Admin Naoma Uiweke Post Yake
Mbunge alia mafao kiduchu kwa wasomi.
Asema wanazidiwa hata na makarani. Akumbuka enzi za Nyerere
Na Joseph Damas, Dodoma.
MBUNGE wa Kyela (CCM) Dk. Harrison Mwakyembe amesema
wahadhiri wa vyuo vikuu nchini hawafundishi vizuri kutokana na kulipwa mishahara midogo, inayozidiwa hata na makarani wa wizara.
Alisema hatua hiyo imesababisha wahadhiri wengi kutumia muda
mrefu katika miradi yao binafsi ili kuweza kujiongezea kipato cha kutunza familia zao.
Dk. Mwakyembe alisema hayo alipokuwa akichangia hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2007/2008 iliyowasilishwa bungeni jana na Waziri, Profesa Peter Msolla.
Alitoa mfano kwamba makatibu wakuu wanapostaafu wanalipwa sh. milioni 172 na kila mwezi wanalipwa zaidi ya sh. milioni moja, tofauti na wahadhiri wa vyuo vikuu ambao wanapostaafu wanalipwa fedha kidogo.
Alitoa mfano wa wahadhiri wa vyuo vikuu wanapostaafu wanalipwa kwa mkupuo sh. milioni 30, kiwango ambacho alisema ni kidogo na ndiyo maana huwalazimu kwenda mitaani kujiongezea kipato.
Dk. Mwakyembe alisema wakati wa utawala wa Baba wa Taifa,
Hayati Mwalimu Nyerere watumishi waliokuwa wakilipwa mishahara mikubwa kuliko wote walikuwa ni wahadhiri na watunza maktaba, lakini sasa mawaziri na makatibu
wakuu wa wizara ndio wanapata mishahara na mafao manono.
Alisema hatua hiyo imechangia
kushuka kwa elimu nchi hasa kwa masomo ya sayansi.
Dk. Mwakyembe alisema wasomi ambao ndio dira kubwa katika kuzalisha elimu bora nchi, wanalipwa mishahara midogo na kwamba, hata wanapostaafu wanapewa marupurupu ya chini kuliko hata makarani wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
"Katika utawala wa Nyerere watu waliokuwa wanalipwa vizuri ni wahadhiri na watu wa maktaba kutokana na kwamba, ndio wazalishaji na waendelezaji elimu nchini.
"Hivi sasa utashangaa mishahara mikubwa ni kwa ajili ya mawaziri na makatibu wakuu, wahadhiri wanalipwa
mishahara midogo sasa wengi hawafundishi vizuri na wanatumia muda mrefu kufanya miradi binafsi," alisema
Dk. Mwakyembe ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Sheria.
Alisema haiwezekani kuingia kwenye dunia ya wasomi kwa kumkabidhi Profesa Msolla gari ambalo halina
matairi na kwamba, kama tutaingia kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki basi tutaburuzwa vibaya.
Akizungumzia kuhusu malalamiko ya mikataba ya madini, Dk. Mwakyembe alisema hatua hiyo inatokana na mikataba hiyo kutopitia kwenye kitengo cha Sheria cha Chuo Kikuu kwa ajili ya kupitiwa na wanasheria wenye fani
yao.
Alisema mawaziri wamekuwa wakipeleka mikataba mikubwa yenye maslahi ya taifa kwenye kampuni za nje kwa sababu ya mikato na kukiacha kitivo cha sheria tofauti na zamani ambapo watalaam wake walikuwa wakishirikishwa kikamilifu.
"Kuna suala la mikato, hii itatumaliza jamani hivi ni virusi. Kama mikataba ya madini ingepitia kwenye kitivo cha sheria kusingekuwa na malalamiko, lakini kwa sababu watu wanapenda mikato," alisema bila kufafanua maana halisi ya mikato.
Katika kuonyesha kukerwa kwake, Dk. Mwakyembe aliweka bayana kuwa, katika bajeti zinazokuja hataunga
mkono wizara ambazo zitapata ushauri wa kuingia mikataba kwenye kampuni binafsi bila kupitia kwa watalaam wa vyuo vikuu.
Dk. Mwakyembe pia alitaka maelezo ya kina kutoka kwa Profesa Msolla kufuatia kusimamishwa kwa ujenzi wa taasisi ya MIST kuwa chuo kikuu na badala yake kujengwa mkoani Arusha.
Naye Wilson Masilingi (Muleba Kusini-CCM) akichangia alisema kwa
kawaida nchi ikiwa masikini basi haitakuwa tofauti na familia masikini, ambayo migogoro ndani ya nyumba ni
kitu cha kawaida.
Alisema wanafunzi wengi nchini wanatoka kwenye familia masikini, hivyo kitendo cha serikali kuwataka
wachangie asilimia 40 na kuwakopesha asilimia 60 hakiwezi kuwasaidia.
Masilingi ambaye alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora katika serikali ya awamu ya tatu, alisema serikali haijachangia elimu kwa
wanafunzi wa vyuo vikuu, kwani huwezi kumkopesha mtu na kujigamba kuwa umechangia elimu yake.
Alisema Rais Jakaya Kikwete aliwahi kuwahakikishia wanafunzi wa vyuo vikuu kuwa, watasoma watoto wote wa
masikini, lakini baadhi ya watendaji wamekuwa wakikwamisha na hivyo ahadi ya Rais kushindwa kutekelezwa.
Masilingi alisema alifurahishwa jinsi
tatizo la mgomo wa wanafunzi wa vyuo vikuu lilivyotatuliwa, lakini alionyesha kushangazwa na tatizo hilo kusababishwa na asilimia 40 ambayo
wanafunzi masikini wanatakiwa kuichangia.
Alisema elimu ndio msingi bora duniani kote, lakini hatua iliyofikia sasa inatia shaka, kwani walimu wengi hawafundishi inavyotakiwa na muda mwingi wanautumia kutafuta fedha mitaani.
Naye Benson Mpesya (Mbeya Mjini-CCM) alionyesha kukerwa kwake na hatua iliyochukuliwa na
serikali ya kutengua maagizo yaliyotolewa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
Alisema Baba wa Taifa aliagiza kuwa Taasisi ya Sayansi na Tekonolijia Mbeya (MIST) iboreshwe na kuwa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia, lakini hivi
karibuni serikali ilikiuka maagizo hayo licha ya maandalizi kufanywa.
Mpesya akionekana mwenye uchungu alihoji hatua ya serikali kuelekeza nguvu zake katika ujenzi wa Chuo
Kikuu kipya cha Nelson Mandela mjini Arusha, ambacho kinategemea fedha za wahisani na kufuta mpango wa
kuifanya MIST kuwa chuo kikuu ambapo tayari kilitengewa fedha na nyingine kutumika kulipa fidia wananchi.
"Mnakiuka maagizo ya Baba wa Taifa, inawezekana mnatafuta laana au nini? Ni lazima tufuate maagizo japo ametangulia mbele za haki, sasa kwanini serikali inakuwa kigeugeu," alihoji Mpesya huku akimuuliza Mwenyekiti wa kikao Jenista Mhagama amwage machozi ama la.
Mpesya aliiomba serikali kubadilisha uamuzi na kuifanya MIST kuwa chuo kikuu kama ilivyoagizwa na watalaamu kutoa baraka zao na kwamba, sababu ilikuwa ni kumuenzi Mandela basi mkoa wa Mbeya ndio unastahili kwa sababu mpigania uhuru huyo aliishi na kusaidiwa na watu wa mkoa huo.
Kwa upande wake, Nimrod Mkono (Musoma Vijijini-CCM), aliiomba serikali kufuta mikopo kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi ili wasome bure.
Mkono ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo alisema wakati umefika kwa serikali kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaochukua masomo ya sanaa tu, huku wale wa sayansi wakisomeshwa bure bila kuangalia daraja.
Alisema nchi nyingi zinaendeshwa kwa mfumo wa sayansi na zimekuwa zikipata maendeleo ya haraka, lakini Tanzania wanafunzi wengi wanakimbilia masomo ya sanaa kwa sababu hakuna maabara.
Mkono alionyesha kushangazwa na wizara, ambayo inahusika na masuala ya sayansi lakini imejaa watendaji ambao si wanasayansi na hivyo kuonekana kama kichekesho kukuza sayansi.
Aliongeza kuwa serikali imejitahidi kujenga shule katika kila kata, lakini akahoji mara watakapohitimu
watakwenda wapi kwa sababu hakuna hata viwanda vya kuweza kuwaajiri kwani, vingi vinamilikiwa na wazungu
na wahindi ambao wanaviendesha kisayansi.