Denis Phombeah alikuwa Meneja wa Ukumbi wa Arnautoglu.
Ukumbi wa Atnautoglu ulijengwa na Mgiriki George Arnautoglu.
Denis Phombeah alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Chihota ambae alifariki Uingereza mwaka wa 1952.
Sikupata kulijua jina la kwanza la Mzee Chihota ingawa wanae Raymond na Gershom nilifahamiananao.
Chihota alikuwa amekuja Tanganyika akitokea Southern Rhodesia (Zimbabwe) kuja kutafuta maisha Tanganyika.
Denis Phombeah alikuwa akipenda kula maisha na ile kazi yake ya kuwa meneja Arnautoglu Hall ilimwenea vyema sana kwa kuwa kila Jumamosi Arnautoglu palikuwa pakipigwa dansi.
Ukumbi wa Arnautoglu ilikuwa haingii mtu dansini sharti awe amefunga tai.
George Arnautoglu alikuwa mtu tajiri sana katika nyakati zlle na mal yake alichuma yote Tanganyika.
Kwa kuonyesha shukurai kwa wananchi wa Tanganyika akajenga huo ukumbi kwa ajili ya Waafrika wawe na mahali ambapo wataweza kufanya shughuli zao na vilevile pawe mahali pa buruduani.
Lakini kikubwa alichokuwa kakiweka rohoni kwake ni kuwa George Arnautoglu akiwachukia Waingereza na alipata kuwapa fedha TANU kwa siri ziwasaidie katika shughuli zao za kudai uhuru.
Hili alinieleza Ali Mwinyi Tambwe ambae yeye ndiye aliyepokea fedha hizo.
Denis Phombeah kama walivyokuwa vijana wote wa nyakati zile alikuwa mwanachama wa TAA.
TAA ilikuwa na wanachama ambao hawakuwa Watanganyika ilimuradi ni Mwafrika aliweza kujiunga na TAA.
Wakati waukoloni hii mipaka haikuwa na maana yoyote na ndiyo ilikuwa rahisi sana kwa wananchi wa nchi jirani kuingia nchi nyingine kutafuta kazi.
Labda kama si kwa Denis Phombeah kujitokeza kumfanyia kampeni Julius Nyerere katika uchaguzi wa mwaka wa 1953 Nyerere alipogombea nafasi ya President wa TAA dhidi ya Abdul Sykes na historia hii yake ikaandikwa katika kitabu cha kwanza kueleza historia ya TANU pamoja na safari yake na Ally Sykes kwenda Salisbury, Southern Rhodesia kuiwakilisha Tanganyika katika mkutano ulioitishwa na Kenneth Kaunda, Phombeah asingekuwa sehemu ya historia ya uhuru wa Tanganyika.
Uchaguzi huu ulifanyika Ukumbi wa Arnautoglu mwezi April, 1953.
Ajabu kubwa katika historia ya Julius Nyerere ni kuwa juu ya kuwa hili lilikuwa tukio kubwa sana katika maisha yake na ndilo liilomtia katika uongozi wa TAA kisha TANU hakupata hata siku moja kufungua kinywa chake kulizungumza.
Historia ya Denis Phombeah ipo kwa ufupi sana katika kitabu cha Judith Listowel, ''The Making of Tanganyika,'' (1965).
Historia hii nilikuja kuiandika kwa kirefu katika kitabu cha Abdul Sykes, ''The Life and Times of Abdulwahid Sykes (1924-1968) The Untold Story of the Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika,'' (1998).
Niliweza kukieleza kisa chote kwa uhakika kwa kuwa Ally Sykes alinifungulia nyaraka za familia yao katika historia ya TAA/TANU na katika nyaraka hizi nikakuta nakala za magazeti ya zamani yakieleza mkasa uliowafika Ally Sykes na Denis Phombeah, Salisbury wakiwa njiani kwenda Lusaka, Northern Rhodesia kuhudhuria mkutano uliokusudia kuwakutanisha wapigania uhuru wa nchi za Kiafrika chini ya Jangwa la Sahara.
Lakini kubwa ni kuwa Ally Sykes mwenyewe alinihadithia mkasa huu.
Mazungumza yangu yote na Ally Sykes yalikuwa kwenye cassette na tatizo la cassette ni shida kutunzika.
Mikanda hii yote imepotea.
Ingekuwa starehe sana leo kama ningekuwekeeni ''audio clip'' mkamsika Ally Sykes na ile sauti yake ya kukwaruza akikuhadithieni habari za Denis Phombeah na historia yake na Kenneth David Kaunda.
Nimebahatika kusoma barua walizokuwa wakiandikiana miaka ile ya 1950s.
Itaendelea In Shaa Allah...