Pokea Pole;
Muumba namtajia, jinale nikianzia
Ni kwake tumetokea, na kwake tutarejea
Punguza kaka kulia, machozi pia futia
Ni kwake tutarejea, ni kwake tumetokea
Habari nimepatia, wakati naperuzia
"Bize bize" mimekua, kijiwe sijapitia
Ni leo nimeonea, ni mama kakuagia
Ni kwake tutarejea, ni kwake tumetokea
Mitihani ya Dunia, "mamenu" kuondokea
Za kwake zilifikia, sikuze hapa Dunia
Ni huko twaelekea, Dunia tunapitia
Ni kwake tutarejea, ni kwake tumetokea
Kwa dua namuombea, peponi aje fikia
Matendo yenu murua, nasema yasaidia
Mtani pole pokea, na ndugu pia jamaa
Ni kwake tutarejea, ni kwake tumetokea
Machungu nayahisia, yakwenu kuwafikia
Tupewacho twapokea, hewala twaitikia
Hakuna tunalojua, Muumba twasubiria
Ni kwake tutarejea, ni kwake tumetokea
Wapole mkono natoa, najuu nanyooshea
Mzidi kuaminia, na dua nawaombea
Dunia tunapitia, na hilo nakumbushia
Ni kwake tutarejea, ni kwake tumetokea
Ni mwisho namalizia, Choveki nawaagia
Simanzi inenijaa, fikira zanizidia
Mikono yatetemea, wakati naandikia
Ni kwake tutarejea, ni kwake tumetokea