All about Tanzania life
Member
- Jul 6, 2023
- 40
- 83
Mwanzoni kabisa mwa mwaka huu nilibahatika kutembelea mkoa huu unaotoa jiji mojawapo kongwe zaidi Tanzania.. Dhumuni kuu likiwa kwenda kujionea mambo kadhaa kuhusu mkoa huo ikiwa na pamoja kutembelea vivutio mbalimbali vinavyopatikana huko na kubwa zaidi kujiwekea kumbukumbu binafsi ya kukanyaga ardhi ya mkoa huo kama ilivyo kwa mikoa mingine niliyotembelea hapa nyumbani Tanzania.
Haikuwa safari ya kuchosha sana kama vile niliyotembelea mkoa wa Tabora na Songwe mbali kabisa mpakani mwishoni mwa Tanzania huko. Kufika hapa itakuchukua masaa machache tu , na kutokana na hali hiyo nililazimika kuunganisha usafiri na kuweza kushuka mpakani eneo kati ya mkoa wa Pwani na Tanga na kupata picha kadhaa hapo kwaajiri ya kumbukumbu, na nikiwa maeneo hayo niliweza kubahatika kuona mashine ya kusagia nafaka kwa ukubwa wake ikisafirishwa kwa kutumia bodaboda 😁 , niliweza kuchangia michango binafsi kadhaa ya ujenzi wa majengo ya ibada niliyokutana nayo njiani ( kwa ufafanuzi ni kuwa pembezoni mwa barabara kunakuwa kumewekwa kitu mfano wa kibubu kikubwa na maelezo machache juu ya sadaka yako utakayoweka hapo) pia nilifanikiwa kuhakikisha kwa macho yangu kuwa eneo hilo hakuna bango linalokuonyesha sasa unaondoka mkoa wa Tanga, hapo kuna karibu Tanga pekee, lakini kwaheri mkoa wa Tanga utalipata kichwani mwako siku ambayo utafanikiwa kutoka huko.
Kiukweli unaweza kufanya aina fulani hivi ya utalii wa kushangaza kabisa, mfano nilifanikisha kutembea zaidi ya kilomita tano kutoka mpakani mwa Mkoa wa Pwani na Tanga huku nikifanikiwa kuona kwa ukaribu maisha halisi ya wakaazi wa vijiji, kuona kwa macho jinsi mabasi na magari binafsi yanavyokatiza kwa kasi ya ajabu, usisahau watu kukushangaa, wewe unaona mambo mapya nao wanaona kitu kipya😁 pia ukipenda kutembea katika maeneo mapya au maeneo ambayo hukutegemea kabisa kama siku moja utakuwa huko unakuwa unajijengea hali fulani tofauti sana na furaha ya nafsi na utulivu wa ajabu sana.
Nilifanya matembezi hayo ya hisani hadi pale nilipoona inatosha sasa miguu inajaa vumbi na jioni inaingia, na uzuri zaidi ni kuwa njia hii ni rahisi sana kupata usafiri wowote kusonga mbele , ambapo ukiwa umesimama eneo zuri unaweza kusimamisha mabasi ya Tanga na ukapanda kama daladala tu, muhimu ujue kutofautisha mabasi yaelekeayo Tanga na mikoa mingine kama Kilimanjarona Arusha. Hivyo nikiwa njiani nikaiona Simba mtoto inakuja imechochea kweli kweli, umbali kama mita 500 hivi nikapunga mkono hewani na chini ya nusu dakika chuma kilikuwa mlango wazi na vile nilikuwa mwepesi ikawa kudandia tu juu kwa juu kama katekwa mtu.
Masaa kadhaa mbele tulikuwa ndani ya jiji la Tanga, njiani kukaribia jiji niliona majengo marefu ya kiwanda cha saruji, mashamba ya mkonge na vinyumba vingi vingi vya nyasi na udongo, barabara nyembamba na miji kadhaa iliyochangamka kiasi. Nilishukia kwa Minchi, kama sikosei, sehemu hiyo ilikuwa njiani mbele kidogo tu baada ya round about na huo ukawa usiku wangu wa kwanza ndani ya jiji la Tanga, siku yangu ya kwanza kukanyaga ardhi tukufu ya mkoa wa Tanga.
Kwa kuwa ilikuwa usiku sikuwa na mambo mengi zaidi ya kufanya utaratibu wa kupata sehemu ya kulala na nikiwa nimepanga kulala sehemu karibu kabisa na mji, na ilivyo bahati nzuri au mbaya kwangu na nafsi yangu nilitembelea jiji hili wakati ndugu zangu waislamu walikuwa katika kipindi cha mfungo mtukufu hivyo kwa mara ya kwanza niliingia kwenye mji huu kipindi hasi sana. Na sikutarajia tena kuona au kukutana na yale niliyokuwa nikisimuliwa na watu kuhusu mkoa huu, maajabu yote ni kama yalishapotea kutokana na wakati wenyewe.
"Haya ni masimulizi ya kweli, itaendelea hapa baada ya kuweka sawa kumbukumbu "
Muendelezo unapatikana maoni no 24 chini.
#Allabouttanzanialife 🔴🟠⚪️