya kuonana.

Lakini baadae nilikuja kupata shaka, vipi kama mwanaume yule ndo' mwenye matatizo na si mimi kama ninavyojiwazia?

Vipi kama bwana Mgaya hana uwezo wa kunipa ujauzito?

Kwa kipindi hiko nilikuwa na shakashaka, lakini baadae bwana Mgaya alivyokuja kusema kuhusu mwanamke yule wa kijijini, Momo, ya kwamba amemuacha hana mimba wala mtoto wake, nikazidi kuthibitisha kichwani mwangu kuwa bwana yule alikuwa na shida bayana kwenye via vyake vya uzazi.

Basi kwasababu ya ile kiu ya mtoto na hivi muda huo sikuwa na uhakika na utimamu wangu wala wa utimamu wa bwana Mgaya, ndipo nikakutana na Anwari katika siku zangu za hatari.

Nilishiriki tendo na bwana huyo mara moja tu ikatosha kabisa kubadilisha wiki yangu ilofuata kwani nilianza kuhisi mwili wangu haupo kawaida na vile nilivyouzoea.

Baada ya juma la pili nilipima na kuhakikisha nina ujauzito, hapo ndo' nikaona ni muda muafaka sasa wa kumpoteza Anwari katika maisha yangu kwa kum-block kila kona, kila mtu aendelee na njia yake .

Lakini sasa ni wazi nishafeli. Anwari niko naye hapa kwenye gari akinieleza mambo ya mtoto, hata akipata kauli kama mimi na yeye hatupo kwenye mahusiano basi haina shida kabisa, yeye anamtaka tu mtoto wake.

Ati mtoto wake?

Hahahaha Anwari ....

Mtoto gani?


****
Mwanzo ilionekana Mgaya alianza mahusiano na Momo wakiwa tayari wana mtoto na Magreth.

Hapa inaonesha mtoto alipatikana baada ya Mgaya kuoa na kuacha Momo
 
Sehemu ya Kumi:


Nilikurupuka sana, kichwa kinaniwaka moto, nikavaa nguo zangu kama nakimbizwa lakini tena nikazivua.

Mwili ulikuwa umechunda kwa jasho. Harufu haieleweki. Vipi nikikutana na Mgaya nyumbani? Akihisi harufu hii haitakuwa tabu?

Nikakimbilia bafuni kuoga, nilijimwagia maji upesiupesi, hata sabuni haikutoka vizuri mwilini nikawa nishatoka na taulo kujifuta.

Nilijipakaa mafuta toka kwenye mkoba wangu, nikavaa upesi na kutengenezea nywele zangu vema, vilevile kama nilivyotoka nyumbani, nilipomaliza nikajipulizia marashi, yale aloniletea mume wangu kama zawadi, baada ya hapo nikawa tayari kuondoka.

Hapo nilitumia robo saa tu mpaka kuwa mkamilifu. Siku ile ndo' nilijua kumbe kujiandaa harakaharaka naweza, maana mimi desturi yangu ni kutumia si pungufu ya lisaa na kitu kwenye kujiandaa tu.

Muda wote huo nikiwa najiandaa, Anwari alikua amejilaza kitandani akinitazama, japo nilikuwa nafoka na kutusi juu, bwana yule hakuonekana kujali, ni kama vile alikuwa anafurahia yale yanayoendelea pale, namna mimi ninavyoteseka na kuhanyahanya.

Aliniuliza nikupeleke? Nikamjibu sitaki hata kuona sura yako, Anwari, achilia mbali kunipeleka.

Kwa hofu nilokuwa nayo, nilichuruza jasho japo nilitoka kuoga muda si mrefu na mule chumbani kulikuwa na kiyoyozi kinachoyoyoa hewa kwa mbali.

Anwari aliniambia; "sasa kama hutaki nikupeleke, utapata wapi usafiri haya maeneo yetu?"

Japo sikutaka kuzungumza naye wala kuongozana naye, ila alichokisema Anwari kilikuwa ni kweli, kule alipokuwa anaishi kulikuwa ni mbali na kituo cha magari na sikuwa na namba yoyote ya dereva aidha pikipikipiki au bajaji.

Kwahiyo hapa nikajikuta namrejea tena Anwari kama waswahil na baniani mbaya ...

Bwana huyo aliongozana na mimi, ndani ya gari yake, simu yangu nimeishikilia mkononi nawaza niandike nini ama nimpigie nani na ninwambie nini.

Niimtazama Anwari, nikayawaza mengi kichwani mwangu, Anwari ni nini umenifanyia? Nilimuuliza. Anwari, kwanini umenifanyia hivi?

Unajua kabisa nina familia nyumbani, mtoto na mume pia, hayo kwako hayakutosha?

Naye akanijibu kwa kuniuliza, kama ningekuambia ungenikubalia? Kisha akaongezea, si ungeanza kusema ngonjera zako za mimi ni mke wa mtu, nina mume wangu?

Bwana huyo akahitimisha akisema alikuwa ananihitaji na ndo' maana akafanya vile.

Akafanya ....?

Hapo ndo' fikra zangu zikakumbuka mchezo ulipoanzia.

Nikiwa pale kwenye benchi la kungojea, mimi pamoja na yule ndugu yake Zai, bwana Anwari alituomba radhi akatoka idogo kwenda mahali nisipopafahamu.

Baada ya dakika kadhaa, bwana huyo alirejea akiwa na chupa mbili za soda na 'foil' lillokuwa na nyama ya kukaanga ndani yake, akaniambia shika hii nimekuletea, najua una njaa.

Na ni kweli nilikuwa na njaa, nyumbani nilipika lakini ile dharura yangu ilin'tia pupa nikaondoka tumbo likiwa tupu, sikuwa nimekula tangu majira ya mchana, tena mchana wenyewe niligusagusa tu chakula cha shuleni maana nacho huwa cha hovyo.

Kwahiyo kwa ile njaa nilokuwa nasikia, 'foil' na kinywaji kile niliviona kama mkombozi.

Nilipovishika niliacha vinipe ahueni ya hali yangu, na kweli vikaninusuru, lakini kumbe vilitumwa kwa mkakati maalum.

Mkakati wa kunidhoofisha taratibu kadiri na muda.

Anwari alijua kunipata kweli, na alijua kunitumia. Makosa yale niliapa kutoyarudia kamwe katika mikono yake.

Huwezi kuamini alinambia, kama mimi nilivyokuwa namhitaji kipindi kile mpaka nikamrubuni akalala na mimi, basi naye ndivyo hivyo hivyo alivyofanya, hamna mwenye dhambi kumshinda mwenziwe.

Aliponifikisha maeneo fulani ambayo naweza nikapata usafiri kwa urahisi, nilimtaka anishushe niende zangu mwenyewe.

Niliposhuka nilinyookea moja kwa moja nyumbani nikitumia usafiri wa pikipiki, kufika Amiri ananipokea mkoba na pia ananipokea kwa maneno ya yale yalotukia pale nyumbani.

Alinambia bwana Mgaya hayupo, ametoka na mtoto kwenda asipopajua lakini alienenda akisema lengo lake ni kunitafuta mahali nilipo kwani simu zake hazipokelewi na hana habari yoyote ile.

Amiri alinambia bwana Mgaya alikuwa kama mtu alochanganyikiwa, anaongea mwenyewe na kufokea hewa, hata alipoingia kwenye gari lake alisahau funguo, alipoenda kuuchukua ufunguo akamsahau mtoto, alipomrejea mtoto akasahau simu!

Alienda akarudi akipiga honi nyingi, niletee simu yangu, niletee simu yangu!

Katikati ya masimulizi hayo ya Amiri, mara simu yangu ikaita, kutazama ni yuleyule tulokuwa tunamwongelea, yaani bwana Mgaya, nikapokea simu hiyo kwa mara ya kwanza na kumwambia niko nyumbani, nimeingia hapo muda si mrefu.

Alipotaka kuniparamia kwa pupa ya maswali, nikamwambia aje kwanza nyumbani, tutaongea kila kitu, haina haja ya kumaliza muda na salio la simu.

Basi nikiwa naongea na simu hiyo ya bwana Mgaya, bado hatujamalizana, mara simu nyingine ikawa inaingia na kuita 'diiii-diiii diii-diiii' kutazama naona jina la Anwari kwenye kioo!

Hii ndo' sababu sikuwa nataka kumpatia bwana huyu namba yangu, najua hana mipaka, hajui muda gani wa kutulia na muda gani wa kutenda, kweli anapiga muda huu na yale yote yalotokea?

Vipi kama ningemkuta bwana Mgaya pale nyumbani?

Mgaya alipokata simu, nilipokea ile simu ya Anwari nikafoka kumuuliza anataka nini? Anahangaika nini na mimi muda huo baada ya kunitenda yote yale? Ajabu bwana yule akawa anaongea mambo nisiyoyaelewa, alikuwa anabwata kama mtu alozidiwa na ulevi na mimi baada ya kuona huo ni upuuzi, nikakata simu yake.

Nilikata simu hiyo lakini nikaendelea kuongea mwenyewe kama mwehu. Nasonya kila mtindo.

Amiri aliyekuwa amesimama kando ananitazama kana kwamba bango, aliniuliza, "kuna tatizo?"

Sikumjibu, nikaingia zangu ndani moja kwa moja mpaka chumbani.

Muda si mrefu, bwana Mgaya akiwa ameongozana na mtoto wailifika nyumbani kikazuka kikao cha dharura.

Bwana Mgaya alikuwa amefura kwelikweli na mimi sikuwa na kingine cha kumweleza isipokuwa kumtumia mgonjwa Zai kama ngao yangu.

Nilimwambia rafiki yangu Zai yu hospitali amelazwa na mimi nilikimbilia huko kumwona baada ya kupewa taarifa hiyo mbaya.

Aliniuliza mbona sikuwa napokea simu yangu wala kurejesha jumbe zake lukuki? Nikasema simu yangu niliisahau nyumbani kwa zile haraka zangu, nilikuja kubaini sina simu nilipofika hospitali na sikuwa na namna tena.

Nilimwambia: "kumbe niliisahau simu jikoni ndani ya shelvu, nilivyorudi Amiri akanisaidia kupekua huku na kule maana simu yenyewe haikuwa na sauti, hata kuipiga isingesaidia."

Hapo nilimtazama Amiri, Amiri naye akajua kila jambo ndani yangu, sikuhitaji kumweleza kitu zaidi ya yale macho mangu, naye akashika hatamu kama vile tulikaa kitako kuyapanga yale mambo.

Akamweleza Mgaya namna tulivyotafuta simu mule ndani na namna mimi nilivyohamaki baada ya kuipata simu hiyo na kuona jinsi Mgaya alivyonitafuta.

Aliyaeleza mambo katika namna ambayo alinishangaza. Aliyasema kwa kujiamini pasipo kupepesa macho hata kunishinda mimi mtunzi wa wongo ule.

Alipomaliza hayo maelezo, Mgaya akabakiwa na hoja dhaifu, hakuwa na kingine cha kusema zaidi ya kukazia kwenye swali lake la kwanini usingechukua simu ya mtu mwingine ukanipa taarifa?

Alisema alikuwa na hofu sana juu ya usalama wangu kiasi cha kuanza kufikiria kupita vituo vya polisi ama kupita hospitalini kuniulizia.

Alisema laiti asingeniona siku hiyo nzima, basi angeanza zoezi hilo mara moja.

Baada ya hiko kikao, niliongozana na Mgaya kwenda naye chumbani, sasa nina amani maana kikwazo kile nimekikwatua.

Baadae nilipiga simu kule hospitali kwa ndugu yake Zai kumuuliza hali ya mgonjwa, nilipopata taarifa njema nikaendelea na ratiba yangu ya kawaida, nikipanga kesho ama keshokutwa nikitoka shule basi nipitie tena hospitali kumjulia hali rafiki.

Kweli baada ya siku mbili, kama nilivyopanga, nilifika hospitali na huko nikamkuta Zai anangoja kupewa bili yake ili apate kurejeshwa nyumbani, hali yake ilikuwa njema, si haba.

Bili ikatoka anadaiwa kama laki sita hivi kwa ujumla, achilia mbali bili ya siku ile ambayo Anwari alikuwa amemsaidia.

Sasa shida ikaja Zai hakuwa na pesa hiyo mfukoni, kwa maelezo yake alibakiwa na laki mbili tu kama akiba, akitoa hiyo hajui atadumu vipi na maisha mpaka kuja kuupata mwisho wa mwezi.

Hata yule ndugu yake anayekaa kwake hana kazi ya maana hivyo mbali na kumhudumia, kwenye swala la mambo ya pesa ni mtu dhoofu l'hali, pangu pakavu tia mchuzi.

Zai alisema; "Anwari aliniahidi atanisaidia kwenye hili janga langu mpaka mwisho wake lakini hata sasa simwoni."

Alisema amejaribu sana kumpigia Anwari pasipo mafanikio, mwanzoni simu yake ilikuwa inaita lakini sasa hivi imekuwa kimya. Ukipiga hapatikani.

Anawaza ni nini kimemkuta bwana huyo kwani si kawaida yake kupitisha siku asije kumwona, achilia mbali zimeshapita siku tatu sasa!

Alilalamika gharama za pale ni kubwa sana, kama ingekuwa ni kwa utashi wake mwenyewe asingekuja hospitali hiyo, angeenda zake hospitali za serikali, lakini Anwari alimsisitizia hapo maana anaamini pana huduma nzuri.

Sasa Anwari hapatikani, anafanyaje?

Nilitazama uwezo wangu binafsi wa kumsaidia rafiki Zai katika adha ile lakini bado sikufua dafu.

Kujikamua kote mifuko yangu niliambulia laki moja na alfu hamsini tu ya akiba ingali pesa inayohitajika pale hospitalini ni pomoni.

Nikajaribu kumpigia Anwari, simu haipatikani. Nikajaribu tena, bado haipatikani.

Nilijaribu kama mara tano lakini hamna nilichoambulia zaidi ya mhudumu kunihasa namba ya mteja ninayempigia hapatikani kwa muda huo.

Hapo akili yangu ikanikumbusha maongezi yangu ya mwisho na mwanaume yule.

Yale maongezi baada ya kuongea na Mgaya.

Yale maongezi niliyomfokea na kumtukana.

Nilichokumbuka katika maongezi hayo ni namna bwana huyo alivyokuwa anazungumza kana kwamba mwendawazimu mpaka mimi nikaikata simu yake.

Sasa leo hii hapatikani, na si tu leo ni tangu siku ile nilipoteta naye hewani.

Anwari, nini kimekukumba?

Sasa nikajiuliza na kichwa safi kisichokuwa na mawingu ya hasira.

Kwanini siku ile ulinipigia?

Ulikuwa unataka kuniambia nini ambacho sikuelewa? Na hicho ulichotaka kuniambia kina mahusiano na wewe kutokuonekana hospitali ama kutopatikana hewani?

Nikamwambia Zai acha niende nyumbani kwa Anwari nikatazame.


***
"Amiri alinambia bwana Mgaya alikuwa kama mtu alochanganyikiwa, anaongea mwenyewe na kufokea hewa, hata alipoingia kwenye gari lake alisahau funguo, alipoenda kuuchukua ufunguo akamsahau mtoto, alipomrejea mtoto akasahau simu!"

Nimecheka[emoji1787]
 
SteveMollel nimesikia kilio cha wasomaji. Nakupa masaa hayo ... Uwe umeweka kisa kingine au ujieleze kwa nini umekuwa na delay kuwatungia visa vingine wasomaji. Kumbuka kuwa hawakukuomba ulete hii story. Ni kiherehere chako mwenyewe. Sasa wameanza kufuatilia usianze kuleta madeko na mapozi.

Nakupa order tunga visa vingine ulete. Na kama umejichanganya sana sasa unakosa mwendelezo sema tu maana najua changamoto za utungaji sometimes kisa kinakosa mwendelezo sababu ulijichanganya sehemu.

Lakini kama sivyo utaniambia kwa nini usichukuliwe hatua kali kwa kuchezea hisia za wasomaji wengi ambao hawana cha kufanya hii story ndo ilikuwa inawasukumia siku zao.
[emoji1787]
 
Back
Top Bottom